Siku kuu ya Tokeo la Bwana, yaani Epifania ni kati ya Sherehe kubwa zinazoadhimishwa
na Mama Kanisa katika Liturujia ya Mwaka wa Kanisa. Mtoto Yesu aliyezaliwa na Bikira
Maria anajifunua kwa mataifa kama Mwana wa Mungu, Masiha na Mwaga wa Mataifa.
Mama Kanisa
katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana, anatangaza pia Fumbo la Pasaka,
linaloonesha kwa namna ya pekee, utukufu wa Kristo kati ya watu wake hadi pale atakapokuja
tena kuwahukumu wazima na wafu. Katika hija ya maisha ya kila siku, waamini wanajitahidi
kumwilisha Fumbo la Ukombozi, kiini cha maadhimisho haya ni Liturujia ya Mwaka wa
Kanisa, lakini kwa namna ya pekee, Siku kuu tatu zinazoonesha: mateso, kifo na ufufuko
wa Kristo kutoka katika wafu, yaani Siku kuu ya Pasaka ambayo kwa Mwaka huu itaadhimishwa
hapo tarehe 5 Aprili 2015.
Kila Jumapili, Mama Kanisa anaadhimisha Pasaka ya
Bwana na kuwawezesha waamini kuendelea kuadhimisha tukio hili kuu katika maisha na
imani yao; kwani Kristo ameshinda dhambi na mauti. Siku kuu ya Pasaka ni chemchemi
ya Siku kuu nyingine zote zinazoadhimishwa na Mama Kanisa. Kipindi cha Kwaresima kwa
mwaka huu, kitaanza rasmi tarehe 18 Mwezi Februari 2015 kwa kupakwa majivu, mwaliko
wa toba na wongofu wa ndani.
Mama Kanisa ataadhimisha Siku kuu ya Kupaa Bwana
Mbinguni hapo tarehe 17 Mei 2015 na Pentekoste, Siku kuu ya kuzaliwa kwa Kanisana
Siku ya Waamini Walei itaadhimishwa hapo tarehe 24 Mei 2015. Jumapili ya kwanza ya
Majilio ambayo kimsingi ni mwanzo wa Mwaka Mpya wa Kanisa, na maandalizi ya ujio wa
Kristo itaadhimishwa hapo tarehe 29 Novemba 2015.
Mama Kanisa anayeendelea
kufanya hija yake hapa duniani anatangaza pia Pasaka ya Bwana, anapoadhimisha Siku
kuu za Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa; Siku kuu za Mitume na Watakatifu mbali
mbali; anapowakumbuka watoto wake waliotangulia katika usingizi wa amani, wakiwa na
tumaini katika ufufuko wa wafu.
Sifa na utukufu kwa Kristo aliyekuwepo, aliyepo
na atakayekuja. Yeye ni Bwana wa Historia na nyakati zote ni zake. Amina.
Padre
Pambo Martin Mkorwe, OSB, a.k.a, Mseminari wa zamani, ndiye aliyesoma ombi kwa lugha
ya Kiswahili katika maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana, Kwenye Kanisa kuu la
Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 6 Januari 2015.
Na Padre Richard A. Mjigwa,
C.PP.S Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.