Bwana Ban Ki-Moon, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anawapongeza vijana kutoka katika
nchi mbali mbali za Bara la Ulaya wanaokutanika mjini Prague, Jamhuri ya Watu wa Czech,
kwa ajili ya kushiriki katika mkutano wa thelathini na saba wa Vijana wa Jumuiya ya
Kiekumene ya Taizè, changamoto kwa vijana sehemu mbali mbali za dunia kuhakikisha
kwamba, wanajikita katika ujenzi wa umoja na mshikamano kwa kushinda kishawishi cha
utaifa, sera na ubaguzi; mambo amabyo yanawagawa watu.
Wakati huu ambapo dunia
inateseka kutokana na vita na kinzani mbalimbali, kuna haja ya kuwa na vijana wanaokutana
na watu mbali mbali, ili kuanza tena mchakato wa upatanisho unaopania pamoja na mambo
mengine, kudumisha amani na usalama, chachu ya maendeleo endelevu itakayowasaidia
vijana kutumia vipaji na karama zao kwa ajili ya mafao ya wengi. Kuna haja ya kushirikiana
ili Jumuiya ya Kimataifa iweze kufaidika na mawazo na mikakati ya maisha, kwa kuwajibika
zaidi na hatimaye, kuona matunda ya kazi zao.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa
anawataka vijana kujikita katika mikakati ya maendeleo endelevu, wakati huu Jumuiya
ya Kimataifa inapoangalia kwa matumaini mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi
unaotarajiwa kufanyika huko Paris Ufaransa, kunako mwaka 2015. Lengo ni kuweka mikakati
ya kupunguza kiwango cha nyuzi joto ili kufikia walau sentigrade mbili, ili kuepuka
athari za mabadiliko ya tabianchi.
Vijana wanapaswa kuwa ni wadau wakuu katika
mchakato huu unaolenga kujikita katika maendeleo endelevu. Huu ni wajibu fungamanishi
unaojikita katika mshikamano, ili kujenga misingi ya amani, kwa kusimama kidete kulinda
na kutetea haki msingi za binadamu; mahali ambapo utawala wa sheria unaheshimwa!
Katibu
mkuu wa Umoja wa Mataifa anawatia shime vijana kuonesha vipaumbele katika maisha yao
mintafafu: amani, maendeleo na haki msingi za binadamu. Vijana wanahamasishwa kuhakikisha
kwamba, wanashiriki kikamilifu katika maisha ya kijamii, kwa kutoa maoni na kuyatekeleza,
ili kujenga dunia iliyo bora zaidi. Umoja wa Mataifa utaendelea kuwaunga mkono vijana
katika mikakati kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi!
Na Padre Richard
A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.