2015-01-01 07:49:14

Msitamani masufuruia ya nyama na vitunguu swaumu utumwani!


Mwenyezi Mungu amependa kujifunua katika historia na nyakati, kama kielelezo cha upendo wake kwa binadamu na kwamba, katika utimilifu wa nyakati, Yesu mwana wa Mungu na Maria akazaliwa ulimwenguni na hivyo nyakati zikawa ni kipindi cha wokovu na neema.

Nyakati zinaelezea hija ya maisha ya mwanadamu, tangu pale anapozaliwa hadi anapoitupa mkono dunia. Mwishoni mwa mwaka, Mama Kanisa anawaalika watoto wake, kuchunguza dhamiri zao, kwa kuangalia mambo makuu yaliyotendeka katika maisha yao, kwa kumshukuru Mungu na kuomba msamaha kwa mapungufu yaliyojitokeza.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Masifu ya Jioni, katika maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu, yaliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumatano tarehe 31 Desemba 2014. Mama Kanisa ameimba utenzi wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, Te Deum, kwa unyenyekevu, kwa kuomba msamaha pamoja na kupokea zawadi mbali mbali kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kanisa linamshukuru Mungu kwa kuwawezesha watu kuwa ni watoto wake wapendwa, ingawa kutokana na dhambi ya asili walijikuta wametengwa na upendo wa Mwenyezi Mungu, kiasi kwamba, mahusiano kati ya Mungu na watoto wake yakaingia dosari, ndiyo maana Mwenyezi Mungu akamtuma Mwanaye wa pekee, Yesu Kristo aje kuwakomboa wanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti kwa kumwaga damu yake azizi. Kwa mwanadamu kumfuata shetani amegeuka na kuwa ni mtumwa wa dhambi.

Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Yesu alitwaa mwili na kuzaliwa na Bikira Maria kwa njia ya Roho Mtakatifu, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi na kumkirimia tena uwezo wa kufanyika kuwa ni mwana mpendwa wa Mungu. Hii ndiyo sababu kubwa ya kuzaliwa Yesu Kristo, Neno wa Mungu, Mungu kweli na Mtu kweli, changamoto ya kujiuliza jinsi ambavyo waamini wanaishi na kutenda katika ulimwengu huu!

Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, kwa kuwa ni watumwa wa dhambi, wanakutana na kikwazo kinachowazuia kuamini kwamba, kweli wanaweza kuota, kuruka na kutumainia, kiasi cha kumfanya mwanadamu hata kama amekombolewa kutoka utumwani, kama ilivyokuwa kwa Waisraeli, kuendelea kutamani masufuria ya nyama na makapu ya vitunguu swaumu kule Misri; hii ni furaha kama moto wa mabua, unaodumu kwa kitambo kidogo.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuchunguza dhamiri zao na kuangilia ubora wa maisha yao ya Kikristo, jinsi wanavyoishi na kutenda, uwepo wao, huduma wanazotoa kwa ajili ya mafao ya wengi na ushiriki wao katika maisha ya kijamii. Kwa waamini wanaoishi mjini Roma watambue thamani kubwa ya Mji wa Roma ambao umejikita katika damu ya mashuhuda wa imani, yaani Mtakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani. Anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi hii kubwa ya kuwa ni Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwamba anatambua dhamana na wajibu wake nyeti kwa ajili ya Kanisa la Kristo, changamoto ya kuendelea kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa.

Baba Mtakatifu Francisko amegusia kashfa iliyoitikisa Manispaa ya Jiji la Roma, kwa baadhi ya vigogo kuhusishwa na wizi wa fedha ya umma iliyokuwa imetolewa na Serikali kwa ajili ya kuwasaidia wahamiaji. Baba Mtakatifu anawataka viongozi na wakazi wa Jiji la Roma kuhakikisha kwamba, wanajenga mji ambao unajikita katika haki na mshikamano kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini waoneshe ujasiri wa kuwalinda na kuwatetea wanyonge badala ya kujilinda dhidi ya maskini; kuna haja ya kuwahudumia maskini badala ya kujihudumia kutokana na umaskini wa watu.

Baba Mtakatifu anasema kwa msisitizo mkubwa kwamba, hazina na utajiri wa Mama Kanisa unafumbatwa katika maskini, wanaopaswa kuhudumiwa kwa heshima na taadhima, lakini pale jamii inapowageuzia kibao maskini na kuanza kuwanyanyasa na kuwadhulumu hata ile haki yao, jamii inaporomoka na uhuru wa kweli unaotoweka na hapo watu wanaanza kutamani masufuria ya nyama na makapu ya vitunguu swaumu ya utumwa yanayojikita katika ubinafsi na hapo kimsingi, ladha ya Ukristo inatoweka kabisa!

Baba Mtakatifu anahitimisha mahubiri yake kwa Mwaka 2014 kwa kumwomba Mwenyezi Mungu msamaha, anazidi kuomba huruma na baraka zake, ili kutembea katika uhuru na kurekebisha makosa yaliyofanyika pamoja na kujiondoa katika utumwa. Mara baada ya masifu ya jioni yaliyoambatana na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na hatimaye, kuimba utenzi wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, Te Deum, Baba Mtakatifu alikwenda kutembelea Pango la Mtoto Yesu, lililoko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.









All the contents on this site are copyrighted ©.