Tafakari ya Neno la Mungu, Siku kuu ya B. Maria Mama wa Mungu
Mpendwa, unayeitegea sikio Radio Vatican, leo Mama Kanisa anasherehekea sherehe ya
Mama wa Mungu ambayo huja daima kila tarehe mosi ya mwezi Januari.
Ni sherehe
ya amani kwa maana Mama Maria ni mama wa amani. Amemzaa Mkombozi mfalme wa amani na
hivi mama Kanisa anaona ni vema tukasali wakati tunapoanza mwaka tukimwomba Mungu
kwa njia ya Mama huyu kwa ajili ya amani ya ulimwengu. Sherehe hii ya amani iliwekwa
rasmi katia kalenda ya liturujia ya Kanisa na Mwenyeheri Papa Paulo VI kunako mwaka
1968.
Salaam Mama Mtakatifu wa Mungu uliyemzaa mfalme mwenye kutawala mbingu
na dunia daima na milele. Hii ndiyo salaam yetu kwa mama mpendelevu Mama asiye na
doa, katika sherehe hii tukufu tunapofungua mwaka mpya. Amani ni tunda ambalo latupasa
kulipalilia daima katika maisha yetu na hivi katika somo la kwanza toka kitabu cha
Hesabu mwandishi anatufundisha namna ya kutunza amani hasa katika wajibu wetu wa kupokea
baraka zitolewazo na Mungu mwenyewe na hasa kwa njia ya Kanisa.
Si hilo tu
bali hata wajibu wetu sote kuwabariki na kuwaombea wengine. Wajibu huu kwa namna ya
pekee wamekabidhiwa wazazi katika familia. Baba na mama wasisahau wajibu huu nyeti
wa kubariki watoto na kuingiza dhana ya baraka katika makuzi ya watoto wao. Ni kwa
njia ya makuzi na malezi, watoto wataweza kuomba baraka kutoka kwa Mungu na kwa Kanisa.
Mama Bikira Maria ni mama mfano mwema ambaye ametenda yote ili Mwanae akue katika
hekima na maarifa kwa ajili ya kutimiza mapenzi ya Mungu.
Mtume Paulo anapowaandikia
Wagalatia anawakumbusha kuwa Kristo amezaliwa chini ya sheria ili aweze kuwakomboa
waliochini ya sheria na hivi kutii mamlaka kwanza na baadaye kuishinda kwa upendo.
Utii ni amani ambayo leo tunaiomba katika sherehe ya Mama wa Mungu.
Somo la
Injili ni mwendelezo wa Injili ya usiku wa Noeli. Tunaona wachungaji “kiwakilishi
cha waliomaskini” wakiwa wamezunguka pango wakimsujudia Bwana, ambaye anatunzwa na
Maria na Yosefu. Pale hawaoni alama yoyote ya utukufu bali wanamwona Mkombozi masiha
katika nguo za kawaida. Alama hii yatudai kuwa na imani thabiti ambayo haikai katika
kuona bali katika kusikiliza mwaliko wa Mungu moyoni. Wachungaji walipokwisha kumaliza
kazi yao ya kumsujudia Bwana walirudi katika makazi yao wakimtukuza Mungu na kusimulia
habari hiyo ya furaha, habari ya utukufu, habari ya amani.
Yote haya yalipokuwa
yanatendeka Bikira Mama mnyenyekevu alikuwa akiangalia na mwisho tunaambiwa akayaweka
yote moyoni”. Jambo hili maana yake ni nini? Ni kwamba Mama Maria anamwona Mungu katika
yote yanayotokea. Ni tofauti nasi ambao wakati fulani tunataka kumwona Mungu kadiri
ya vionjo vyetu, na hata wakati fulani asipoonekana tunakata tamaa.
Kumbe,
leo tujifunze kuyaweka yote moyoni kama Maria Mama wa Mungu. Kwa akina mama wote Mama
Maria ni mfano wa mama mtulivu na mwenye subira iliyojaa hekima ya Mungu, anayetunza
Familia Takatifu. Kumbe, igeni mfano wake daima kwa ajili ya mafaa ya familia na taifa
la Mungu kwa ujumla.
Ninakutakieni sherehe njema ya Mama Bikira Maria na mwanzo
mwema wa mwaka 2015. Ninatakieni heri Parokia zote zilizowekwa chini ya ulinzi wa
Bikira Maria Mama wa Mungu.
Tumsifu Yesu Kristo na Maria. Tafakari hii imeletwa
kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.