2014-12-27 10:40:07

Onesheni mshikamano wa dhati kwa waathirika wa Ebola!


Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwasaidia wananchi wa Afrika Magharibi walioathirika kutokana na virusi vya ugonjwa wa Ebola, ili kusimama tena na kuendelea na shughuli za uzalishaji na utoaji wa huduma. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu 7, 518 wamekwishafariki dunia kutokana na ugonjwa wa Ebola.

Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani anasema, athari za janga la Ebola zimewatikisha wananchi wengi walioko Afrika Magharibi, hasa zaidi, Sierra Leone, Liberia na Guinea. Itakumbukwa kwamba, Kardinali Turkson hivi karibuni ametembelea Afrika Magharibi, ili kuonesha upendo na mshikamano kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa wananchi wa Afrika ya Magharibi ambao wanakabiliwa na madhara makubwa ya ugonjwa wa Ebola.

Monsinyo Robert Vitillo ni mwakilishi wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, hivi karibuni, aliambatana na Kardinali Turkson kwenda katika nchi za Afrika Magharibi zilizoathirika kutokana na virusi vya ugonjwa wa Ebola. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Monsinyo Vitillo anasema kwamba, hali kwa sasa inatishia amani na usalama nchini Sierra Leone na Liberia. Watu wanahofu, shule zimefungwa, watu wanashindwa kufanya kazi na kwa sasa kuna kundi kubwa la watoto yatima ambao wamepoteza wazazi wao kutoka na ugonjwa wa Ebola.

Kuna kundi kubwa la wasichana ambao wamepewa ujazito kutokana na kukosa ulinzi na tunza ya wazazi wao; wasichana ambao kwa hakika wanahitaji msaada wa hali na mali, ili kusonga mbele kwa imani na matumaini, vinginevyo, wanaweza kujikatia tamaa ya maisha katika mazingira hatarishi kama haya! Takwimu zinaonesha kwamba, kuna watoto kati ya 2, 500 hadi 5, 000 ambao ni yatima na hakuna Wasamaria wema wanaotaka kujisadaka kwa ajili ya kuwasaidia kwa kuhofia usalama wa maisha ya familia zao. Kanisa katika maeneo haya limeanzisha mbinu mkakati wa kichungaji ili kuwapatia watoto hawa hifadhi pamoja na kuendelea kuhimiza familia kuonesha upendo, ukarimu na mshikamano kwa kuwatunza watoto hawa.

Ebola ni janga la kimataifa kwani limepelekea watu wengi kukosa fursa za ajira Afrika Magharibi kwa shule, ofisi na viwanda kufungwa kwa kuogopa maambukizi ya Virusi vya Ebola. Wananchi wengi wanakabiliwa na ukata kwani ugonjwa umetikisa mchakato mzima wa uzalishaji na huduma; mambo ambayo yanaweza kuchochea uvunjifu wa sheria kwa baadhi ya watu kutaka kupata njia ya mkato katika maisha.

Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuangalia jinsi ya kuwasaidia wananchi waliokumbwa na virusi vya Ebola katika medani mbali mbali za maisha, kwa kuimarisha huduma za afya, uchumi na uzalishaji, ili waweze kujitegemea na kuwa na matumaini zaidi kwa siku za usoni. Kanisa la kiulimwengu linachangamotishwa kuonesha mshikamano kwa kuyasaidia Makanisa mahalia na Mashirika ya kitawa kuendelea kutoa huduma za kiroho na kimwili kwa wananchi walioathirika kwa ugonjwa wa Ebola. Kipindi cha Noeli, kiwe kweli ni kielelezo cha upendo na mshikamano kwa wananchi waliokumbwa na ugonjwa wa Ebola!







All the contents on this site are copyrighted ©.