2015-01-06 10:52:11

Msiwageuzie maskini kisogo!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini kama sehemu ya maandalizi ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo, kuanzia tarehe 15 hadi 19 Januari 2015, linawataka Wakleri kuhakikisha kwamba, wanatoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo na Kanisa lake pamoja na kuendelea kujipambanua kwa njia ya huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani maskini ni hazina ya Kanisa na wanayo nafasi ya pekee kabisa katika moyo wa Baba Mtakatifu Francisko.

Maaskofu wanawakumbusha Wakleri kwamba, mahubiri yao yawe ni sehemu ya ushuhuda wa maisha na utendaji wao wa kazi za kichungaji na kwamba, Upadre ni huduma kwa Familia ya Mungu na wala si cheo wala madaraka. Wakleri kwa njia ya ushuhuda makini, wawe ni mfano wa kuigwa na vijana wa kizazi kipya, kwa kuwaona Mapadre wao wanajibidisha zaidi kwa mambo ya kiroho kuliko kumezwa mno na malimwengu.

Kuna hatari kwamba, Wakleri kutokana na ugumu na changamoto za maisha wakajikuta wakichakarika zaidi kutafuta fedha na mali na kusahau kwamba, wao wamewekwa wakfu kwa ajili ya kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu. Kabla ya kuomba zaka na sadaka, Mapadre waoneshe bidii ya kuwahudumia waamini wao barabara kwa kuwamegea watu Mafumbo ya Kanisa.

Mapadre wawe ni vyombo vya huruma, upatanisho na upendo wa Mungu kwa watu wake; kwa njia hii, waamini wanaweza kupata cheche zitakazowaletea mabadiliko katika maisha yao ya kiroho na kiutu! Sakramenti ya Daraja Takatifu ni kwa ajili ya huduma na kwamba, mageuzi makubwa katika historia ya Kanisa yameanza katika maisha ya Wakleri na Watawa na baadaye kuenea kwa waamini walei. Kumbe, Wakleri ni kitovu cha mageuzi katika maisha na utume wa Kanisa. Mapadre waoneshe moyo wa unyenyekevu na kiasi katika maisha na utume wao!

Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini linawakumbusha Wakleri kwamba, Kanisa nchini humo linaadhimisha Mwaka wa Maskini, unaopania kuwaonjesha maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Maskini, wapate huduma makini kwenye Parokia na taasisi za Kanisa na kama ni kukosea basi wakosee kwa vile wamekuwa wakarimu sana kwa maskini na wala si kinyume chake.

Familia ya Mungu nchini Ufilippini inachangamotishwa kukumbatia na kushuhudia ufukara wa Kristo, kwa kuwa na kiasi, ili waweze kuwa tayari kumpokea na kumtoa Yesu kwa watu wengi zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.