Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili ambayo imeadhimishwa hivi karibuni
na Mama Kanisa, limekuwa ni tukio la pekee kabisa katika mwendelezo wa Maadhimisho
ya Mwaka wa Watawa Duniani, uliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko.
Baraza la
Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, limezindua mshikamano wa mnyororo
wa sala, unaowataka Watawa wa ndani kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mwaka
wa Watawa Duniani kwa kuchangia kikamilifu katika sala, ili kuchachua maisha na utume
wa watawa ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake, kwa njia ya ushuhuda unaojikita
katika: sala, tafakari, maisha ya kijumuiya na unabii.
Kwa upande wa Italia,
Monasteri ya Mtakatifu Klara, iliyoko mjini Assisi ndiyo iliyokuwa ya kwanza kufungua
mshikamano wa sala katika Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani. Nchini Eritrea,
monasteri iliyochagulia ni ile ya Bikira Maria Aliyepalizwa mbinguni, iliyoko Asmara.
Lengo ni kuhakikisha kwamba, Watawa wa ndani ambao wanajisadaka kwa ajili ya kusali
na kutafakari Neno la Mungu, wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa kuwaombea Watawa
wanaotekeleza dhamana na utume wao sehemu mbali mbali za dunia, ili kwa moyo wa imani
na ujasiri, waweze kweli kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika
maisha yao.