Mti wa Noeli ni kielelezo cha mwanga, matumaini na mapendo!
Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 19 Desemba 2014 amekutana na ujumbe kutoka
Jimbo kuu la Verona na Catanzaro ili kuwashukuru kwa zawadi kubwa ya Mti wa Noeli
ambao umepambwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican; mti
ambao kwa sasa ni kivutio kikubwa kwa mahujaji na watalii wengi wanaoendelea kumiminika
mjini Vatican kutoka sehemu mbali mbali za dunia.
Baba Mtakatifu anawashukuru
viongozi wa Mfuko wa Arena kutoka Verona ambao umetoa mchango mkubwa katika kukuza
na kudumisha Mapokeo na Tasaufi inayobubujika kutoka katika Kanisa, ili kuendeleza
utamaduni, fasihi, muziki na sanaa katika maeneo haya. Utajiri huu ni amana kubwa
inayopaswa kulindwa na kuhifadhiwa, ili kuwarithisha vijana wa kizazi kipya kwa siku
za usoni.
Mti wa Noeli ni kielelezo cha Fumbo la Umwilisho na Mwanga wa Mataifa
unaokuja kumwokoa mwanadamu na kufukuza giza katika maisha yake. Ni mti unaogusa udugu,
upendo na mshikamano; urafiki na kwamba, hii ni changamoto kwa watu wa nyakati hizi
kujikita katika kiasi na mshikamano wa upendo. Ni mwaliko wa kujenga na kudumisha
umoja, maridhiano na amani; kuhakikisha watu wanatengeneza nafasi kwa Mwenyezi Mungu
ili aweze kupata makazi katika maisha yao ya kila siku, ili hatimaye, waonje upendo
wake. Mti wa Noeli ni kielelezo cha mwanga, matumaini na upendo.
Baba Mtakatifu
amewatakia wajumbe wote kutoka Veneto na Calabria amani na utulivu katika maadhimisho
ya Siku kuu ya Noeli, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, awaletee mwanga ili kupambana
kikamilifu na dhambi, ili kumkirimia mwanadamu mwanga wa Kimungu ulioletwa na Yesu
mwenyewe na kuwapatia matumaini wale wote wanaoteseka kutokana na kuelemewa na giza
totoro katika undani wa maisha yao!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.