Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo na
kwa mara nyingine tena Heri kwa Mwaka Mpya 2015! Tunawatakia wasikilizaji wote wa
Radio Vatican heri na Baraka katika mwaka huu na nyakati zote. Kumbuka: Muda ni zawadi
kutoka kwa Mungu, mwito kwa kila mmoja wetu kuutumia muda vizuri kwa ajili ya maendeleo
binafsi na kwa manufaa ya wengi.
Basi, karibu
tuendelee kupapasa hati za mtaguso Mkuu wa pili wa Vatikani, kutokamo tuendelee kuhekimishwa
katika yale yenye kutujenga katika maisha yetu ya kumwendea Mungu. Baada ya kuitazama
ile hati iliyohusu daraja ya Mapadre katika Kanisa katika kipindi kilichopita, leo
kwa mantiki tuitazame hati inayohusu malezi ya Waseminari; ijulikanayo kwa lugha ya
kikatini kwa jina la OPTATAM TOTIUS, maana yake kuchagua yaliyo bora.
Mintafaru
malezi ya Waseminari, Mtaguso umegusa maeneo mbalimbali ya malezi kwa majandokasisi
wetu wanapokuwepo Seminarini na pia wanapokuwepo katika mazingira ya nje. Mfumo wa
malezi umeratibiwa kwa hekima kubwa, ili kuweza kuwapata mapadre walioiva vizuri kuweza
kuifaa jamii ya watu wa nyakati zetu. Mfumo huo wa malezi ya kiroho na kitaaluma uliowekwa,
unalengo la kumuunda mseminari katika ukomavu mkamilifu, ili kuweza kumpata padre
aliyekomaa kimwili, kiroho, kiakili, kifikra, kijamii, kisaikolojia na kiutendaji.
Ni kwa mtazamo huo tunaona kwamba, malezi ya Kipadre ni ya kina na yanachukua muda
mrefu wa kutosha.
Mama Kanisa amepanga mfumo huo wa malezi kwa uzito mkubwa,
akijua fika uzito na umuhimu wa huduma ya Kipadre katika Kanisa. Mama Kanisa anataka
wale walioitwa katika huduma takatifu ya altare, waandaliwe vema, ili kweli waweze
kumudu kazi ya kuzinena siri za Kristo, kufafanua mafumbo ya Mungu kwa watu na kuadhimisha
sakramenti za Kanisa kwa ajili ya wokovu wa watu.
Katika hati hii, jumuiya
nzima ya waamini imejukumishwa swala la malezi ya vijana na ustawi wa miito hasa kwa
njia ya sala. Njia ya kawaida ya kuotesha mbegu za miito ni seminari ndogo. Na kwa
nyakati zetu hizi, milango ya miito inachipua sana pia kupitia katika sekondari zisizo
za mlengo wa ki-jandokasisi. Iwe ni seminarini, au nje ya seminari, jambo la msingi
kabisa ni malezi bora, ili pale vijana wetu wenye kuitikia wito wanapoenda katika
majiundo makini katika seminari kuu, malezi hayo ya seminari kuu yawe ni ukuta unaojengwa
katika msingi wa malezi bora ya kiimani na kitaaluma waliyoyapata tangu awali.
Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, umetoa mwangwi mkubwa wa uwajibikaji wa malezi
hayo kwa sisi wakristo wote. Ni jukumu letu kuchochea, kuibua, kukuza na kutunza mbegu
ya wito ndani ya vijana wetu na kuwasindikiza hatua kwa hatua hadi wafikie altare
takatifu ya Bwana. Tunaambiwa sisi Wakristo tutatekeleza wajibu huo vema kwa kuishi
maisha bora ya Kikristo. Tunakubaliana kwamba, sisi kama waamini tunahitaji wachungaji,
na wachungaji hao ni watoto wetu, wanatoka kwetu sisi wenyewe. Hivyo ni wajibu wetu
kuwaandaa vizuri, kushirikiana na taratibu zilizowekwa na Kanisa ili tupate wahudumu
bora wa altare.
Mpendwa Mwana Kanisa la Nyumbani, Mtaguso unatuambia kwamba
‘familia zetu zikiongozwa na roho ya imani, upendo na uchaji wa Mungu, hapo hufanywa
kama ndio seminari ya kwanza kabisa’. Tazama, leo, tunaambiwa kuwa familia zetu ndio
seminari za msingi. Mwito kwa familia kujibidisha kweli kufundisha watoto dini na
maadili na kuwekea mkazo maendeleo ya kitaaluma kuanzia katika shule za msingi, ili
wakifika ngazi ya seminari, wasioone masomo ni magumu na hivyo kuhisi kuwa upadre
ni mgumu.
Mtaguso pia unagusa juu ya uwajibikaji wa Parokia katika malezi ya
waseminari. Tunaelekezwa kwamba, parokia zilete uhai, na vijana wenyewe washiriki
katika malezi yao. Katika mikutano mbalimbali, mada zihusuzo wito mtakatifu zifundishwe
kwa vijana, ili waweze kutambua wito huo na kuufuata kwa hiari. Na mapadre na maaskofu
wetu nao wameelekezwa kuonesha juhudi zao za kitume katika kuiendeleza miito mitakatifu,
na kujibidisha kuivutia mioyo ya vijana waume kupenda maisha ya upadre. Hadi hapo
tunaona jinsi ambavyo sote katika Kanisa tunawajibika katika suala hili muhimu.
Mpendwa
msikilizaji, tukubaliane kwamba, mtu anayejitoa kwa ajili ya kumtumikia Mungu, anatoa
sadaka ya nafsi yake kamilifu. Ndiyo maana kuna vigezo vya kiimani, kiakili, kimwili
na kijamii, kuhakikisha kuwa huyu mtu anafaa kwa ajili ya huduma takatifu. Imetokea
bahati mbaya sana katika nyakati fulani, badala ya kuwatia moyo vijana wetu wasonge
mbele katika njia yao ya kumtumikia Mungu, tukawakatisha tamaa kwa sababu tu za ubinafsi
wetu.
Watoto wetu wakionekana wana akili nyingi, ni sisi wazazi na wanandugu
na watu wengine wasiomtakia Mungu mema, tunawashawishi kwamba, kwa akili nzuri uliyo
nayo hupaswi kwenda Seminari kuu, nenda chuo kikuu usome uajiriwe. Kwa sababu ya tabia
hizo, tutaona kwamba katika seminari ndogo tunakuwa na waseminari wengi, lakini baada
ya malezi ya seminari ndogo na za kati, vijana wanapukutika kwa sababu tele za kupoteza
mwelekeo.
Ni nani aliyesema Upadre hauhitaji watu wenye akili nzuri? Ni nani
alisema wanaokuwa mapadre ni wale walioshindwa maisha? Dhana hizo potovu kutoka kwetu
sisi wenyewe ambao tuna wajibu wa kuwalea vema waseminari wetu, ndio zimewafanya baadhi
ya vijana wazuri waliokuwa na wito haswa wakakata tamaa, na Kanisa linaendelea kukosa
wachungaji. Kwa kufanya hivyo tunalitakia nini Kanisa letu?
Pamoja na maelekezo
ya Mtaguso Mkuu wa II wa Vaticani mintarafu malezi ya waseminari wetu, sisi nasi,
kwa kuzingatia hali halisi ya nyakati zetu, tunaomba tutoe rai kwako mpendwa msikilizaji.
Nyakati zile Kanisa la Missioni lilikuwa linategemezwa kwa kiasi kikubwa sana na Kanisa
la Ulaya. Wafadhili waliweza kulipia masomo ya waseminari na malipo ya waalimu wao
pia. Leo ndugu mpendwa upepo umebadilika! Imani Ulaya imepoa, watu wamepungua kabisa
makanisani na wafadhili hakuna tena.
Ni jukumu langu mimi na wewe, kumsaidia
Askofu wetu kuwasomesha Waseminari hadi wafikie daraja Takatifu. Tunaamini kwa dhati
kwamba tukitaka tunaweza. Parokia nzima haitashindwa kulipa karo ya mseminari mmoja
katika Seminari Kuu kwa miaka yote anayosoma huko.
Pia tunapeleka mwito kwa
watu binafsi, au familia au jumuiya ndogondogo, jisadakeni kwa dhati ili kuweza kumfadhili
kiuchumi mseminari mmoja mmoja kupitia mikono ya Askofu hadi afikie daraja takatifu.
Hakika, tuwe wafadhili wa sala na ada. Wakati mwingine waseminari wetu wanaishi katika
maisha duni na ya kukatisha tamaa hadi inakuwa aibu kuwa mseminari, na hatimaye hufikia
hatua ya kupoteza wito, kwa sababu sisi Wanaparokia kuonekana kwamba hatuwajali, hatuwatunzi
vizuri, hatuna ukaribu wa ukarimu kwao, ni kuwasemasema tu na kuwatishatisha na kuwazulia
majanga ambayo yanawakwamisha katika safari yao. Tuwajenge, tuwatie moyo, wasije wakakata
tamaa.
Wakati mwingine tunasali tu, kumwombea mseminari wetu afikie upadre.
Hilo ni sawa lakini peke yake halitoshi!! Sala pekeyake hazilipi ada wala kununua
madaftari na sabuni. Tuwafadhilie mahitaji yao ya kila siku. Tuamke wapendwa, wakati
ndio huu wa kutupilia mbali blanketi zito lenye ndoto za ufadhili wa Ulaya. Wewe na
mimi ndio wafadhili wenyewe. Tuitikie wito huu wa Mtaguso Mkuu, ili tumpatie Mama
Kanisa Wahudumu wa Altare Takatifu, kwa ajili ya utakatifu wa ulimwengu na wokovu
wa roho zetu.
Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin
Mkorwe OSB (Mseminari wa zamani).