2015-01-03 10:21:56

Mawasiliano yelenge kujenga na kudumisha amani na mshikamano!


Wadau mbali mbali katika tasnia ya habari wanasema kwamba, Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican na mkurugenzi mkuu wa Radio Vatican, kupewa Shahada ya heshima ya uzamivu katika sayansi ya mawasiliano ya jamii, ni sawa na “upele kupata mkunaji”, ni kiongozi ambaye ametekeleza dhamana na wajibu wake kwa kujisadaka na majitoleo makubwa bila hata ya kujibakiza. RealAudioMP3

Kitivo cha mawasiliano ya Jamii cha Chuo Kikuu cha Kipapa cha Salesiani, katika maadhimisho ya Jubilee ya miaka 25 tangu kilipoanzishwa, kimetambua na kuona mchango uliotolewa na Padre Federico Lombardi katika tasnia ya habari katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, huu ni umri wa mtu mzima kabisa!

Padre Lombardi alianza kuogelea katika vyombo vya habari akiwa ni mkurugenzi msaidizi wa Jarida maarufu sana linalochapishwa na Wayesuit la “Civiltà Cattolica”, baadaye akateuliwa kuwa mkurugenzi wa Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV; akawa ni Mkurugenzi wa Vipindi na hatimaye Mkurugenzi mkuu wa Radio Vatican na Msemaji mkuu wa Vatican, utume ambao ameutekeleza kwa ari na moyo mkuu, akionesha shukrani kwa karama na mapaji ambayo Mwenyezi Mungu amemkirimia kwa moyo wa unyenyekevu pasi na makuu.

Padre Lombardi katika mhadhara wake, amezungumzia umuhimu wa vyombo vya habari kukazia amani, jambo ambalo limevaliwa njuga na Mababa Watakatifu katika kipindi cha miaka ishirini na mitano iliyopita, kama alivyofanya Mtakatifu Yohane Paulo II hata wakati mwingine akitambua kwamba, ni jambo ambalo si rahisi, lakini alithubutu kulizungumzia kwa ukali na nguvu zote.

Mawasiliano ya kijamii hayana budi kusaidia mchakato wa ujenzi wa amani katika medani mbali mbali za maisha ya binadamu. Vyombo hivi visaidie kuitanabahisha jamii changamoto na ugumu uliopo katika ujenzi wa amani duniani sanjari na kuwaunga mkono wale wote wanaojitahidi kuwa kweli ni vyombo vya ujenzi wa amani. Ujenzi wa amani ni mchakato unaomwilishwa kila siku ya maisha na vipaumbele vya watu, kwa njia ya majadiliano, picha au sauti za watu.

Padre Lombardi anasema, kutunukiwa kwa Shahada ya heshima ya uzamivu katika sayansi ya mawasiliano ya jamii kwake binafsi ni kama kichocheo cha kusonga mbele kwa matumaini zaidi, huku akitambua kwamba, kuna watu wengi mashuhuri na maarufu katika tasnia ya mawasiliano ya kijamii ambao wangestahili kupewa tuzo heshima hii, lakini, Kitivo cha mawasiliano ya jamii, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Wasalesian, kimemwona na kutambua mchango wake katika tasnia ya habari. Padre Lombardi anasema, anamshukuru Mungu kwamba, amethubu kufanya huduma hii kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa na kwamba, anachangamotishwa kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi.

Padre Lombardi anasema, katika mhadhara wake amekazia kwa namna ya pekee umuhimu wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki na amani, kwani mawasiliano kimsingi lazima yapanie kuwaunganisha watu na wala si kutenga watu kwa vita na kinzani za kijamii, kisiasa wala kiuchumi. Mawasiliano yasaidie watu kufahamiana, kuelewana na kusaidiana wakati wa raha na shida.

Kwa njia hii, mawasiliano yanaweza kujikita katika uhalisia wa maisha badala ya kubaki kuwa ni nadharia tu. Mawasiliano yawawezeshe watu kukutana na kutembea kwa pamoja, badala ya kuangaliana kwa “jino pembe”. Ni mawasiliano yanayolenga kujenga umoja na mshikamano kati ya watu, changamoto ya kuondokana na dhana ya kwamba mawasiliano lazima yazue cheche za kinzani na misigano ndani ya jamii. Padre Lombardi anasema, dhana ya namna hii katika mawasiliano ni jambo ambalo linamletea kichefuchefu na kamwe hawezi kukubaliana na mawazo kama haya!

Katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii, lakini Padre Lombardi anasema, ujumbe kwa watu makini umebaki kuwa ni ule ule. Kanisa limeendelea kutangaza Injili, Imani kwa Kristo na Kanisa lake; kanuni msingi za maisha ya kiroho na kiutu; mambo ambayo yanakwenda sanjari na tunu msingi za Kiinjili.

Padre Lombardi anashukuru na kupongeza juhudi zinazofanywa na wataalam katika tasnia ya habari, lakini teknolojia haina budi kuwa ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu; kwa ajili ya kupata hadhira mpya; ili kuhabarisha, kuelimisha, kuburudisha na kufunza. Teknolojia isaidie kufikia umati mkubwa wa watu unaoendelea kuishi pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali.

Radio Vatican katika uhai wake, imejitahidi daima kuvuka vikwazo vilivyowekwa ili kuwafikia watu wengi zaidi, kwa kutumia masafa mafupi na kwa sasa inaendelea kujielekeza zaidi katika matumizi ya mitandao, ili watu wengi waweze kuhabarishwa Injili ya Furaha kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko.

Maendeleo ya teknolojia hayana budi kuwa na lengo maalum, ambalo kwa Mkristo ni kufikisha ujumbe wa Injili kwa Watu wa Mataifa, kwa kujikita katika haki, ukweli na amani, ili kusaidia mchakato wa maendeleo na ukuaji wa mtu mzima: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.