2014-12-30 11:57:59

Iweni chachu ya upatanisho kati ya watu!


Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Cantebury na Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani anawatakia vijana wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè, heri na baraka kutoka kwa Yesu Kristo Mkombozi wa dunia, wakati huu wanapokutana mjini Prague, Jamhuri ya Watu wa Czech, ili kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana wa Taizè kutoka Barani Ulaya kwa Mwaka 2015.

Anasema, nyakati hizi zinashuhudia tofauti zinazosababisha hofu, chuki na uhasama kati ya watu; kumbe mkutano huu wa vijana ni kielelezo cha upatanisho na amani; chachu muhimu sana katika kuharakisha mchakato wa mageuzi, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu amefanyika mwili, ili kuleta mabadiliko katika ulimwengu, ikiwa kama watu wataweza kuambatana na kushikamana na Yesu katika maisha yake, ili kweli waweze kupata nguvu ya kujipatanisha wao kwa wao!

Kwa njia ya Roho Mtakatifu na Fumbo la Pasaka, kila kijana amekirimiwa mabadiliko katika maisha kwa kupita kutoka katika kifo na kuingia katika maisha mapya; kwa kutoka katika giza na kuanza kutembea katika mwanga wa maisha ya Kristo. Licha ya mapungufu yanayojionesha katika maisha ya wanadamu, lakini wanapaswa kukumbuka kwamba, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wakiwa na utu na heshima inayopata chimbuko lake katika Fumbo la Pasaka.

Vijana wanakumbushwa kwamba, wao ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, wapate kuziangaza fadhili zake yeye aliyewaita kutoka gizani, ili waingie katika nuru yake ya ajabu. Kwa watu watakaokubali kielelezo hiki watakuwa ni watu wapya, watu wa Mungu, wasiojitambulisha kwa utaifa, siasa wala mapambano ya kutafuta ukuu.

Askofu mkuu Welby anawataka vijana kuendelea kuwa na ndoto ya kupatanishwa kwa njia ya Roho Mtakatifu, ili kuvuka vikwazo vya kibinadamu; kwa maskini kupata ukombozi; wafungwa kufunguliwa kwao kutoka katika dhuluma, nyanyaso, dhambi, chuki; ulaji wa kupindukia, madeni na woga kwa siku za usoni. Kila mtu anapaswa kufahamu kwamba, amejaliwa uwezo wa kuwa ni raia wa mbinguni, ili kufurahia maajabu ya Mungu.

Vijana wanatakiwa kuendelea kusherehekea kwa furaha huku wakionesha umoja na mshikamano katika tofauti zao, wakifurahi kufanyika kuwa ni watu wake Kristo kwa ajili ya huduma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.