Maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu sanjari na maadhimisho ya Siku
ya 48 ya Kuombea Amani Duniani, ni matukio ambayo yanapaswa kuwaongoza waamini na
watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanatoa kipaumbele cha pekee kwa
uwepo wa Yesu Kristo kati yao, ili aendelee kuwaangaza na kuwakirimia neema na baraka
katika mapito ya maisha yao ya kila siku!
Yesu Mwana wa Mungu aliyezaliwa ni
zawadi inayoonesha kwamba, Mungu anaokoa, changamoto na mwaliko kwa waamini kujikita
katika hija ya toba na wongofu wa ndani, kama chachu ya kukua na kukomaa katika maisha
ya kiroho na kiutu; tayari kujenga na kuimarisha umoja, upendo na mshikamano wa kidugu,
kwa kutambua kwamba, wote ni ndugu na hakuna tena mtumwa, kwani wote wameumbwa kwa
sura na mfano wa Mungu. Katika utu na heshima ya binadamu, Makanisa yanapaswa kuonesha
umoja na mshikamano kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko.
Hii ni sehemu
ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Angelo Scola, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Milano,
lililoko nchini Italia, tarehe Mosi, Januari 2015 ambaye amekazia pamoja na mambo
mengine umuhimu wa kujenga na kudumisha udugu ambao ni kielelezo makini cha uhuru
wa mtu binafsi. Pale dhambi inapobomoa na kuharibu mahusiano kati ya Mungu na mwanadamu,
ubinafsi unachukua na nafasi na hapo ni mwanzo wa mifumo mbali mbali ya utumwa.
Kardinali
Scola anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujikita katika mchakato
wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano; kwa kuondokana kabisa na misimamo
mikali ya kiimani ambayo imekuwa ni Njia ya Msalaba kwa Wakristo huko Mashariki ya
Kati. Ni watu ambao wamejaribiwa sana na vita, dhuluma na nyanyaso, wana woga na kweli
wamechoka sana kutokana na mateso na mahangaiko ya kila siku, lakini imani yao kwa
Kristo na Kanisa lake, bado ni hai na inawawezesha kushinda woga, mchoko na hali ya
kukata tamaa.
Kardinali Scola anawaalika waamini kuendelea kuwa ni wajenzi
wa amani inayojikita katika ukweli, haki, upendo na uhuru wa kweli kama alivyokazia
Mtakatifu Yohane XXIII, ili kujenga dunia mpya, kwa kufanya mabadiliko ya kweli katika
taasisi na mashirika ya kimataifa yaliyopo, ili kukidhi mahitaji msingi ya binadamu
katika ulimwengu mamboleo.
Maadhimisho ya Siku ya Kuombea Amani Duniani, uwe
ni mwanzo wa maandalizi ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani, mateso, kifo na
ufufuko wa Kristo, utimilifu wa Fumbo la Umwilisho, linalopania kumwokoa mwanadamu
kutoka katika lindi la dhambi na mauti!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.