2014-12-24 08:33:35

Maisha ya watu wasiokuwa na hatia yanazimishwa kama kibatari!


Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linasema, wananchi wa Canada wanaadhimisha Siku kuu ya Noeli wakiwa wamegubikwa na majonzi ya mauaji ya askari wawili yaliyotokea hivi karibuni nchini humo. Haya ni maisha ya watu wasiokuwa na hatia yaliyozimishwa kama “kibatari”. RealAudioMP3

Lakini bado Nchini Canada kuna matukio mengi ya uhalifu wa kutumia nguvu; utekaji nyara; mauaji ya kutisha; maandamano yenye vurugu na ghasia na uvamizi wa jengo la Bunge. Haya ni matukio ambayo yanaonekana kana kwamba, yamepitwa na wakati, lakini bado yanaendelea kuwaandama wananchi wa Canada katika medani mbali mbali za maisha. Katika mwelekeo kama huu, Canada kamwe haiwezi kujidai kwamba, iko salama, kama ambavyo watu wengi wangelipenda kujisadikisha.

Baraza la Maaskofu Canada linasema kwamba, Noeli ni kipindi cha imani, matumaini na mapendo; ni wakati wa kuchuchumilia unyofu wa ndani na utakatifu wa maisha; tayari kuanza mchakato wa kutafuta unyofu na uadilifu, katika ulimwengu ambao kwa sasa umegauka kuwa kama tambara bovu kutokana na: vita, mauaji ya kutisha, unyonyaji na ukosefu wa haki. Mtoto Yesu ambaye ni Mfalme wa Amani, anawarejeshea tena watu ile ndoto ya kuwa na jamii isiyokuwa na hatia. Ni mtoto mdhaifu anayependa kuwarudishia watu unyofu na uadilifu; anataka kulainisha mioyo ya watu, ili iguswe na upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Umwilisho.

Mtoto Yesu, Mfalme wa Haki na Amani si tu kwamba, ni chemchemi ya ndoto, lakini anawataka watu kufanya maamuzi magumu katika maisha kwa kujitosa kimasomaso kusimamia upendo wa kweli. Yesu ataendelea kukua na kuongezeka kimo na hekima; atakuwa ni Nabii wa ulimwengu mpya ambamo: haki, amani na furaha ya kweli vinatawala.

Alipokuwa Msalabani alikabiliana na Fumbo la Msalaba kwa macho makavu; akajibu kashfa na kejeli kwa huruma na msamaha, changamoto na mwaliko kwa walimwengu kujikita katika mchakato wa upatanisho na uhuru wa kweli. Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Yesu, kilikuwa ni kielelezo makini kwa wafuasi wake kwamba, maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ni neema ya Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Hili ndilo Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, ambalo linaadhimishwa na Mama Kanisa katika maisha na utume wake.

Kwa waamini na watu wenye mapenzi mema, unyofu na uadilifu wa maisha vinaweza kupatikana, kuponywa na kumwilishwa tena katika uhalisia wa maisha ya watu; kwa kuwashirikisha wengine na jamii nzima ya watu. Noeli kiwe ni kipindi cha matumaini kwa kuondokana na woga usiokuwa na mashiko, ili kutakiana kheri na baraka za Siku kuu ya Noeli. Waamini wathuibutu kweli kuimwilisha furaha katika maisha yao ya kila siku.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP. S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.