2014-12-26 10:51:00

Je, umemwona anavyochefua watu!


Leo ni Sikukuu ya Familia takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Katika sikukuu hii tunapata masomo ya kumtolea Yesu hekaluni. Katika kanisa la mashariki sikukuu ya kumtolea Yesu hekaluni inaitwa "hypapante" yaani Sikukuu ya kukutana, au sikukuu ya maonano.

Katika Sikukuu hii, Mwinjili Luka anatuletea “hypapante” au maonano mbalimbali yanayoweza kujieleza kitaalimungu zaidi kuliko kihistoria. Mathalani, Yesu alisema: “Libomoeni hekalu hili nami nitalijenga kwa siku tatu, Hekalu lililo na maana ya nafsi yake mwenyewe. Kwa hiyo mkutano wa kwanza ni ule wa hekalu hai la Agano Jipya yaani Yesu Kristo mwenyewe au Wakristu, na Yerusalem hekalu la Agano la Kale au waisraeli.

Halafu Yesu ni Neno umbaji la Mungu aliyefanyika mwili (Neno la Agano jipya). Kadhalika ndani ya hekaluni kuliwekwa Torah, yaani Neno umbaji la Mungu la Agano la Kale. Kwa hiyo, mkutano wa pili ni kati ya Neno la Agano Jipya na Torah. Kuna pia kukutana kwa binadamu Yesu na binadamu wenzake waliokusanyika Yerusalemu. Lakini katika mkutaniko huo ni watu wawili tu walioweza kumtambua Yesu kuwa binadamu wa pekee. Watu hao ni mzee Simoni, na bibi Anna binti Fanuel wa kabila la Asher. Watu hawa wanafurahia kumtambua na kumshika na kumkumbatia Mungu aliyejifanya binadamu kama wao.

Tunajulishwa wazazi Yosefu na Maria waliofika hekaluni na sadaka zao nyonge: “Hua wawili au makinda ya njiwa wawili.” (Lk. 7:22-23). Kwa kitendo cha wazazi hao tunapata ujumbe wa kujifunza. Mosi wazazi hawa wanatufundisha kuwa kila mtoto ni mali ya Mungu, wao wamekabidhiwa mtoto wamwandae ili aweze kuishi wito wake alioumbiwa hapa duniani, yaani wamsaidie mtoto wao atimilize ndoto aliyo nayo Mungu kwa huyo mtoto.

Aidha kila mtoto anayezaliwa duniani ni zawadi ya upendo itokayo kwa Mungu kwa ajili ya ulimwengu na kwa binadamu wenzake. Kwa hiyo wazazi wasijimilikishe mtoto huyo na kumkandamiza bali wamtolee Mungu. Aidha, wazazi wanatolea hekaluni njiwa wawili, alama ya ufukara ni tofauti na utajiri wa zawadi ya Mungu anayoupatia ulimwenguni.

Baada ya kutoa sadaka sasa wanaonana na wazee wawili Simoni na Anna. Hao wanawakilisha watu wa Agano Kale waliongojea ujio wa Agano jipya. Yesu alikuwa ni mmojawapo kati ya watoto wengi waliofika kutolewa hekaluni. Kulikoni ni watu wawili tu Simoni na Anna wanaofaulu kumtambua mtoto huyu kuwa ni masiha.

Injili yatuambia kuwa mwenye moyo safi ndiye atakayemwona Mungu. Simoni alikuwa “mtu wa haki na mwenye moyo safi.” Kutokana na usafi wake wa moyo, Simoni anafaulu kuona hadhi na sifa ya pekee ya mtoto kwa macho tofauti na wanavyoona wengine. Aidha Simoni alikuwa na “roho wa Mungu ndani yake.” Huyo roho wa Mungu ndiye aliyemwangazia kuwa asingeona kifo bila ya kumwona Masiha. Kwa njia ya roho wa Mungu Simoni hakuchanganyikiwa na kuvurugwa na mizengwe ya ulimwengu huu.

Sisi kama hatuvurugiki, hatuchafui sauti hii kwa namna yetu ya kuishi na kufikiri, huyo roho anaweza pia kuongea nasi na kutushuhudia. Tujitahidi kumwona roho katika neno lake, katika jumuiya, katika wale wanaoshuhudia Ufalme wa Mungu katika maisha yao, na tutaweza kuigundua sauti ya Bwana.

Kwa vile Simeoni alimsikiliza roho huyo akaweza kumsifu Mungu kwa sababu Mungu amempa utambuzi wa umaana wa maisha yake. Ndiyo maana sasa anasali: “Sasa Ee Bwana wamruhusu mtumishi wake anaenda sehemu ya amani, kwani macho yangu yameona wokovu…” Huyo mzee anatufundisha jinsi ya kuzeeka vizuri. Hatazami nyuma bali mbele.

Kwake yeye kifo kinaleta maana ya maisha yote. Kifo ni hatima ya maisha yaliyokuwa na maana kwani kwa vile yalikuwa daima yanaongozwa na roho. Simeon, analiacha pazia la ulimwengu huu na kuelekea kwenye amani “sasa ni wakati wangu wa kuacha pazia la imani”( Paulo kwa Timoteo). Simeoni baada ya kuona na kushuhudia yote sasa hajifikirii tena mwenyewe, bali anawafikiria watu wote kwamba sasa wamepata wokovu. Ameona mwanga na sasa kwa amani anaenda kupelekea habari njema aliyoiona kwa wale wote waliozaliwa kabla yake na hawakuona huo mwanga. Watu hao ni akina Adamu na Eva, Abrahamu, Isaka, Yakobo na wengineo.

Kisha anawabariki Maria na Yosefu na kutabiri: “Yeye ni ishara ya kuanguka na kufufuka kwa wote katika israeli, na alama ya ukinzani, nawe upanga utakupenya”. Mara nyingi unabii juu ya upanga utakaompenya Maria unaunganishwa na uchungu wa Maria aliposimama chini ya msalaba wa mwanae. Ufasiri huo ni potovu, kwani kazi ya upanga uliotajwa hapa ni kukata na kutenganisha pande mbili kitu kinachokatwa.

Kutokana na wito wa kuushuhudia alio nao mtoto huyu kwa ulimwengu, watu wengine wa ulimwenguni watampokea na wengine watamkataa. Kwa hiyo upanga utakaomchoma Maria anayewakilisha taifa la Israeli ni uchungu utakaowasibu kwa vile wengine kati yao hawatampokea Masiha.

Kwamba wachache watamtambua (watampokea) na wengi hawatamtambua (watamkana). Hata kwa Maria binafsi alijihisi kugawanyika katika safari yake ya imani, kwa vile mambo mengine ya Kristu aliyaelewa mengine hakuyaelewa: “Wazazi wake hawakuelewa waliyoambiwa lakini wakayaweka yote moyoni.” Kadhalika mgawanyiko huo uliwakumba pia mitume wake. Mama Bikira Maria anaitwa mbarikiwa, kwani alikuwa daima kati ya mitume waliokuwa katika sala, wakilisikiliza Neno la Mungu na kulishika.

Kuhusu Nabii wa kike Anna, binti Fanuel wa kabila la Asher. Kabila linalomaanisha mbarikiwa. Lilijiingiza mno katika utajiri wa watu wa mahali walipokuwa kisha likafifia lote. Mama huyu wa miaka 84, aliishi miaka 7 tu na mume wake kisha akabaki mjane mwaminifu kwa miaka mingi bila kuolewa tena. Nambari hiyo ni alama ya ukamilifu ukizidisha namba mbili kamilifu 7 mara 12.

Mwanamke huyu ndiye anayempokea Bwana arusi Masiha Yesu Kristu. Ni ngumu kumpokea Mungu na ni ngumu zaidi kuishi kidhati maisha ya imani kwa Kristu. Tukiwa na moyo safi, tukiongozwa na roho wa Mungu (Kristu) na kudumu tutaweza kumtambua Mungu katika maisha na kumwishi daima.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.