Serikali ya Canada kwa kutambua mchango wa Mtakatifu Yohane Paulo II katika kulinda,
kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani, utu na heshima ya binadamu, imepitisha
sheria inayoanzisha Maadhimisho ya Siku ya Yohane Paulo II, ambayo itaadhimishwa kila
mwaka ifikapo tarehe 2 Aprili, siku aliyofariki dunia, Baba Mtakatifu Yohane Paulo
II.
Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linaipongneza Serikali kwa hatua hii
muhimu ambayo inatambua na kuthamini mchango wa Mtakatifu Yohane Paulo II katika kukuza
na kuendeleza uhuru, utu na heshima ya binadamu. Kwa mara ya kwanza siku hii inaadhimishwa
tarehe 2 Aprili 2015, miaka kumi, tangu Papa Yohane Paulo II alipofariki dunia.
Sheria
hii mpya iliyotungwa nchini Canada inatambua mchango na dhamana iliyotekelezwa na
Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Alisaidia sana mchakato wa majadiliano, haki na amani kati ya watu wa mataifa. Ni
kiongozi aliyekuwa na mvuto wa pekee kwa vijana, kiasi cha kuwahamasisha vijana hao
kuambatana na Yesu Kristo katika maisha yao, kwa kumwilisha mafundisho yake katika
uhalisia wa maisha yao.
Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Yohane Paulo II
alitembelea nchini Canada mara tatu; katika mwaka 1984, 1987 na mwaka 2002. Ni kiongozi
aliyebahatika kutembelea nchi mbali mbali duniani, kiasi hata cha kuchangia kuporomoka
kwa Ukomunisti, Ulaya ya Mashariki.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.