Vijana wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè kutoka nchi mbali mbali za Ulaya, waliokuwa
wanakusanyika mjini Prague, nchini Czech, ili kusali, kutafakari na kushirikishana
imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, mwishoni mwaka 2015 watakusanyika Jimbo kuu la
Valencia, nchini Hispania, ili kuwasha moto wa Injili ya Kristo; tangazo ambalo limepokelewa
kwa mikono miwili na Familia ya Mungu, Jimbo kuu la Valencia.
Kardinali Antonio
Canizares wa Jimbo kuu la Valencia, Hispania anawaalika vijana wa Jumuiya ya Kiekumene
ya Taizè kuanza kujinoa tayari kushiriki kikamilifu katika mkutano wao wa thelathini
na nane, utakaofanyika Jimboni mwake. Hii itakuwa ni nafasi ya kukutana na kusali
kwa ajili ya kuombea umoja wa Kanisa, ili kutekeleza amri ya Kristo, ili wote wawe
wamoja, ili walimwengu wapate kuamini na kwa kuamini waweze kuwa na matumaini mapya!
Umati
mkubwa wa vijana umeshiriki katika mkutano wa thelathini na saba uliokuwa unafanyika
mjini Prague, kiasi cha kuwashangaza watu waliokutana nao. Hawa ni vijana waliokuwa
wanatema cheche za furaha, imani na matumaini, huku wakionesha heshima kwa watu na
mazingira.
Vijana wanaoamini na wale wasioamini, walijikuta wakishiriki katika
sala na tafakari, zaidi hata na matarajio ya wale waliokuwa wameandaa tukio hili la
Kikanisa. Vijana hawa ambao walipata hifadhi kwenye familia na taasisi mbali mbali
mjini Pargue, walikuwa wanakusanyika kwenye Makanisa makuu kumi na saba mjini humo.
Fra
Alois ametangaza kwamba, mwezi Aprili 2015, akiwa ameambatana na umati wa vijana wa
Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè, wanatarajiwa kwenda mjini Moscow, Russia, ili kuhudhuria
Siku kuu ya Pasaka ya Waorthodox, ili kuonesha umuhimu wa kushikamana kwa pamoja,
ili walimwengu wapate kuamini!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.