2014-12-18 14:35:54

Mwaka 2017 Wakatoliki na Waluteri kuungama imani, kusali na kuombana msamaha


Tume ya Majadiliano ya Kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri, nchini Ujerumani, katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita imepata mafanikio makubwa kwa msaada wa Mungu, katika mchakato unaopania kuimarisha urafiki unaojikita katika msingi wa imani na tasaufi.

Licha ya tofauti kati ya waamini wa Makanisa haya, bado wameendelea kuishi kama ndugu, huku wakipania kuendeleza majadiliano ya kiekumene, kwa kutambua kwamba, hii ni dhamana nyeti kwa Kanisa linalohimizwa kujielekeza katika ujenzi wa umoja kadiri ya imani katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Tamko la pamoja kuhusu kuhesabiwa haki, lililotiwa sahihi na Makanisa haya mawili, yapata miaka kumi na mitano iliyopita, huko Augsburg ni muhimu sana katika kukuza na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene.

Ni changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 18 Desemba 2014 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Tume ya Majadiliano ya Kiekumene kati ya Kanisa Katoliki la Kanisa la Kiinjili la Kiluteri, Ujerumani, ilipomtembelea mjini Vatican, Lengo la pamoja ni kuwa na umoja kamili kati ya Wakristo, lakini umoja huu wakati mwingine unaonekana kana kwamba, unasua sua kutokana na tafsiri mbali mbali zinazotolewa katika majadiliano ya kiekumene kuhusu Kanisa na dhana ya Umoja.

Changamoto zote hizi zisiwe ni sababu ya kuwakatisha Wakristo tamaa na badala yake wajikite zaidi na zaidi katika ujenzi wa urafiki, heshima, tafiti za kitaalimungu pamoja na kuangalia mbele kwa matumaini. Ndiyo maana anasema Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 21 Novemba 2014 Makanisa makuu nchini Ujerumani yaligonga kengele kuwaalika Wakristo popote pale walipokuwa kushiriki katika Ibada ya pamoja, kama kilele cha kuadhimisha Jubilee ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Waraka wa Majadialiano ya Kiekumene unaojulikana kwa lugha ya Kilatini "Unitas redintegratio".

Baba Mtakatifu Francisko anapongeza juhudi zinazofanywa na Tume hii ya pamoja katika kukamilisha kazi inayopembua tema ya "Mungu na utu wa mwanadamu": ni mada muhimu sana kwa nyakati hizi kwani inagusa masuala tete ya Injili ya Uhai; Familia na Ndoa ili kupata mwelekeo wa Kiekumene. Itasikitisha kuona kwamba, hata katika masuala haya, Wakristo wanagawanyika tena kwa misingi ya madhehebu yao.

Baba Mtakatifu anasema, kunako mwaka 2017, Wakatoliki na Waluteri kwa pamoja wataadhimisha kumbu kumbu ya Jubilee ya Karne tano tangu yalipotokea Mageuzi makubwa ndani ya Kanisa, kwa kuungama pamoja imani kwa Fumbo la Utatu Mtakatifu, Mungu mmoja katika Nafsi kuu tatu!. Itakuwa ni fursa ya kusali na kuombana msamaha, ili kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili kujenga na kudumisha umoja badala ya kuendekeza kinzani na mitafaruku.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, maadhimisho haya kwa msaada wa Roho Mtakatifu yanaweza kusaidia kupiga hatua kubwa katika majadiliano ya kiekumene, ili hatimaye, kufikia umoja kamili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.