2014-12-22 10:05:02

Waziri mkuu Pinda yuko Qatar!


Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda yuko Doha, Qatar kwa ziara ya siku tatu kwa mwaliko wa Serikali ya nchi hiyo. Lengo la ziara ya Waziri Mkuu ni kukuza mahusiano baina ya nchi hizi mbili, kuangalia fursa za kiuchumi na miradi mikubwa inayoweza kuzinufaisha nchi hizo na nje ya mipaka yake kwenye Ghuba ya Arabuni (Arabian Gulf) na Bara la Afrika.

Vile vile Waziri Mkuu anatarajiwa kutangaza fursa za uwekezaji nchini Tanzania, fursa za biashara, za utalii na kutafuta mitaji kwa ajili ya sekta za uchimbaji gesi na mafuta, usindikaji mazao, uvuvi na mifugo, ajira na uendelezaji miundombinu. Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Waziri Mkuu atakuwa na mazungumzo ya kiserikali na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Sheikh Abdulla Nasser Al Thani. Vilevile atakutana na Mawaziri wa Kazi na Ustawi wa Jamii; Uchukuzi; Miundombinu na Uwekezaji wa nchi hii. Naibu Mawaziri atakaokutana nao ni wa Uchumi na wa Nishati.

Vilevile Waziri Mkuu amepangiwa kukutana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Qatar (Qatar Business Community), wajumbe wa Chama cha Wafanyabiashara cha Qatar (Chamber of Commerce of the State of Qatar) na pia atakutana na Watanzania waishio Qatar. Atatembelea pia Mamlaka ya Bandari ya Qatar na makao makuu ya kampuni ya uchimbaji gesi ya Qatar.

Waziri Mkuu amefuatana na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kimani; Waziri wa Kilimo na Maliasili wa Zanzibar, Dk. Sira Ubwa Mamboya; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Mahadhi Maalim; Naibu Waziri wa Nishati, Bw. Charles Kitwanga; Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Bw. Godfrey Zambi. Wengine ni ​ Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Abbas Kandoro, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Bi. Halima Dendego, wabunge wawili Bi. Amina Makilagi na Bw. Aeshy Hilali na Wakuu wa taasisi za TPSF na TPDC.








All the contents on this site are copyrighted ©.