Askofu mkuu Dieudonnè Nzapalainga wa Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika
ya Kati, hivi karibuni alitishiwa maisha, makazi yake kuchomwa moto hivi karibuni
baada ya kutembelea kambi ya wakimbizi kutokana na mchafuko ya kisiasa yanayoendelea
nchini humo.
Kikundi kinachopingana na Kikosi cha balaka kilimtishia maisha,
lakini hajukali kitu kwani anasema, ni kheri Kiongozi kujisadaka maisha yake, ili
kweli: haki, amani, upendo na mshikamano viweze kupatikana. Vijana wanaotumiwa na
baadhi ya wanasiasa ni kundi linalohitaji majiundo na mshikamano wa kweli, ili kusimama
kidete kulinda na kutetea amani, badala ya kuwa ni vibaraka wa wanasiasa wachache
wanaowatumia kwa ajili ya mafao yao binafsi!
Askofu mkuu Nzapalainga anawataka
waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, kwa
kuonesha upendo na mshikamano kwa watu walioguswa na kutikiswa na vita pamoja na migogoro
na kinzani zinazoendelea nchini humo. Watu wanataka kujenga maisha yao kwa kujikita
katika matumaini, utu na heshima ya binadamu.
Kanisa linapenda kumwilisha
mafundisho yake kwa njia ya huduma ya mapendo kwa Mungu na jirani, ndiyo maana, kuna
haja kwa watu ambao wanaendelea kutishia maisha ya watu kuweka silaha zao chini, huku
wakiongozwa na dhamiri zao nyofu, kuona shida na mateso ya wananchi wengi wasiokuwa
na hatia. Wananchi wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati wanapaswa kushirikiana, ili
kuanzisha mchakato wa ujenzi mpya wa nchi yao, kwa kuendeleza pia upatanisho, msamaha,
haki na amani.
Katika mapambano ya silaha kati ya Seleka na Balaka, zaidi
ya watu elfu mbili wamepoteza maisha yao, na kuna kundi kubwa la watu ambalo limeyakimbia
makazi yake kwa kuhofia usalama wa maisha yake. Katika mazingira kama haya, Kanisa
limeendelea kutoa msaada kwa wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum bila ubaguzi,
kwani linatambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wanapaswa kupendwa,
kuthaminiwa na kuhudumiwa kadiri ya uwezo uliopo!