2015-01-05 08:21:27

Adhabu ya kifo imepitwa na wakati!


Askofu mkuu Ignatius Suharyo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Indonesia anasema, maisha ya binadamu ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, hakuna mtu au taasisi yenye mamlaka ya kutoa adhabu ya kifo, kwani adhabu hii inakwenda kinyume kabisa cha haki msingi za binadamu, yaani haki ya mtu kuishi. Kanisa linapinga adhabu ya kifo.

Askofu mkuu Suharyo ametoa tamko hili, hivi karibuni baada ya Rais Joko Widodo kutangaza kwamba, atapambana na wafanyabiashara wa dawa za kulevya hadi kieleweke na wale watakaopatikana na hatia, watakabiliwa na adhabu ya kifo. Askofu mkuu Suharyo anasema, Kanisa linapinga adhabu ya kifo na kwamba, kuna njia mbadala za kuweza kuwawajibisha wahalifu pamoja na kuhakikisha kwamba, haki inatendeka. Adhabu ya kifo, si suluhu ya matatizo yanayotokana na biashara haramu ya dawa za kulevya! Uchu wa mali, madaraka, uchoyo na ubinafsi ni mambo yanayoendeleza biashara haramu ya dawaza kulevya.

Nchini Indonesia, kadiri ya adhabu ya makosa ya jinai, wale wote wanaopatikana na makosa ya mauaji na biashara ya haramu ya dawa za kulevya, wanakabiliwa na adhabu ya kucharazwa viboko adharani na baadaye kupewa adhabu ya kifo. Adhabu ya kifo, ilikuwa imesimamishwa kuanzia mwaka 2008 na tangu mwaka 2013 imeanza kutekelezwa tena na tayari watu watano wamekwisha hukumiwa kunyongwa hadi kufa!

Takwimu zinaonesha kwamba, kuna wafungwa 136 waliotiwa hatiani kutokana na kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya na kati yao kuna wafungwa 64 wanaokabiliwa na adhabu ya kifo kwa kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya; wafungwa wawili wanakabiliwa na kosa la ugaidi na wengine waliobakia wanahusishwa na makosa ya mauaji.








All the contents on this site are copyrighted ©.