Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 17 Desemba 2014 ameadhimisha kumbukumbu
ya miaka 78 tangu alipozaliwa. Tukio hili, limewashirikisha watu mbali mbali kwa kukutana
kwanza kabisa na baadhi ya maskini kutoka Roma na kuwapatia zawadi kama kumbu kumbu
ya tukio hili muhimu katika historia ya maisha yake.
Rais Giorgio Napolitano
wa Italia ni kati ya viongozi wakuu wa nchi waliomtumia salam na matashi mema Baba
Mtakatifu Francisko, kwa kuwashirikisha Watu wa Mataifa ujumbe wa amani na matumaini;
mambo msingi yanayoacha chapa ya kudumu katika mioyo ya watu. Serikali ya Italia na
Kanisa, wataendelea kushirikiana kwa karibu zaidi kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa jamii.
Baba Mtakatifu amepokea pia mafuriko ya salam na matashi
mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia bila kusahau kwamba, waamini na watu wenye
mapenzi mema wametolea sala na maombi yao kwa ajili ya maisha na utume wake kama Khalifa
wa Mtakatifu Petro. Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican uligeuka
kuwa ni ukumbi wa dansi, watu walipoamua kujimwaga uwanjani na kuanza kucharaza muziki
wa "tango" kwa heshima ya Baba Mtakatifu Francisko anapomshukuru Mungu kwa zawadi
ya uhai.
Kardinali Claudio Hummes, akizungumza kutoka San Paolo, Brazil, amemtakia
Baba Mtakatifu Francisko heri na baraka kwa kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 78 tangu
alipozaliwa. Anamsihi asonge mbele kwa ujasiri, imani na matumaini katika mchakato
wa kuleta mageuzi makubwa ndani ya Sekretarieti ya Vatican kama walivyoshauri Makardinali
katika mikutano yao elekezi, bila ya kukata tamaa, kwani Familia ya Mungu iko nyuma
yake.
Kardinali Claudio Hummes amemtakia afya njema, furaha na amani anapotekeleza
utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, hata kama kuna ugumu na changamoto zake.
Kardinali Hummes anatambua uzito na unyeti wa utume huu, lakini asiogope, waamini
wanaendelea kumkumbuka na kumsindikiza kwa sala na sadaka zao, ili yote yafanyike
kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu pamoja na ustawi wa Kanisa la Kristo.