Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema kwamba, Vatican inapenda
kuwakumbuka na kuwashukuru wale wote walioachangia kwa namna ya pekee katika mchakato
wa ujenzi wa mahusiano mapya ya kidiplomasia kati ya Marekani na Cuba.
Kwa
namna ya pekee, shukrani hizi zinamwendea Baba Mtakatifu Francisko aliyeamua kuivalia
njuga changamoto hii kwa kuwaandikia Marais Barack Obama wa Marekani na Rais Raùl
Castro wa Cuba barua ambayo iliwaalika kuangalia uwezekano wa kupata ufumbuzi wa tatizo
la nchi hizi mbili, ili watu wake waweze tena kukutana na kwa ajili ya ustawi na mafao
ya wengi!
Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuhamasisha watu kujenga na kuimarisha
utamaduni wa kukutana, kujadiliana na kushirikiana kwa pamoja hata katika tofauti
zao, ili kudumisha misingi ya haki, amani, upendo, mshikamano wa kidugu kwa ajili
ya ustawi na mafao ya wengi. Utamaduni wa kukutana iwe ni nyenzo msingi katika kutatua
migogoro na kinzani zinapojitokeza kati ya watu badala ya kukimbilia mtutu wa bunduki.
Dipolimasia
ya Vatican inajikita katika mambo makuu yafuatao: haki, amani na mshikamano wa kimataifa
katika mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi; mambo yanayoendelea kunyanyasa
na kudumaza utu na heshima ya binadamu. Vatican inapenda kutandaza "mkeka wa ofisi
zake" unaoweza kutumiwa na watu mbali mbali katika kukoleza mchakato wa majadiliano
yanayojikita katika ukweli, uwazi na mafao ya wengi.
Mahusiano mapya ya kidiplomasia
kati ya Marekani na Cuba yalioneshwa na viongozi wakuu wa nchi hizi mbili yanaweza
kuwa ni kikolezo cha ustawi na maendeleo ya wananchi wanaoishi huko Amerika ya Kusini,
kwa kuwahamasisha viongozi mbali mbali wanaokabiliana na kinzani na migogoro ya ndani
kufungua macho yao kwa ajili ya kuanza mchakato wa majadiliano, unaoweza kuwakutanisha
watu.
Kardinali Pietro Parolin anasema, habari za mahusiano mapya ya kidiplomasia
kati ya Marekani na Cuba, zimepokelewa kwa mikono miwili kiasi kwamba, kengele za
Makanisa mengi nchini Cuba ziligongwa kuashilia mwanzo mpya na matumaini kwa siku
za usoni. Kanisa litaendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake msingi kwa ajili ya
ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Cuba, kwa kujikita katika mshikamano wa kidugu
kwa ajili ya mafao ya wengi.
Kanisa linamshukuru Mwenyezi Mungu kwa ushirikiano
mkubwa ulioneshwa na watu wenye mapenzi mema, waliotaka kuona Marekani na Cuba zikianza
uhusiano mpya wa kidiplomasia kwa kuvunjilia mbali lile "Pazia la Chuma" lililowatenganisha
wananchi wa Marekani na Cuba kwa miaka 53 ya vita baridi!
Na Padre Richard
A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.