Salam za Noeli kwa Wananchi wa Korea kutoka kwa Papa Francisko!
Baba Mtakatifu Francisko amewatumia wananchi wa Korea ujumbe wa matashi mema wakati
huu Mama Kanisa anapoadhimisha Siku kuu ya Noeli, huku akikumbuka kwa furaha na shukrani
hija yake ya kitume aliyoifanya nchini humo, mwezi Agosti, mwaka huu.
Baba
Mtakatifu anakumbuka kwa namna ya pekee, maadhimisho ya kukata shoka kwa ajili ya
kuwakumbuka Mashahidi wa imani, mkutano wake na vijana kutoka sehemu mbali mbali za
Bara la Asia na matukio mengine katika hija hii yataendelea kubaki kuwa ni kumbu kumbu
ya kudumu katika maisha na utume wake.
Baba Mtakatifu anasali ili kwamba, mwanga
angavu unaoiangazia dunia kutoka kwa Mtoto Yesu aliyezaliwa Bethlehemu, uijaze daima
mioyo, familia na jumuiya zao. Noeli ni siku kuu ambayo Yesu anapenda kuwavuta watu
kwake kwa njia ya wema wake wa kimungu. Yesu ni mwema, tena mwema sana anasema Baba
Mtakatifu. Uwepo wake pekee unaweza kumkirimia mwanadamu furaha ya kweli, bila Yesu,
hakuna jambo la maana, kwani Yesu ana nguvu ya kufanya yote mapya pamoja na kuwakirimia
watu maisha mapya.
Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini na wananchi
wote wa Korea kusali na kumwombea katika maisha na utume wake, wote anawatakia amani
na utulivu katika kipindi hiki cha Noeli.