2014-12-30 10:08:13

Acheni ubinafsi na uchoyo!


Baraza la Maaskofu Katoliki Perù katika ujumbe wake kwa Siku kuu ya Noeli linasema kwamba, Kipindi cha Noeli ni muda muafaka uliokubalika mbele ya Mwenyezi Mungu, ni kipindi cha kushirikishana na kumegeana upendo kwa moyo wa ukarimu na majitoleo. Ni wakati muafaka wa kupandikiza mbegu ya upatanisho, msamaha na amani katika mioyo ya watu, kwa kushinda chuki, wivu na mashindano yasiyokuwa na tija wala mashiko kwa maisha na maendeleo ya watu. RealAudioMP3

Noeli ni wakati muafaka kabisa wa kujifunga kibwebwe ili kupambana kufa na kupona na ubinafsi na uchoyo; rushwa na ufisadi mambo ambayo yamekuwa ni sababu ya majanga kwa watu wengi duniani. Umefika wakati wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya wengi badala ya kuelemewa na ubinafsi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Perù pamoja na mambo mengine linapenda kutoa kipaumbele cha kwanza kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; taasisi ambayo kwa nyakati hizi, inakabiliwa na matatizo na changamoto nyingi ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi, ili Kanisa liweze kutoka kifua mbele kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Familia. Upendo umetoweka ndani ya familia nyingi. Kwa masikitiko makubwa kuna watoto ambao hawawezi kuzaliwa kutokana na baadhi ya wazazi kukumbatia utamaduni wa kifo na kutema Injili ya Uhai.

Kuna watoto wanaoishi katika mazingira magumu kutokana na mafarakano ya wazazi wao na matokeo yake wameachana, hivyo watoto wanakosa: upendo, malezi na tunza ya wazazi wa pande zote mbili. Hili ni kundi kubwa la watoto ambalo halina mwelekeo w adira ya maisha. Matokeo kwa watoto kama hawa ni kutumbukizwa katika biashara haram ya binadamu na utumwa mamboleo, mambo ambayo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu na unyama mkubwa ambao unaendelea kupenya kwa kasi katika ulimwengu mamboleo. Watoto hawa wote wanaonesha ile sura ya Mtoto Yesu, wanapaswa kusaidiwa, kulindwa, kupendwa na kutunzwa kwa heshima na upendo mkuu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Perù linasema kwamba, kuna Wananchi wengi kutoka Perù wanaoishi ughaibuni, kwa lengo la kutafuta maisha bora zaidi kwa ajili yao na familia zao, wote hawa wanakumbukwa na Maaskofu katika sala zao, wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Siku kuu ya Noeli. Wakumbuke kwamba, wanahamasishwa kuchangia kwa hali na mali katika mchakato wa ujenzi wa nchi yao kwa kujikita katika misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa; daima wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Maaskofu wanawatakia wananchi wote amani na upendo kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, hakuna mtu yeyote anayetengwa na kazi ya Ukombozi iliyoletwa na Yesu Kristo, changamoto ya kuchuchumilia Injili ya Uhai pamoja na kukuza upendo, mshikamano na udugu kati ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.