2015-01-01 08:45:36

Amani ya kweli inajikita katika: haki, upendo, ukweli na uhuru!


Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, CENCO, katika maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli na Mwaka Mpya 2015, linawaalika waamini na wananchi wote wa DRC kuonesha furaha na matumaini pamoja na kuendeleza mchakato wa amani na ushuhuda unaojikita katika ujenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho katika mikakati ya shughuli za kichungaji.

Maaskofu wanaishukuru na kuipongeza mihimili ya Uinjilishaji kwa kuendelea kujisadaka kwa ajili ya kutangaza Injili ya Amani hata katika mazingira magumu na hatarishi! Huduma na ushuhuda wao ni nyenzo muhimu katika kuendelea kuimarisha imani na matumaini katika maisha ya waamini nchini DRC.

Baraza la Maaskofu Katoliki DRC katika ujumbe uliotiwa mkwaju na Askofu Nicolas Djomo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki DRC anawataka wadau wa Uinjilishaji kuendeleza mchakato wa kulinda na kutetea haki msingi za binadamu kwa kutambua kwamba, DRC bado inachapisha kurasa chungu katika maisha ya kijamii, kisiasa na hasa wakati huu wanapojiandaa kwa ajili ya kufanya uchaguzi mkuu. Kuna kinzani ambapo zinapata chimbuko lake kutokana na hali ngumu ya kiuchumi pamoja na usimamizi mbaya wa ardhi.

Baraza la Maaskofu linasema kwamba, utawala bora na utawala wa sheria, unaowahakikishia watu haki zao msingi kadiri ya Katiba ya Nchi umepokwa na watu wachache, kiasi cha watu kujitambulisha kutokana na maeneo wanakotoka, jambo ambalo ni hatari kwani linaweza kujenga na kukuza tabia ya ukabila na ubinafsi, sumu ya maendeleo endelevu. Kuna matumizi mabaya ya vyombo vya upashanaji habari, uvunjwaji wa sheria; umaskini wa kutupwa; uchochezi unaofanywa na baadhi ya wanasiasa kwa kuwatumia vijana pamoja na kuendelea kukosekana kwa haki jamii.

Baraza la Maaskofu linalaani kwa kauli moja vitendo vyote hivi na linataka kuwa ni sauti ya watu wasiokuwa na sauti; watu wanaodhulumiwa na kunyimwa haki zao msingi. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanachangamotishwa kuwa kweli ni mashuhuda wa udugu unaopata chimbuko lake kutoka kwa Yesu Kristo. Wajenge na kudumisha mahusiano mema kati yao na Mwenyezi Mungu kwa kutambua kwamba, matumizi ya nguvu na uhalifu ni mambo ambayo yanakwamisha mchakato wa amani.

Baraza la Maaskofu Katoliki DRC linakumbusha kwamba, amani ya kweli inajikita katika mambo makuu manne yaani: haki, upendo, ukweli na uhuru, kumbe, Kanisa Familia ya Mungu Barani Afrika inahamasishwa kujenga jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na utulivu; mambo yanayojionesha katika uhalisia wa maisha ya kifamilia. Kanisa linapaswa kuwa kweli ni mahali pa upatanisho, ili kuwamegea watu huruma ya Kristo, Mfalme wa amani, kwani kwa Mkristo hakuna kuta zinazowatenganisha watu kwa misingi ya ukabila, lugha, jamaa au mahali anapotoka mtu!

Baraza la Maaskofu Katoliki DRC linaitaka mihimili ya Uinjilishaji kuhakikisha kwamba, inaendeleza kwa kasi na ari kuu zaidi mchakato wa kuwafunda vijana, ili kweli waweze kuwa ni wajenzi wa amani; dhamana inayopaswa kutekelezwa kuanzia ndani ya familia. Vijana wa kizazi kipya wafundwe tunu msingi za maisha zinazojikita katika ukweli, haki, upendo na amani, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Maaskofu wanasema, majiundo ya amani miongoni mwa vijana ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, ili waweze kujifunza kuheshimu na kuthamini utawala wa sheria, jambo msingi katika maisha ya pamoja. Upatanisho uwasaidie watu kuvuka kinzani, ili hatimaye, utu, heshima, mafao ya wengi na maendeleo yaweze kupewa msukumo wa pekee, kwa kutambua kwamba, amani ya kudumu ni jina jipa la maendeleo endelevu ya binadamu. Baraza la Maaskofu Katoliki DRC linawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu katika utume wa amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.