Licha ya kinzani, matatizo na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika Jamhuri ya
Watu wa Afrika ya Kati, lakini kuna haja ya kuhakikisha kwamba, makundi yanayopingana
nchini humo yanaweka silaha chini, tayari kuanza mchakato wa upatanisho, msamaha na
amani inayojikita katika ukweli, uwazi na mafao ya wengi. Kanisa litaendelea kusimama
kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya watu, kamwe halitaogopa wala kunyamazishwa
na watu wachache wanaotaka kuvuruga misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa
kitaifa kwa ajili ya mafao yao binafsi.
Ni maneno makali yaliyotolewa hivi
karibuni na Askofu mkuu Dieudonnè Nzapalainga wa Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Afrika
ya Kati, aliyetishiwa maisha mara baada ya kutembelea kijiji cha Gbangou, ngome ya
kikosi cha waasi cha balaka, ambacho kwa muda wa miaka miwili iliyopita kimeendelea
kupandikiza mbegu ya kifo, chuki na uhasama kati ya wananchi. Balaka na Seleka ni
makundi makubwa yanayotishia amani na usalama tangu mwezi Machi 2013 baada ya Bozizè
kubwaga manyanga baada ya kukumbana na nguvu ya umma iliyomzuia kufanya mabadiliko
katika Katiba ya nchi, ili aendelee kukaa madarakani.
Askofu mkuu Nzapalainga
anasema, kijiji cha Gbangou kinatisha, watu wanaishi na kutendewa kama wanyama, jambo
ambalo kamwe haliwezi kuvumiliwa na wapenda haki na amani duniani, ndiyo maana waliamua
kwenda kutembelea na kujionea hali halisi, ili Serikali na Jumuiya ya Kimataifa, iweze
kuona kile kinachotendeka huko na hatimaye kuchukua maamuzi machungu. Watu wanaendelea
kukabiliana na kifo pole pole kama moto wa kifuu na hakuna mtu anayejali hali kama
hii.
Kama mchungaji na mpenda amani, aliamua kwenda kuwatembelea wanakijiji
hao ili kuwahakikishia kwamba, hata katika mahangaiko na kilio chao cha damu, bado
Mwenyezi Mungu anawapenda na kuwajali, iko siku atawaonesha ile nyota ya matumaini.
Askofu pamoja na ujumbe kutoka Caritas Bangui, walifanikiwa kutoa huduma ya tiba kwa
wagonjwa waliokuwa wamejikatia tamaa na hivyo wakwafanikiwa tena kuwaonjesha imani
na matumaini mapya!
Akiwa njiani, Askofu mkuu Nzapalainga amefanikiwa kukutana
na kuzungumza na viongozi mbali mbali wa kidini, kwa kuwataka kuunganisha nguvu na
sauti yao, ili kutetea maisha, utu na heshima ya watu wanaoendelea kuteseka kutokana
na kinzani pamoja na vita nchini humo. Tangu mwaka 2012, shule nyingi zimeharibiwa
kiasi kwamba, watoto na vijana hawana tena fursa ya kuendelea mbele na masomo, ili
kuwa na matumaini ya kesho iliyo bora zaidi.
Watoto na vijana kama hawa wanapaswa
kumegewa matumaini, kwa kupatia fursa ya kwenda shule ili kujifunza. Umefika wakati
wa kuvuka mipaka ya tofauti zinazowagawa na kuwakinzanisha, ili kutoa kipaumbele cha
kwanza kwa mafao na ustawi wa wananchi wengi, kuliko tabia ya kuendelea kugubikwa
katika chuki, uhasama na ubinafsi uliokomaa kiasi cha kuleta kero na kichefuchefu
kati ya watu!
Askofu mkuu Nzapalainga anawataka wahusika wakuu, kuweka silaha
pembeni na kuanza mchakato wa majadiliano yanayopania kujenga na kudumisha msamaha,
upatanisho wa kitaifa, haki na maendeleo ya wengi. Ni fursa ya kusikilizana katika
ukweli na uwazi kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya wengi, kwani haki na
amani ni mchakato unaochukua muda mrefu kuweza kuonesha matunda yake, lakini lazima
watu waanze kuwajibika. Kila mtu asukumwe na dhamiri safi na nyofu kwa ajili ya kutafuta
na kujenga misingi ya haki na amani, ili kufungua ukurasa mpya kwa ajili ya Afrika
ya Kati!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya Kiswahili ya Radio
Vatican.