Majadiliano ya kidini yajikite katika maisha ya kila siku!
Askofu Claude Rault wa Jimbo Katoliki la Laghouat Gardaia, nchini Algeria anasema,
Kipindi cha Noeli kwa Wakristo na Siku kuu ya Maulidi kwa waamini wa dini ya Kiislam
ni fursa muafaka kabisa wa kujenga na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini,
ili kudumisha mshikamano wa upendo, haki na amani; mambo msingi yanayomwilishwa katika
uhalisia wa maisha ya watu nchini Algeria.
Siku kuu hizi ziwe ni fursa ya
kuendeleza upendo kwa Mungu na jirani, kwa kushikamana na kusaidiana kwa hali na mali,
licha ya tofauti zao za kidini, kwani yote haya ni mambo yanayopaswa kuwaunganisha
zaidi badala ya kuwajengea chuki na uhasama usiokuwa na mashiko, tija wala maendeleo
kwa wanachi wa Algeria. Majadiliano ya kidini yanapaswa kusimikwa katika maisha ya
kila siku, ili kujenga na kudumisha umoja, udugu na urafiki kati ya Wakristo na Waislam.
Upendo
kwa Mungu na jirani kanuni msingi ambayo waamini wa dini hizi mbili wanapaswa kuizingatia
na ikiwa kama wataimwilisha katika maisha yao ya kila siku, basi hapana shaka kwamba,
amani inaweza kutawala na hivyo kusaidia katika mchakato wa maendeleo endelevu ya
binadamu na ustawi wake.