Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi
mema, kutoka kifua mbele ili kuwatangazia na kuwashirikisha walimwengu furaha ya Injili
ya Familia, Mama Kanisa anapoadhimisha Siku kuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria
na Yosefu, inayoadhimishwa tarehe 28 Desemba 2014.
Maaskofu wanaitaka
Familia ya Mungu nchini Hispania kujifunga kibwebwe ili kuinjilisha na kutangaza Injili
ya Familia, kwa kuwa na mwelekeo sahihi kuhusu utu na heshima ya binadamu; upendo
na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Hii ni changamoto kwa waamini na watu
wote wenye mapenzi mema kutambua upendo wa kweli unaojionesha kama wito mtakatifu
kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si katika kuridhisha tamaa na vionjo vya mwili;
mambo ambayo wakati mwingine yanaacha ukakasi, majuto na machungu katika maisha ya
mwanadamu.
Wito wa upendo kati ya Bwana na Bibi unapata utimilifu wake katika
moyo wa mwanadamu, kwa kujikita katika uhuru na furaha ya kweli inayobubujika kutoka
katika undani wa wapendanao. Wito wa upendo ni kiini cha Injili ya Familia wanasema
Maaskofu wa Hispania na ndilo chimbuko la upendo wa Mungu unaomwilishwa katika maisha
ya mwanadamu.
Huu ni upendo unaopania kuendeleza Injili ya Uhai katika maisha
ya mwanadamu mintarafu mshikamano wa upendo kati ya Bwana na Bibi na wala si vinginevyo.
Maaskofu wanasema kwamba, ilimpendeza Mwenyezi Mungu kuchagua fadhila ya upendo kama
njia ya kumshirikisha Bwana na Bibi katika kuendeleza kazi ya uumbaji. Kumbe, upendo,
uaminifu na udumifu kati ya Bwana na Bibi ni kielelezo cha upendo na uaminifu wa Kristo
kwa Mchumba wake, yaani Kanisa.
Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linasema
kwamba, dhamana na utume wa wazazi katika malezi na makuzi ndani ya familia hauna
mbadala. Wazazi wanawajibu wa kuwafundisha na kuwarithisha watoto wao ukweli kuhusu
tunu msingi za maisha ya kifamilia; na taasisi za Kiserikali hazina budi kusaidia
mchakato huu kwa kutunza, kulinda na kuendeleza taasisi ya familia, kwa kutambua kwamba,
Familia inawajibu pamoja na mambo mengine kuhakikisha kwamba, inarithisha imani hai
inayomwilishwa katika uhalisia wa wanafamilia wote, ili kukuza na kuimarisha: furaha,
upendo na matumaini.
Kanisa, kama Jumuiya ya Waamini linakumbushwa kwamba,
linawajibu mkubwa wa kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji, kwani wamepokea na kuonjeshwa
upendo wa Mungu, unaowawajibisha kuwa ni mashuhuda wa upendo mpya ili uweze kuwa ni
chachu inayochachua tamaduni katika ulimwengu mamboleo, ili watu waweze kusimama kidete
kulinda na kutetea upendo wa kweli ambao ni asili ya Injili ya Uhai, kama msingi wa
Jumuiya na maisha ya binadamu.
Mwishoni, Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania
linawaalika kwa namna ya pekee, Familia za Kikristo pamoja na watu wote wenye mapenzi
mema kuonesha ushuhuda wa furaha ya Injili ya Familia katika nyumba zao, Parokia na
Majimbo yao, kwa kuwashirikisha maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii,
furaha, upendo na matumaini mapya yanayobubujika kutoka katika Injili ya Familia!
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.