Wakristo wametikiswa sana huko Mashariki ya Kati, lakini wamebaki "ngangari"
Padre Pierbattista Pizzaballa, Mlinzi mkuu wa Maeneo Matakatifu katika Nchi Takatifu
anasema, Wakristo huko Mashariki ya Kati wametikiswa na kujeruhiwa vibaya sana kutokana
na misimamo mikali ya kiimani, lakini bado wameendelea kuwa imara na thabiti katika
imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kufanyika
huko Mashariki ya Kati vinahatarisha amani, mshikamano na mfungamano wa Jumuiya ya
Kimataifa kwa misingi ya kidini.
Vita na mauaji yanayoendelea huko Mashariki
ya Kati vina malengo mbali mbali yanayofumbatwa na baadhi ya nchi kutoka Ulaya na
kwamba, madhulumu ya kidini dhidi ya Wakristo ni mwendelezo huu, ambao baadhi ya viongozi
wakuu wa dini ya Kiislam wameshindwa kukemea wala kulaani, hadi pale ambapo, Chuo
kikuu cha Kiislam cha Al Azhar, kilichoko Cairo, Misri kiliposikika kikilaani mauaji
ya Wakristo huko Mashariki ya Kati, kiasi cha watu wengi kushikwa na bumbuwazi!
Baba
Mtakatifu Francisko hazungumzii kuhusu vita na machafuko ya kisiasa huko Mashariki
ya Kati, jambo ambalo anaendelea kulipatia kipaumbele cha kwanza ni majadiliano ya
kidini yanayojikita katika ukweli, haki na mafao ya wengi; kama suluhu ya watu kujenga
na kuimarisha amani ya kudumu. Madhulumu na nyanyaso dhidi ya Wakristo huko Mashariki
ya Kati zimewaimarisha zaidi badala ya kuogopa, sasa wanaweza kukabiliana na fumbo
la kifo kwa macho makavu.
Hii ni changamoto kubwa huko Mashariki ya Kati kuhakikisha
kwamba, masuala ya kisiasa kamwe, hayachanganywi na mambo ya kidini, yanayoibua misimamo
mikali ya kiimani, kwani watu wamechoshwa na vita, wanataka kuona haki, amani, upendo
na mshikamano kati ya watu vinatawala. Licha ya magumu yote haya, bado kuna cheche
za matumaini kati ya watu wanaotaka kuona mchakato wa majadiliano ya kidini, kisiasa
na kijamii yanaendelezwa kwa ajili ya mafao ya wengi.
Na Padre Richard A. Mjigwa,
C.PP.S Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.