Rais Jakaya atumbua jipu la kashfa ya Akaunti ya Escrow!
Ifuatayo ni hotuba ya Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania wakati alipozungumza na Wazee
wa Mkoa wa Dar es Salaam, tarehe 22 Desemba 2014. Katika hotuba hii ambayo imevuta
hisia kubwa kwa watanzania ndani na nje ya Tanzania, amegusia mambo makuu mawili:
uchaguzi mkuu wa Serikali za mitaa, kasoro zilizojitokeza na hatua ambazo Serikali
imechukua ili kuhakikisha kwamba, uchaguzi mkuu mwakani, unakuwa huru na salama. Rais
kwa kina na mapana amelipembua sakata la akaunti ya Tegeta Escrow na kubainisha maamuzi
machungu yaliyochukuliwa na Serikali. Lakini jambo la msingi hapa ni kwamba, Rais
ameeleza sakata hiloi katika msingi wa ukweli na uwazi, kwa ajili ya mafao ya taifa.
Wananchi Wenzangu;
Nawashukuru sana wazee wangu wa Dar es Salaam, kwa
kukubali mwaliko wangu na kuja kuzungumza nami siku ya leo. Natambua kuwa taarifa
ilikuwa ya muda mfupi lakini mmeweza kuja kwa wingi kiasi hiki. Naomba radhi kwamba
ilikuwa tukutane Ijumaa lakini kwa sababu zilizo nje ya uwezo wangu tukaahirisha mpaka
leo. Asanteni sana kwa uvumilivu wenu.
Kama mjuavyo, kila ninapoomba kukutana
nanyi ninalo jambo au mambo muhimu kitaifa ambayo napenda kuzungumza nanyi, na, kwa
kupitia kwenu taifa zima linapata habari. Leo nina mambo mawili. Wazee Wangu; Kwanza
kabisa, nataka kurudia kuwashukuru Watanzania wenzangu kwa moyo wenu wa upendo mliouonyesha
kwangu katika kipindi chote cha matibabu yangu nikiwa nje na hata baada ya kurejea
nchini. Kwa kweli nina deni kubwa kwenu. Lazima nikiri kuwa, salamu zenu na taarifa
kwamba watu wamekuwa wananiombea uponaji wa haraka na uzima zinanipa faraja kubwa
na kunitia moyo. Nadhani zimechangia sana kuifanya afya yangu kuendelea kuimarika
kila kukicha. Bado sijawa “fit” kabisa lakini naendelea vizuri. Hali yangu ilivyo
sasa sivyo ilivyokuwa wiki iliyopita au siku niliporejea nchini. Uchaguzi wa Serikali
za Mitaa Ndugu Wananchi;
Jambo la kwanza ninalotaka kulizungumzia leo ni uchaguzi
wa Serikali za Mitaa uliofanyika Jumapili iliyopita tarehe 14 Desemba, 2014 na jana
tarehe 21 Desemba, 2014 katika maeneo ambayo uchaguzi huo uliahirishwa. Bila ya shaka
sote tumesikia taarifa ya awali ya zoezi la upigaji kura iliyotolewa na Mheshimiwa
Hawa Ghasia, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI tarehe 17 Desemba, 2014.
Katika taarifa yake hiyo, Mheshimiwa Waziri alieleza kwamba kwa jumla zoezi limeenda
vizuri kwenye maeneo mengi nchini. Uchaguzi ulifanyika kwa ukamilifu katika Halmashauri
141 kati ya 162. Katika Halmashauri 21 uchaguzi wake uliahirishwa na umefanyika jana
tarehe 21 Desemba, 2014.
Kwa jumla, katika maeneo mengi uchaguzi ulifanyika
kwa salama na amani na hivyo kuwapa wananchi fursa ya kuchagua viongozi wanaowapenda
kuongoza vijiji vyao, vitongoji vyao na mitaa yao. Kufanyika kwa uchaguzi huu ni uthibitisho
mwingine wa kuendelea kukomaa kwa demokrasia nchini. Napenda kutumia nafasi hii kutoa
pongezi za dhati kwa wale wote walioshiriki katika uchaguzi huu kwa maana ya vyama
vya siasa na wagombea. Natoa pongezi maalum kwa walioshinda. Nawaomba sasa wakae chini
kutengeneza mikakati na mipango ya kuwaongoza wananchi wa maeneo yao katika kupata
ufumbuzi wa changamoto za maendeleo na za maisha, zinazowakabili.
Ndugu wananchi; Katika
taarifa yake hiyo pia, Waziri Hawa Ghasia alielezea masikitiko yake kuhusu kasoro
za uendeshaji wa zoezi zilizojitokeza katika maeneo mbalimbali. Aidha, aliahidi kuchukua
hatua stahiki za kinidhamu dhidi ya watendaji na viongozi wa Serikali waliosababisha
kasoro hizo. Alifafanua kuwa miongoni mwa hatua zinazoweza kuchukuliwa ni pamoja na
kufukuzwa kazi, kusimamishwa kazi, kushushwa cheo, kukatwa mshahara au kupewa onyo.
Napenda
kuelezea kufurahishwa kwangu na msimamo huo wa Waziri wa TAMISEMI na nampongeza kwa
hatua alizochukua. Namuunga mkono na namtaka aendelee na msimamo huo katika kukabili
vitendo vya utovu wa nidhamu wa watumishi wa umma. Lazima kila mtumishi wa umma ajue
kuwa asipotimiza ipasavyo majukumu yake kuna adhabu inayolingana na kosa alilofanya.
Isitoshe, watu hao ndio watakaoendesha na kusimamia Uchaguzi Mkuu wa mwakani wakiwa
mawakala na wasaidizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Hivyo basi, kuwajibishwa wale
waliozembea katika uchaguzi, itakuwa fundisho kwao na kwa wengine katika uchaguzi
wa mwaka 2015 na chaguzi nyingine zijazo.
Ndugu wananchi; Kwa upande wa
ghasia, fujo na ugomvi uliotokea wakati wa zoezi la uchaguzi, nimezungumza na viongozi
wa juu wa Jeshi la Polisi na kuwataka kuhakikisha kuwa wale wote waliofanya vitendo
vya kuvunja sheria wanatiwa nguvuni na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Nimewataka
wasifanye ajizi na watu wa aina hiyo. Hawa ni watu hatari ambao hawana budi kuchukuliwa
hatua thabiti za kuwadhibiti na kuwaadabisha. Tusipofanya hivyo tunawakatisha tamaa
raia wema na watiifu wa sheria. Aidha, watu wakikamatwa na kuachiliwa muda mfupi baadae,
wakati mwingine hata bila dhamana ya namna yo yote inawachanganya sana watu wema.
Isitoshe tutakuwa tunalea maradhi ya watu wabaya na kuwafanya waendelee kusumbua jamii.
Nimewakumbusha kuwa wasipokuwa wakali sasa tunaweka mazingira ya hatari ya kuja kutokea
mambo mabaya zaidi mwaka ujao kwenye uchaguzi mkuu.
Sakata la Akaunti ya Tegeta
ESCROW
Ndugu Wananchi; Jambo la pili ninalotaka kulizungumzia si geni masikioni
kwenu, nalo ni sakata la Akaunti ya Escrow ya Tegeta. Bila ya shaka mtakumbuka kuwa
wakati wa kikao cha Bunge la Bajeti mwezi Juni, 2014, kulitolewa madai kuwa fedha
zilizokuwemo katika Akaunti ya Escrow ya Tegeta iliyoko Benki Kuu zimechotwa kinyemela
na mmiliki wa Kampuni ya Pan African Power Solution (PAP) akishirikiana na Maafisa
wa Serikali. Serikali iliahidi kufanya mambo mawili. Kwanza, kumtaka Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa Akaunti hiyo na kwamba
taarifa yake itawasilishwa Bungeni. Na, pili, kumuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi wa mwenendo mzima wa
miamala katika Akaunti hiyo na kama kuna uhalifu wo wote uliopo kwenye mamlaka yake
achukue hatua zipasazo kwa mujibu wa mamlaka na madaraka aliyonayo.
Ndugu Wananchi; Yote
mawili tuliyoahidi tumefanya. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amefanya
ukaguzi wa miamala katika Akaunti ya Escrow ya Tegeta iliyoko Benki Kuu na taarifa
yake ilishawasilishwa Bungeni. Pia niliagiza taarifa hiyo ichapishwe kwenye magazeti
na tovuti ya Serikali ili watu waweze kuisoma. Agizo hilo nalo limetekelezwa. TAKUKURU
wameendelea na uchunguzi wao na watakapomaliza na kuridhika kuhusu makosa yaliyofanywa
watawafikisha wahusika Mahakamani. Mkurugenzi Mkuu wa PCCB alifika kwenye Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali na kutoa baadhi ya mambo kuhusu suala hili aliyoyaona
ni muhimu Kamati iyajue. Mambo Manne Makuu
Ndugu Wananchi; Tarehe 8 Desemba,
2014 nilipoanza kazi baada ya mapumziko ya ugonjwa nilikabidhiwa taarifa mbalimbali
kuhusu sakata hili. Tangu wakati huo nimekuwa nazisoma pamoja na kuzungumza na watu
mbalimbali na kuagiza nipatiwe ufafanuzi wa mambo mbalimbali kutoka kwa wahusika.
Shabaha yangu ni kuyaelewa vizuri mambo hayo ili niweze kufanya uamuzi ulio sahihi
na wa uhakika. Nimebaini kuwa yapo mambo makuu manne:- Akaunti ya ESCROW Miliki
ya PAP kwa IPTL Kodi za Serikali, na Tuhuma za Rushwa Akaunti ya ESCROW
Ndugu
Wananchi; Katika Mikataba ya Kununua Umeme (Power Purchase Agreements) ambayo TANESCO
imetiliana sahihi na kampuni binafsi za kuzalisha umeme za IPTL, SONGAS, SYMBION POWER
na AGGRECO, kuna malipo ya namna mbili yanayofanywa na TANESCO. Kwanza, hulipia umeme
ilionunua kutoka kwa kampuni hizo yaani tozo ya umeme (energy charges). Na, pili hulipia
gharama za uwekezaji uliofanywa na kampuni hizo, yaani tozo ya uwekezaji (capacity
charges). Katika mikataba yote hiyo imekubaliwa kuwa iwapo kutatokea kutofautiana,
au mzozo unaohusu uwekezaji, upo utaratibu wa usuluhishi. Utaratibu huo unataka kwanza
kufanyike mazungumzo, wakishindwa kuelewana watafute mtu wa kuwashauri na kuwasuluhisha;
wakishindwa kukubaliana wapeleke shauri lao kwenye Kituo (Mahakama) cha Kimataifa
cha Usuluhisi wa Migogoro ya Uwekezaji, (International Centre for Settlement of Investment
Disputes – ICSID) kilichopo London, Uingereza.
Ndugu Wananchi;
Mwaka
1998 TANESCO walifikisha kwenye Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya
Uwekezaji, London, malalamiko kwamba gharama za uwekezaji za IPTL ni kubwa mno kuliko
kiasi halisi walichowekeza. Mwaka 2001 Kituo cha Usuluhisi kilifanya uamuzi wa shauri
hilo. Madai ya TANESCO yalikubaliwa kuwa uwekezaji halisi uliofanyika ni Dola za Marekani
127 na siyo Dola milioni 163.17 walizodai IPTL. Kutokana na kupungua huko kwa gharama
za uwekezaji, tozo ya uwekezaji (capacity charges) nayo ilipunguzwa kutoka Dola za
Marekani milioni 3.6 kwa mwezi mpaka Dola za Marekani milioni 2.6 kwa mwezi. Kituo
pia, kilitoa mwongozo kuhusu ukokotoaji wa tozo hiyo.
Ndugu Wananchi;
Miaka
minne baadaye TANESCO ilianza vuguvugu la kutaka kupata nafuu zaidi. Waliamua kugomea
kulipa tozo ya uwekezaji kwa mkokotoo wa mwaka 2001. Nimeambiwa kuwa wanasheria wa
TANESCO walishauri Shirika hilo lidai ukokotoaji kiwango cha tozo ya uwekezaji wa
IPTL ufanyike kwa kuzingatia thamani ya hisa walizolipia wawekezaji ambayo ni shilingi
50,000 badala ya kutumia msingi wa mtaji uliotokana na mkopo wa Dola za Marekani milioni
38.16 wa wanahisa uliotumiwa na usuluhisho wa kwanza ICSID-1. Wakati wakisubiri mchakato
wa usuluhishi wa mzozo huu mpya kuanza, pande zote mbili zilikubaliana kuanzisha Akaunti
ya Escrow ya Tegeta. Tarehe 5 Julai, 2006, akaunti hiyo ikaanzishwa kwa mkataba uliyotiwa
sahihi na IPTL upande mmoja na Wizara ya Nishati na Madini kwa niaba ya TANESCO upande
mwingine. Aidha, Benki Kuu iliteuliwa kuwa wakala wa kutunza akaunti hiyo nayo ilitia
sahihi.
Ndugu Wananchi;
Kwa mujibu wa mkataba huo, Kampuni ya IPTL
iliendelea kupeleka madai ya tozo ya uwekezaji kwa TANESCO ambayo nayo iliwajibika
kulipa madai hayo. Malipo hayo yalitakiwa kupelekwa kwenye Akaunti ya Escrow ya Tegeta
tofauti na ilivyokuwa kabla ambapo yalipelekwa IPTL moja kwa moja. Utaratibu huu mpya
ulikubaliwa kutumika hadi pande mbili zitakapofikia mwafaka kuhusu kiwango cha ukokotoaji.
Kwa upande wa malipo ya gharama ya umeme (energy charges) TANESCO imeendelea kulipa
moja kwa moja kwa IPTL bila kupitia Akaunti ya Tegeta ESCROW maana hizo hazikuwa na
mgogoro.
Ndugu Wananchi;
Kwa miaka saba tangu tarehe 5 Julai, 2006,
akaunti hiyo ilipoanzishwa mpaka tarehe 5 Septemba, 2013, wakati Mahakama Kuu ilipokabidhi
shughuli zote za IPTL kwa PAP, hakuna hatua stahiki zilizochukuliwa kutafuta ufumbuzi
wa mzozo wa tozo ya uwekezaji baina ya ITPL na TANESCO. Pande mbili husika hazikuwahi
kukaa kuzungumza na wala hakuna shauri lililofikishwa kwenye Kituo cha Kimataifa cha
Usuluhishi wa Mogogoro ya Uwekezaji kama ilivyofanyika mwaka 1998.
Wakati
wote huo, TANESCO iliendelea kulipa madai ya tozo ya uwekezaji ya IPTL na kupeleka
malipo hayo kwenye Akaunti ya Escrow. Ulipaji ulisimama katika kipindi kifupi wakati
kampuni ya IPTL ilipowekwa kwenye ufilisi. Kwa mujibu wa taarifa ya CAG, wakati akaunti
hiyo inafungwa tarehe 20 Novemba, 2013, kulikuwa na fedha taslimu shilingi 8,020,522,330.37;
Hatifungani zenye thamani ya shilingi 159,231,370,000 na Dola za Marekani 22,198,544.
Fedha zote hizo ni sawa na shilingi bilioni 202.9.
Ndugu Wananchi;
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo, kama TANESCO ingelipa tozo ya uwekezaji ipasavyo, wakati huo
Akaunti hii ingekuwa na shilingi bilioni 306.7. Kwa sababu ya kutolipa fedha zote
ipasavyo, wakati Akaunti inafungwa TANESCO walikuwa wanadaiwa na IPTL shilingi bilioni
103.8. Kwa mujibu wa Mkataba wa Mauzo ya Umeme (PPA) malipo yaliyocheleweshwa, yanatozwa
riba ya asilimia mbili ya fedha zote ambazo hazikulipwa kwa wakati. Hivyo basi, riba
iliyotokana na TANESCO kuchelewesha malipo ilikuwa Dola za Marekani milioni 33.6.
Ni matumaini yangu kuwa ufafanuzi uliotolewa katika Taarifa ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali unasaidia kuweka kumbukumbu sawa na sahihi kuhusu
kiasi gani kilichokuwepo kwenye Akaunti ya ESCROW siku uamuzi wa Mahakama ulipofanya
akaunti hiyo ifungwe. Kwa kifupi Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali inaeleza kuwa Akaunti hiyo ilikuwa na shilingi bilioni 202.9 na siyo shilingi
bilioni 306.7 kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.
Fedha za Nani: Ndugu
Wananchi; Ni matumaini yangu pia kwamba maelezo haya kwa kiasi fulani yamesaidia
kutoa jibu kwa swali maarufu la fedha za kwenye akaunti hii ni za nani? Je, ni za
umma au za IPTL? Pengine nianze kwa kuelezea Akaunti ya ESCROW ni nini? Akaunti ya
ESCROW ni tofauti na akaunti nyingine tunazozijua katika Benki zetu ambazo mtu anaweka
fedha zake. Kama tujuavyo, katika Benki zipo Akaunti za aina tatu ambazo wengi tunazifahamu
na kuzitumia yaani Akaunti ya Akiba (Savings Account), Akaunti ya Hundi (Current Account)
na Akaunti ya Muda Maalum (Fixed Deposit Account). Akaunti ya Escrow ni akaunti maalum
inayoanzishwa kwa ajili ya kufanya kazi maalum, kwa masharti maalum na kazi hiyo ikiisha
akaunti yenyewe hufungwa. Akaunti hiyo husimamiwa na wakala aliyeteuliwa kwa makubaliano
ya wale wanaofungua akaunti hiyo. Wakala ndiye mwenye jukumu la kusimamia akaunti
na kumlipa mwenye fedha wakati ukifika. Kwa akaunti ya Escrow ya Tegeta pande mbili
husika zilikubaliana kuwa Benki Kuu ndiyo iwe Wakala. Ni muhimu kujua kuwa akaunti
hiyo ingeweza kufunguliwa kwenye Benki yoyote siyo lazima BoT. Akaunti ya Tegeta
ESCROW ilifunguliwa BoT mwaka 2006 kwa ajili ya kuhifadhi fedha za malipo ya tozo
ya uwekezaji (capacity charges) zilizokuwa zinalipwa na TANESCO kabla hazijakabidhiwa
kwa anayelipwa ambaye ni IPTL. Kabla ya hapo TANESCO ilikuwa inalipa moja kwa moja
kwa IPTL. Kama nilivyokwishasema, awali ilifanyika hivyo ili kutoa nafasi kwa pande
hizo mbili husika kumaliza tofauti zao kuhusu kiwango cha tozo ya uwekezaji ya IPTL.
Kimsingi basi, fedha hizi ni za IPTL kwani ndiye mlipwaji na ni malipo yanatokana
na madai ya IPTL kwa TANESCO kuhusu tozo ya uwekezaji. Hata hivyo, kwa mujibu wa CAG,
inawezekana katika fedha hizo kuna fedha za umma. Hi ni kwa namna mbili. Kwanza,
kama mgogoro baina ya TANESCO na IPTL ungetatuliwa na kiwango cha tozo ya uwekezaji
kupungua kama ilivyofanyika mwaka 2001 katika ICSID-1 na kama pande mbili husika zingekubaliana
au kuagizwa kuwa punguzo hilo lianze kuhesabiwa tangu tarehe ilipofunguliwa Akaunti
hiyo (tarehe 5 Julai, 2006), basi kungekuwepo pesa za kurejeshwa TANESCO. Maadamu
hili halikufanyika mpaka Mahakama ilipofanya uamuzi uliosababisha akaunti hiyo kufungwa.
Katika mazingira hayo fedha zote zinakuwa ni za IPTL maana hakuna madai ya TANESCO.
Ndugu
Wananchi;
Namna ya pili ni ile ambapo katika fedha hizi kunaweza kuwepo fedha
za umma na iwapo kuna kodi za Serikali ambazo hazijalipwa. Kwa mujibu wa Taarifa ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kuthibitishwa na TRA ni kwamba kulikuwa
na kodi ya VAT ambayo haikulipwa. Nimeambiwa kuwa TANESCO ndiyo ilikuwa na wajibu
wa kukata kodi hizo kabla ya kulipa madai ya IPTL lakini kwa baadhi ya malipo haikufanyika
hivyo. Hivi IPTL inastahili kudaiwa kodi ya Serikali? Kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa,
kodi inayotakiwa kulipwa na IPTL ni shilingi bilioni 21.7. IPTL wameshapelekewa madai
na TRA, na IPTL wamekubali kulipa. Katika ukaguzi wa Hesabu za TANESCO za mwaka 2012,
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aliwaelekeza TANESCO kuacha kuhesabu
fedha zilizopo kwenye Akaunti ya ESCROW kama ni fedha zao. CAG aliwaambia TANESCO
kwamba fedha hizo si zao.
Maagizo hayo ya CAG yanasomeka kama ifuatavyo: “As
a result, the deposit balance in Escrow account does not meet the definition of an
asset of the Company and therefore an adjustment has been made to de-recognize the
asset and related liability to the tune of the amounts available in the Escrow account”
Kwa tafsiri yake ni kuwa: “Hivyo basi, fedha zilizowekwa kwenye akaunti ya
Escrow hazina sifa ya kutafsiriwa kama ni mali ya kampuni (TANESCO) hivyo, marekebisho
yamefanywa ili kutotambua mali na madeni yanayohusu fedha hizo kwa kiasi cha fedha
zilizopo kwenye akaunti ya Escrow.”
Kutokana na maelezo haya ni dhahiri kwamba,
fedha zilizokuwa kwenye Escrow siyo za TANESCO na hazikupaswa kuingizwa kwenye vitabu
vya TANESCO kama mali yake. Chimbuko la Sakata Wazee Wangu;
Chimbuko la kadhia
yote hii Bungeni na kwenye jamii ni uamuzi wa tarehe 5 Septemba, 2013, wa Mahakama
Kuu ya Tanzania wa kuitambua PAP kuwa mmiliki halali wa IPTL na kuagiza Mfilisi akabidhi
shughuli zote za IPTL kwa PAP. Katika utekelezaji wa uamuzi huo wa Mahakama Kuu ukazuka
mjadala mkali kuhusu fedha zilizomo kwenye akaunti ya ESCROW kukabidhiwa kwa PAP.
Kwanza kabisa mjadala ulikuwa ndani ya Serikali miongoni mwa viongozi na watendaji
wa Wizara na Taasisi zinazohusika moja kwa moja na akaunti hiyo. Hizi ni Wizara ya
Nishati na Madini, TANESCO na Benki Kuu. Viongozi na Watendaji husika walikuwa wanajiuliza
na kuuliza kama walipe au wasilipe. Walipotaka ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali
wakaelekezwa watekeleze uamuzi wa Mahakama Kuu. Alisema uko sawa na hauna matatizo.
Halikadhalika, Benki Kuu walipoulizia kuhusu kodi za Serikali, Mwanasheria Mkuu wa
Serikali alielekeza kuwa hakuna kodi ya kulipwa.
Kwa kuzingatia ushauri wa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, malipo yakafanyika kwa IPTL tena bila ya kodi kulipwa.
Baada ya malipo kufanywa ndipo mjadala huo ukahamia katika jamii na Bunge na kugeuka
kuwa kadhia kubwa iliyochukua sura ya kashfa yenye dalili za rushwa na wizi. Uamuzi
Unaotiliwa Shaka Wazee Wangu na Ndugu Wananchi; Kwa jumla uamuzi wa Mahakama Kuu
kuhusu akaunti ya Escrow, ushauri wa Mwanasheria Mkuu kwa Serikali wa kuelekeza uamuzi
huo utekelezwe na viongozi wa Serikali kutekeleza ushauri huo vimetiliwa shaka. Umeonekana
kuwa haukuwa uamuzi sahihi na kwamba umeitia hasara nchi. Isitoshe uamuzi huo umeibua
hisia za kuwepo harufu na vitendo vya rushwa. Wapo waliosema si bure iko namna! Wapo
waliotaja majina na watu wanaodai wamepata mgao wa Escrow tena wengine wamechukua
fedha kwa viroba, sandarusi na rumbesa. Bahati mbaya sana katika mjadala ilijengeka
dhana isiyokuwa sahihi kwamba jambo hili lilianzishwa na Maafisa hao wa Serikali kwa
nia ya kujinufaisha wao binafsi. Ukweli ni kwamba uamuzi ulifanywa na Mahakama Kuu
na kwenye Serikali ilikuwa utekelezaji wa amri hiyo.
Wazee Wangu;
Nilipokutana
na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupata maoni yake kuhusu kadhia hii ameendelea
kusema alichosema Bungeni kuwa hakukosea katika ushauri wake na wala Mahakama haikufanya
makosa. Hivyo basi, hakuona sababu ya kwenda Mahakamani kuomba marekebisho ya uamuzi
wa Mahakama kuhusu fedha zilizokuwepo kwenye akaunti ya Escrow ya Tegeta kukabidhiwa
kampuni ya PAP mmiliki wa IPTL. Vilevile haoni kama kuna hasara yo yote ambayo nchi
imepata kwa sababu fedha zile ni za IPTL na imelipwa IPTL.
Akifafanua, alisema
kuwa akaunti ya Escrow ilianzishwa kwa ajili ya kutunza fedha za malipo ya tozo ya
uwekezaji kwa IPTL yaliyokuwa yanafanywa na TANESCO. Kabla ya mzozo kuhusu ukokotoaji
wa tozo hiyo na kuanzishwa kwa akaunti ya Escrow ya Tegeta, TANESCO ilikuwa inalipa
tozo ya uwekezaji moja kwa moja kwa IPTL. Baada ya kutokea mzozo na akaunti kuanzishwa
mambo mawili hayakubadilika. Kwanza kwamba IPTL haikuacha kupeleka madai ya tozo ya
uwekezaji kwa TANESCO. Na, pili, kwamba TANESCO haikuacha kulipa madai hayo. Mdai
na mdaiwa hawakubadilika. Kuwepo kwa akaunti ya Escrow hakubadili mwenye fedha zake.
Akaunti hiyo iliundwa kuhifadhi fedha za IPTL wakati suluhu inatafutwa kuhusu kiwango
cha tozo. Matumaini ni kwamba kama kiwango kitapunguzwa, TANESCO inaweza kupata nafuu
ya malipo.
Kuhusu uamuzi wa Mahakama Kuu kuruhusu IPTL ilipwe fedha za akaunti
ya Escrow, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema ni uamuzi sahihi na wala taifa halikupata
hasara kwa sababu pesa zimelipwa IPTL na siyo mtu mwingine. Isitoshe anaona uamuzi
wa Mahakama umeisaidia TANESCO kutua mzigo mkubwa iliyokuwa nao kwa miaka saba. Kama
mjuavyo, akaunti ya Escrow ilianzishwa kuhifadhi pesa za malipo ya tozo ya uwekezaji
ya IPTL. Ilianzishwa kwa matumaini kuwa TANESCO watapata nafuu ya tozo ya uwekezaji.
Lakini, hapakuwahi kufanyika mazungumzo baina ya TANESCO na IPTL kuhusu jambo hilo
na wala suala hilo halijafikishwa ICSID. Haikuweza kufanyika hivyo kwa sababu washauri
wa kisheria wa TANESCO hawajafanya hivyo. Wapo wanaodai kuwa hawafanyi hivyo kwa
sababu hakuna sababu mpya zinazoweza kupatikana kuifanya ICSID ibadili uamuzi wake
wa 2001 kuhusu kiasi cha tozo na namna ya ukokotoaji wake.
Matokeo yake ni
TANESCO kuwa na akaunti ya Escrow ambayo mwisho wake haujulikani. TANESCO inaendelea
kudaiwa na IPTL tozo ya uwekezaji na kulazimika kulipa kwenye akaunti hiyo. Kwa masharti
ya akaunti ya Escrow wanaposhindwa kulipa wanatozwa riba. Kwa mujibu wa taarifa ya
CAG mpaka tarehe 20 Novemba, 2013, TANESCO ilikuwa inadaiwa shilingi bilioni 103.8
ambazo hawajalipa kwenye akaunti ya Escrow na riba ya Dola za Marekani milioni 33.
Kwa sababu hiyo basi uamuzi wa kufunga Akaunti ya Tegeta Escrow unalipatia unafuu
TANESCO dhidi ya kulimbikiza madeni na riba. Kwa upande wa kodi za Serikali ambazo
hazikulipwa, Mheshimiwa Jaji Werema alisema yeye alitoa ushauri tu. Hata hivyo, kama
mamlaka husika inaona zipo kodi zinazostahili kulipwa izidai. Hakuna kilichopotea
kwa sababu anayedai, yaani TRA yupo, na mdaiwa yupo, IPTL.
Uamuzi wa ICSID
II Kuhusu Tozo ya Uwekezaji
Wazee Wangu;
Yalitolewa mawazo kuwa kama
fedha za akaunti ya Tegeta Escrow zingelipwa baada ya uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa
ya Kusuluhisha Migogoro ya Uwekezaji (ICSID II) kutoa uamuzi wake, TANESCO ingepata
nafuu ya kupungua kwa tozo ya uwekezaji. Kuhusu jambo hilo nimeambiwa kwamba kuna
mambo mawili ya msingi. Kwanza kwamba Mahakama hiyo haikutoa viwango vipya vya tozo
kama ilivyofanya mwaka 2001 kwenye ICSID–I. Haikubadili mwongozo wa ukokotoaji wa
tozo. Imesema madai yanaweza kuzungumzwa na kusisitiza kuwa katika mazungumzo hayo
TANESCO watambue kwamba wanahisa waliwekeza mtaji wao binafsi wakati wa kununua mtambo
na pia walikopa madeni, na kwamba kiasi cha fedha walichowekeza kilitakiwa kiwe na
kiwango cha juu zaidi cha faida.
Jambo la pili ni kwamba, shauri hili la pili
la ICSIDI II halikuihusisha kampuni ya IPTL mwenye Mkataba wa Kuuza Umeme na TANESCO
na siyo Benki ya Standard Charterd. IPTL wameweka pingamizi la utekelezaji wa uamuzi
wa shauri hilo hapa nchini, hivyo inakuwa vigumu kwa TANESCO kufanya mazungumzo kwa
msingi wa shauri hilo. Kinga Dhidi ya Madai. Wakati wa kufunga akaunti ya Escrow,
upande wa Serikali ulielezea hofu yake ya uwezekano wa siku za usoni mtu kudai tena
kulipwa fedha hizi hizi ilizolipwa PAP. Nimeambiwa kuwa suala hilo haliwezi kutokea
kwani limetengenezewa wigo imara wa kimkataba kuzuia. PAP imetiliana sahihi na Serikali
kwamba iwapo kutatokea mdai yo yote PAP itawajibika kulipa. Mashaka ya Miliki ya PAP
kwa IPTL
Ndugu Wananchi;
Hofu nyingine kuhusu uwezekano wa Serikali
kupata hasara ni yale madai kuwa huenda miliki ya PAP kwa asilimia 70 za hisa za IPTL
zilizokuwa za kampuni ya Mechmar Berhard ya Malaysia siyo halali. Pale mwanzoni ilidaiwa
kuwa kampuni ya Mechmar ilipouza hisa zake kwa kampuni ya Piper Link ya British Virgin
Islands ilikuwa chini ya mchakato wa ufilisi kule Malaysia. Kama ingekuwa hivyo, kisheria
mtu hawezi kuuza hisa zake akiwa kwenye mazingira hayo. Katika uchunguzi wa CAG alieleza
kuwa amethibitisha kwamba madai hayo si kweli, Mechmar walipouza hisa zao tarehe 9
Septemba, 2010 kampuni haikuwa kwenye ufilisi. Iliingia kwenye mchakato wa ufilisi
mwaka 2012. Lakini kwa upande wa kampuni ya Piper Link ya Uingereza inasemekana
iliuza hisa hizo baada ya kuwa wamepokea amri ya Mahakama ya Malkia ya BVI kuizuia
isiuze hisa hizo. Je ni kweli? Imefanyika hivyo? Kama ni kweli je PAP waliponunua
hisa hizo walijua kama kuna zuio au hapana? Kama walijua basi na wao ni sehemu ya
njama za kufanya udanganyifu. Kama hawakuwa wamejua basi wametapeliwa. Nimeagiza uchunguzi
wa kina ufanyike kupata ukweli.
Natambua hivi sasa Mahakamani zipo kesi zinazohoji
uhalali wa PAP kumiliki asilimia 70 za hisa za Mechmar Berhad. Uchunguzi wetu hautaingilia
mchakato huo lakini unaipa Serikali fursa nzuri ya kuchukua hatua zipasazo kuhusu
suala hili lenye mjadala mkubwa. Jambo lingine muhimu ambalo limeleta matatizo kwa
Mahakama zetu nchini na BRELA ni uuzaji wa hisa za IPTL au kuwekwa rehani hisa hizo
bila ya uamuzi huo kusajiliwa BRELA na kwenye Mahakama zetu. Sheria zetu ambazo ndizo
za nchi ya Jumuiya ya Madola kama ilivyo kwa Hong Kong, Malaysia, na BVI, inaitaka
kampuni ya Piper Link ya BVI iliponunua hisa za Mechmar katika IPTL kusajili BRELA
ununuzi huo. Hali kadhalika, inaitaka SCB ya Hong Kong na kupata amri ya Mahakama
kuzuia deni la Mechmar na kuwekwa dhamana ya hisa za Mechmar katika IPTL. Piper Link
isiuze hisa 70 za Mechmar katika IPTL. Walitakiwa wasajili na BRELA na Mahakama yetu.
Kutokufanya hivyo ndiko kunazua maneno mengi na mzozo kuhusu uuzaji wa hisa hizo kwa
PAP. Kwa SCB wanapata usumbufu wa kudai madeni yao IPTL kwa sababu hiyo hiyo. Uchunguzi
utakaofanyika utapata ukweli wa yote kwa uhakika.
Ndugu Wananchi;
Taarifa
niliyopewa wakati najiandaa kuzungumza nanyi ni kuwa katika Mahakama zetu nchini kuna
mashauri yahusuyo miliki ya PAP ya hisa 70 zilizokuwa za Mechmar katika IPTL na yapo
mashauri yahusuyo PAP kupewa fedha za akaunti ya Escrow. Zipo pia nyingine za masuala
mbalimbali yakiwemo mashauri yaliyofunguliwa na PAP dhidi ya watu, na makampuni binafsi
na vyombo vya Serikali. Naamini uamuzi wa Mahakama zetu utatoa majibu kwa masuala
yote hayo.
Pamoja na hayo yatakayokuwa yanaendelea Mahakamani, Serikali itaendelea
kufanya uchunguzi wake na kuamua namna ya kushughulikia taarifa zitakazopatikana ili
nayo iweze kwenda Mahakamani itakapolazimu kufanya hivyo.
Jambo lingine muhimu
nataka uchunguzi wa kina ufanyike ni kujua nani ni nani katika uuzaji na ununuzi wa
hisa za Mechmar. Hususan nataka tujue kwa ukweli na uhakika hisa hizo zimeuzwa kwa
bei gani. Je, ni kweli gharama zinazosemwa ndizo zenyewe? Nataka kuthibitisha ukweli
huo ili tujue kodi yetu ya ongezeko la mtaji (Capital Gains Tax) inayostahili kulipwa
Tanzania ni kiasi gani? Je kiasi gani kimelipwa na kipi hakijalipwa ili kidaiwe?
Tuhuma
za Kuwepo kwa Harufu ya Rushwa
Wazee Wangu;
Kumekuwepo na tuhuma za
vitendo vya rushwa katika mchakato mzima wa kufunga akaunti ya Escrow na kukabidhi
fedha hizo kwa kampuni ya PAP. Halikadhalika, kumekuwepo na hisia hizo hizo kwa upande
wa jinsi kampuni ya VIP Engineering and Marketing ilivyotumia pesa zake zilizoko kwenye
Benki ya Mkombozi. Yamesemwa mengi sana na mmeyasikia na kuyasoma.
Rushwa
ni kosa la kijinai ambalo kwa Serikali yetu ni kosa ambalo ni vigumu kulivumilia wala
kulifumbia macho. Mara baada ya kupata fununu za uwezekano wa vitendo hivyo kufuatia
taarifa ya awali ya CAG ya kwenda kukagua miamala, niliagiza taarifa husika zifikishwe
kwenye Taasisi ya Kupamba na Kuzuia Rushwa (PCCB) kwa uchunguzi zaidi. Naambiwa taarifa
hizo zimefika na kazi ya uchunguzi inaendelea. Tayari watu kadhaa wamehojiwa na wengine
wanaendelea kuhojiwa. Wakati nawasihi wananchi kuvuta subira ili tuwape nafasi PCCB
wakamilishe kwa ufanisi wa hali ya juu kazi yao waliyokwishaianza, nawaomba PCCB waongeze
kasi ya uchunguzi.
Napenda kufafanua kwamba kwa upande wa miamala iliyotoka
katika akaunti ya kampuni ya VIP Engineering and Marketing ya Ndugu James Rugemalila,
Serikali inashughulika na watumishi wa umma kwa kuzingatia Sheria ya Maadili ya Utumishi
wa Umma, maana suala lao ni la kimaadili. Hatuwahoji wasiokuwa watumishi wa umma.
Maazimio ya Bunge
Ndugu Viongozi;
Wazee Wangu;
Ndugu Wananchi;
Niliona
nianze kwa kutoa maelezo hayo ya utangulizi kabla ya kuyazungumzia maazimio ya Bunge.
Serikali imepokea maazimio hayo ya Bunge na kuyafanyia kazi kwa ajili ya utekelezaji
wake. Nawapongeza Wabunge wetu kwa moyo waliouonesha wa kuchukia maovu na kutaka yashughulikiwe
ipasavyo. Napenda kuwahakikishia kuwa niko pamoja nao. Nampongeza Mheshimiwa Anna
Makinda, Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai, Naibu Spika na Mwenyekiti wa Bunge
Mheshimiwa Mussa Zungu kwa uongozi wao mahiri. Hakika haikuwa kazi rahisi, lakini
chini ya uongozi wao mambo yameisha salama na tumepata maazimio nane yanayozungumzika
na kutekelezeka.
Nawashukuru na kuwapongeza sana Wajumbe wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), chini ya uongozi wa Mheshimiwa Zitto Kabwe na
Mheshimiwa Deo Filikunjombe na pia Wajumbe waliounda Kamati ya Mapendekezo kwa kufikia
mwafaka wa mapendekezo haya 8 ambayo yaliazimiwa na Bunge.
Mwisho lakini si
ya mwisho kwa umuhimu, nawapongeza Wabunge wote kwa michango yao mizuri. Jambo lililonifurahisha
sana ni ushirikiano wa Wabunge wa kambi zote katika kutafuta ufumbuzi wa suala hili
muhimu,. Hivi ndivyo inavyotakiwa Bunge liwe. Kwa kweli lazima nieleze mshangao wangu
niliposikia kambi ya upinzani ikijaribu kufanya maamuzi yale ni yao wao na wenzao
hawamo. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali ina Wajumbe 19 wa CCM na wa
Upinzani 5. Bunge lina Wabunge wa CCM asilimia 74 na wa upinzani asilimia 26. Hivi
kama ni yao wao pekee na wa upande wa CCM wangepinga yangekuwa? Yasingefika po pote,
yangefia kwenye Kamati. Huku ni kutafuta umaarufu kwa mgongo wa wengine. Na, Wabunge
wengi wa CCM na nyie semeni msikike kwa uamuzi mliyofanya wote.
Napenda kuwahakikishia
kuwa mimi na wenzangu Serikalini hatuna upungufu wa dhamira ya kutekeleza yale maazimio
yanayoangukia katika dhamana yetu. Napenda kuainisha mtazamo na mwelekeo wa Serikali
katika utekelezaji wa maazimio hayo manane kama ifuatavyo:-
Azimio la kwanza:
Serikali iangalie uwezekano wa kuchukua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha
kwa TANESCO kwa mujibu wa Sheria za nchi. Pendekezo tumelipokea, ni jambo linalowezekana
kufanya. Hata hivyo, tunapopima ujumbe tunaoupeleka kwa jumuiya ya wawekezaji tunachelea
kuwa inaweza kuleta hofu na kuwatisha wawekezaji waliopo na wajao. Nalisema hivyo
kwa sababu sisi tuna historia ya kutaifisha mali za kamapuni binafsi. Hofu hiyo bado
ipo. Tukichukua mitambo hii tunaweza kurudisha hofu za kurudi tulikokuwa na kukimbiza
mitaji tunayohitaji kwa uchumi kukua na nchi kupata maendeleo. Nashauri tuendelee
kuyapatia ufumbuzi matatizo ya IPTL kila tunapoyabaini. Aidha, Mahakama imetusaidia
sana kwa kuamuru mitambo ya IPTL ibadilishwe ili itumie gesi asilia na kutoza bei
ya umeme isiyozidi senti nane za Marekani. Tuyafuatiliye haya kwanza.
Azimio
la Pili: Azimio hilo linazungumzia kuhusu uwazi wa Mikataba linasomeka ifuatavyo:
“Bunge limeazimia kwamba Serikali itekeleze Azimio husika la Bunge mapema iwezekavyo
na kwa vyovyote vile kabla ya kumalizika kwa Bunge la Bajeti. Serikali iwasilishe
taarifa ya utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya umeme”. Azimio hili tumelipokea na
tunaangalia namna bora ya kulitekeleza ili kuweza kuua ndege wawili kwa jiwe moja.
Kwanza, kuitikia kilio cha muda mrefu kuhusu uwazi katika mikataba ambayo Serikali
inaingia na wawekezaji; na pili kuhakikisha usiri wa mikataba hiyo ambayo ni haki
ya wawekezaji hao dhidi ya washindani wao inazingatiwa. Serikali na Bunge tutakaa
chini hivi punde kutafuta namna bora ya kisheria na tutafanya hivyo kwa kujifunza
pia kutokana na uzoefu wa nchi ambazo zina utaratibu wa aina hii.
Azimio
la Tatu: Linasomeka; “Bunge linaazimia kwamba TAKUKURU, Jeshi la Polisi na vyombo
vingine husika vya ulinzi na usalama vichukue hatua stahili kwa mujibu wa sheria za
nchi yetu dhidi ya watu waliotajwa kwenye taarifa maalum ya Kamati husika na vitendo
vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya Akaunti ya ESCROW, na watu wengine watakaogundulika
kufuatia uchunguzi mbalimbali unaoendelea kuhusu kuhusika kwao katika vitendo hivyo
vya jinai” Vyombo husika vimekwishaagizwa kufanya hivyo na kazi imeanza na inaendelea.
Ikiwa wapo watu wenye makosa hatua zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria.
Azimio
la nne: Linasomeka, “Kamati za Bunge kuwavua nyadhifa zao wenyeviti wa Kamati za Bunge
waliotajwa kupewa fedha na kampuni ya VIP Engineering kabla ya kikao kijacho cha Bunge”
Azimio hilo liko chini ya mamlaka ya Bunge lenyewe. Nawaachia wao waamue.
Azimio
la Tano: Linasomeka; “Bunge linaazimia kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
aunde Tume ya Kijaji ya Uchunguzi kuchunguza utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius
Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania” Azimio hili
nimelipokea, tumelijadili hata hivyo, itabidi tufuate utaratibu wa kikatiba na kisheria
wa kushughulikia masuala ya namna hiyo. Inatakiwa suala kama hili lianzie kwenye Mhimili
wa Mahakama yenyewe na siyo kwa Rais au Bunge. Tume ya Mahakama ndiyo yenye mamlaka
ya kumtaka Rais aunde Tume ya Kijaji ya kumchukulia hatua Jaji yeyote pale inaporidhika
kuwa amepoteza sifa za kuendelea kufanya kazi hiyo. Nashauri suala hili tumuachie
Jaji Mkuu wa Tanzania alishughulikie atakavyoona inafaa.
Azimio la Sita:
“Bunge linaazimia kwamba mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi kuitaja Stanbic
Bank Ltd. na benki yeyote itakayogundulika kufuatia uchunguzi wa mamlaka ya uchunguzi,
kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika akaunti ya ESCROW kuwa ni
taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu (Institutions of money laundering
concerns). Pendekezo la Bunge ni zuri kwamba mamlaka husika na udhibiti wa vitendo
vya utakatishaji fedha vifanye uchunguzi kwa mujibu wa Sheria. Serikali imelipokea
na mamlaka husika yaani Financial Intelligence Units kulishughulikia. Naamini wameshaaza,
tuwape muda watimize wajibu wao kwa mujibu wa sheria.
Azimio la Saba:
“Bunge liliazimia kwamba Serikali iandae, na kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya
Sheria iliyounda TAKUKURU kwa lengo la kuanzishwa Taasisi mahsusi itakayoshughulikia
kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia
uhai wa taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa. Kazi ya kufanya mageuzi katika TAKUKURU
inaendelea. Tayari Sheria mbalimbali zimetungwa ikiwa ni pamoja na Sheria Mpya ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2008, Sheria ya Kudhibiti Matumizi ya Fedha
Haramu ya mwaka 1991 ambazo zote zinaweka utaratibu wa kushughulikia vitendo vya rushwa.
Tutaendelea kuziboresha sheria hizo kwa kadri itakavyohitajika. Kazi iliyopo
mbele yetu ni kuimarisha usimamizi wa sheria hizo. Jambo hilo nalo litazingatiwa katika
maboresho hayo. Ni dhamira yangu na ya Serikali ninayoiongoza kupambana na kushinda
vita dhidi ya rushwa. Kwa hiyo tuko tayari kulifanyia kazi pendekezo lolote linaloimarisha
dhamira yetu hii njema.
Azimio la nane: “Bunge linaazimia kwamba Waziri
wa Nishati na Madini, Waziri wa Ardhi na Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi ya
Wakurugenzi ya TANESCO wawajibishwe kwa kuishauri mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi
wao. Azimio hili ndilo Azimio ambalo limevuta hisia za watu wengi, na pengine ndilo
ambalo utekelezaji wake unasubiriwa kwa hamu. Utekeelzaji wake umeanza. Kwanza, ni
kuhusu Bodi ya TANESCO, tumeanza mchakato wa kuunda Bodi mpya kwani iliyopo imemaliza
muda wake. Kuhusu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, kwa vile ni mtumishi
wa umma anatawaliwa na Sheria na Kanuni za Utumishi wa umma, hivyo nimeshaelekeza
Mamlaka kuchunguza tuhuma zake na hatimaye ikibainika ana makosa hatua za kinidhamu
zitachukuliwa. Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameshajiuzulu. Tumelitafakari suala la
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi la kupokea fedha kutoka VIP Engineering
and Marketing ambazo kwa maelezo yake ni kwa ajili ya shule anayoimiliki na kuiendesha.
Mwenyewe ameeleza wazi kupitia vyombo vya habari. Pamoja na hayo yapo mambo ya msingi
kimaadili ambayo hayakuzingatiwa, hivyo tumemwomba atupishe tuteue mwingine. Kuhusu
Prof. Muhongo nimemuweka kiporo, kuna uchunguzi niliagiza ufanywe na vyombo vyetu
bado nasubiri taarifa hiyo ili nifanye uamuzi ndani ya siku chache zijazo.
Hitimisho Wazee
Wangu; Nawashukuruni kwa kunisikiliza.