Wahudumieni wananchi kwa kuzingatia: ukweli, uwazi na uaminifu!
Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika mahubiri
yake kwa Wabunge wa Italia, kama sehemu ya maadhimisho ya maandalizi ya Sherehe za
Noeli kwa Mwaka 2014, amewataka Wabunge na viongozi wa Serikali katika ujumla wao,
kuhakikisha kwamba, wanawahudumia wananchi kwa kutumia: ujuzi, maarifana weledi; mambo
yanayojikita katika: uaminifu, nidhamu, ukweli, uwazi na majitoleo kwa ajili ya ustawi
na maendeleo ya wengi.
Wanasiasa wanapaswa kukumbuka kwamba, wamepewa dhamana
na wananchi kwa ajili ya kusaidia mchakato wa kuwaletea maendeleo na wala si fursa
ya wanasiasa hawa kujitajirisha au kutafuta mafao binafsi, mambo ambayo yanakwenda
kinyume kabisa cha lengo la wananchi kuwapatia dhamana ya kuwaongoza!
Ibada
hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa pia na viongozi wakuu wa Bunge na Serikali ya Italia.
Kardinali Bagnasco anasema, Fumbo la Umwilisho wa Mwana wa Mungu ni changamoto kwa
viongozi waliopewa dhamana na wananchi kuwa kati ya wananchi ili kuwahudumia kwa hekima
na busara; huku wakisimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai, utu na heshima
ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Fumbo la Umwilisho, liwasaidie
kujikita katika kutafuta, kuufahamu na kuukumbatia ukweli, ili haki, amani na ustawi
wa wengi viweze kushika mkondo wake. Haya ndiyo malengo makuu ya mchakato wa uongozi
katika siasa! Wanasiasa wakumbuke kwamba, kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu
na kwamba, hii ni fursa makini kwa mtu kuweza kujiendeleza mwenyewe na familia yake.
Mwanadamu
anapokosa fursa za ajira, anajisikia mpweke na utu wake kuanza kuingia mashakani.
Wanasiasa wawe mstari wa mbele kuhakikisha kwamba, wanatunga sera makini zitakazowawezesha
watu kupata ajira pamoja na kuendelea kuwa na matumaini kwa vijana wa kizazi kipya.
Maandalizi na hatimaye, maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli, ni wakati muafaka wa kutakiana
kheri na fanaka; ukweli na uwazi; sadaka na majitoleo, ili kushinda cheche za maovu
zinazotaka kupenyeza miongoni mwa watu kwa kujikita katika uchu wa mali. Kila raia
anapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa ajili ya mafao ya wengi.
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.