2014-12-23 10:20:08

Askofu Niwemugizi anena!


Ifuatayo ni tafakari kutoka kwa Askofu Severine Niwemugizi, wa Jimbo Katoliki Rulenge- Ngara anapoyaangalia matukio kadhaa yaliyoigubika Jamii ya Watanzania katika Kipindi cha Mwaka 2014, tayari kujisahihisha na kujiwekea mikakati ya kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, ukweli na uwazi, daima mafao ya wengi yakipewa kipaumbele cha kwanza. Watanzania wajifunze kusema na kutetea ukweli, unaweza kuendelea zaidi kwa raha zako mwenyewe!

Ninapenda kuanza makala haya na ujumbe wa Noeli, “Msiogope kwa kuwa Kristo analeta habari njema ya furaha Kuu itakayokuwa kwa watu wote. Ujumbe huo unaletwa pia kwetu leo hii. Kwa ajili yetu amezaliwa Mwokozi ndiye Kristo Bwana. Sisi ndio wachungaji wa leo, maskini wa leo tunaohitaji neno la kututia moyo, la kututuliza na kutuhakikishia kuwa Mungu hayuko mbali nasi, bali yuko nasi, ndiyo maana ya Emmanueli, (Isa 7:14; 8:8) Mungu yu pamoja nasi (Isa 8:10).

Yesu anamleta Mungu Baba kwetu, anakuja kumdhihirisha kwetu. Mimi nimejiuliza sana kwa nini hasa nawatakia heri waamini wenzangu na watanzania wote kwa ujumla? Nafanya hivi kwa sababu nawajali. Nawatakia heri kwa sababu naona hali inayotia shaka huko mbele tuendako. Ninaona shaka kwa sababu ya hayo niliyoyaona tulikotoka tangu Januari mwaka huu, na kufikiria mambo yaliyo mbele yetu mwaka 2015.

Tumesafiri mwaka mzima kama jamii ya Tanzania tukishuhudia matukio mbali mbali nchini mwetu ya kutia moyo na ya kukatisha tamaa au kuzua hofu. Mimi si mwandishi wa kutunza kalenda ya matukio. Ukitembelea blog ya Michuzi unaweza kupata baadhi ya matukio ya mwaka 2014. Nitayaacha matukio ya kijimbo na ya Kanisa kiulimwengu kwa nafasi nyingine. Tunaweza pia kuweka pembeni safari za viongozi wa vyama vya CCM na Chadema waliopigana vikumbo kwenye mitaa yetu wengine wakikagua kuona utekelezaji wa ilani ya chama na wengine wakiwa na operesheni Delete chama fulani.

Najikita katika mambo matatu makubwa kitaifa ninayotaka sote tuyarejee na kuona yanatuweka katika hali gani; ya furaha au ya woga? Moja ni Bunge Maalum la Katiba, pili ni Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, na tatu ni Sakata la Pesa za akaunti ya Tegeta Escrow.

Nikianza kugusia jambo lililotikisa nchi baada ya hoja kuibuliwa bungeni kuwa zimechotwa pesa za umma kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, mtu anaweza kusema Askofu amekwepa nini kuhusu hilo? Nikwambie kwanza kwamba rafiki yangu mmoja alinipigia simu tokea Dar es salaam baada ya sakata hilo akinipongeza kwa kutopokea “mgawo wa Escrow”! Aliniambia kuwa maadui wangu walisubiri kusikia natajwa huko, na ingekuwa hivyo nisingepata njia ya kupita kwa sababu ya kelele zangu dhidi ya Bunge la Katiba.

Mimi niseme kwa jambo hilo la pesa za Escrowmimi nilijiuliza: je, hivi jambo hilo halikuwa na agenda za siasa na chuki nyuma yake? Je, lilizungumzwa kwa upendo na uzalendo wa kweli kwa nchi yetu na nia njema kabisa tangu mwanzo hadi mwisho? Je ukweli wote ulisemwa, au yalisemwa yale tu yaliyolenga malengo yaliyokusudiwa? Kama kweli kuna wizi vyombo vya dola vinapaswa kuthibitisha ukweli wa jambo hilo, na wahusika wawajibike ipasavyo. Ila najua umeme ulizalishwa kwa gharama zilizopaswa kulipwa kwa anayeuzalisha.

Je, tuamini kwamba mwekezaji hakuingia gharama kuuzalisha umeme? Kama wazalishaji ni wezi basi waliotumia umeme nao wametumia mazao ya wizi? Haki ya mdai na mdaiwa inapaswa kuzingatiwa. Kwa upande wa tuhuma zilizoelekezwa kwa Benki ya Kanisa na viongozi wa Kanisa niliona siyo za haki. Ukweli haukusemwa wote bungeni. Watoa hoja walikuwa watumwa wa malengo yao binafsi. Benki daima hutenda kwa kuzingatia sheria na taratibu zitolewazo na benki kuu. Benki kama mfanya biashara yeyote lazima afuate kanuni katika utendaji wake.

Benki ya Mkombozi ilifuata taratibu hizo zote, lakini watoa hoja hawakusema hilo, na sifikiri kuwa hawakujua kama benki ile iliuliza benki Kuu kujihakikishia kama zile ni pesa safi au chafu na ikajibiwa. Hawakusema ukweli kuwa benki ya Mkombozi ilifuata agizo la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na ikahamisha pesa ya kodi iliyotakiwa.

Watoa hoja walidai kodi haikulipwa! Hii ilionyesha nia mbaya ya watoa hoja kwani walijua hilo. Wengine walinuia tu kuichafua benki hiyo ikimbiwe na wateja. Ambacho sijajua hadi sasa ni kama zile bilioni 306 zinajumlisha pesa ya hisa zote kumi (yaani 7 za Singasinga Sethi na 3 za Rugemalira) au hizo ni za zile hisa 3 za James Rugemalira? Lakini tunaambiwa kuwa baadhi ya watu waliojua mengi zaidi waliokuwa watendaji wa juu wa IPTL walifukuzwa nchini mwaka jana ili kuficha ukweli. Hivyo ni sehemu tu ya ukweli inajulikana. Ni vizuri na haki uchunguzi zaidi ufanywe, na watafutwe au wafuatwe waliko hao waliofukuzwa waeleze ukweli ili mambo yote yawekwe wazi.

Kwa viongozi wa kanisa kupokea pesa kwa kutumiwa kwenye akaunti wakasemwa kuwa wameiba siyo haki. Kanisani daima tunapokea zaka na sadaka za waamini bila kuuliza zimetoka wapi. Tunafanya miradi mingi kwa kuomba misaada kwa wahisani mbali mbali. Wahisani wanaolisaidia Kanisa hatuwaulizi wamezipataje! Wao walipokea pesa kwa mtindo huo bila kujua zimetoka akaunti ipi. Nafikiri watoa hoja walinuia tu kulichafua Kanisa na kuzima sauti yake ya Kinabii. Lakini sauti ya kinabii haizimwi na mwanakanisa mmoja au elfu kutenda makosa!

Kanisa ni jumuia na siyo mtu mmoja. Mtu ni tawi ambalo likiharibika Bwana analikata na mzabibu unaendelea (Yoh 15:2,6). Ingetosha kuthibitisha kisheria kama pesa zimetolewa kimakosa, na hivyo waliopokea watakiwe kuzirudisha katika akaunti ya mtoaji. Wathibitishe kisheria kwanza. Kutakiana heri leo kutuelekeze katika kuwajali wengine, hasa maskini na wahitaji. Unapokula na kushiba na kustarehe ukisherehekea sikukuu hii, jiulize umefanya nini kumpa furaha maskini pia aliye karibu nawe ili aonje kuwa kweli kuzaliwa kwa Kristo kunaleta furaha kuu kwa watu wote? Kutakiana heri kutuelekeze katika kuipokea amani ambayo Kristo Bwana anatuletea.

Tutambue kazi yake yeye ni kutia hamasa mioyoni mwetu ili tufanye kazi kuipata na kuilinda amani. Wakristo tunakubali na kuamini kuwa Yesu Kristo ni neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote iliyofunuliwa kwetu. Huyu Kristo Yesu amekuja kutufundisha wanadamu wote “kukataa ubaya na tamaa za kidunia, tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa; tukilitamia tumaini lenye Baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na mwokozi wetu; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema” (Tit 2:12-14).

Wapo baadhi ya wakana Mungu na wasio Wakristo lakini wanaomkubali Yesu Kristo na wanaishi wakifuata mafundisho yake. Fundisho lake kuu ni: mpende Mungu na mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe. Hakuna ubaya hata wewe usiye mkristo ukizingatia fundisho hilo, litakubariki pia. Nawatakia tena heri ya Noeli, na amani ya Bwana iwe nanyi.

+Severine NIWEMUGIZI
Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara.








All the contents on this site are copyrighted ©.