2014-12-18 14:42:13

Mabalozi wapya wawasilisha hati za utambulisho kwa Papa Francisko


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 18 Desemba 2014 amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Mabalozi wapya kumi na tatu wanaoziwakilisha nchi zao mjini Vatican. Balozi hawa ni kutoka: Tanzania, Rwanda, Mali na Togo. Wengine wanatoka Mongolia, Bahamas, Denmark, Malaysia, Finland, New Zealand, Bangaladesh na Qatar.

Balozi Philip Sang'ka Marmo kutoka Tanzania, alizaliwa kunako tarehe 29 Desemba 1951. Ameoa na amebahatika kuwa na watoto. Alipata shahada yake ya kwanza katika sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kunako mwaka 1977 na baadaye kati ya mwaka 1978 hadi mwaka 1984 alijiendeleza katika Sheria na kubahatika kupata Shahada ya uzamili. Kuanzia mwaka 1985 hadi mwaka 2010 alikuwa ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na kushika nafasi kadhaa za Uwaziri katika Serikali ya Tanzania hadi mwaka 2010.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akamteuwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini China kuanzia mwaka 2011 hadi mwaka 2013. Kuanzia mwezi Januari 2014 akateuliwa kuwa ni Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani pamoja na kuwakilisha Tanzania katika nchi kadhaa za Ulaya.

Balozi Francoise Xavier Ngarambe kutoka Rwanda alizaliwa kunako tarehe 24 Agosti 1957, ameoa na amebahatika kupata watoto wanne. Kunako mwaka 1984 alipata shahada ya kwanza katika masuala ya utawala kutoka katika Chuo Kikuu cha Rwanda, baadaye akajiendeleza na hatimaye kujipatia Shahada ya uzamili kutoka katika Chuo kikuu cha Serikali cha Tarlac, kilichoko nchini Ufilippini, kunako mwaka 2013.

Katika maisha yake, amewahi kuwa Mkurugenzi mkuu wa Mfuko wa usalama wa kijamii kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2006. Aliwahi kuwa Rais na Mkurugenzi mkuu wa Tume ya Bima ya Taifa kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2007. Kunako mwaka 2007 hadi mwaka 2010 akateuliwa kuwa katibu mkuu wa maendeleo katika sekta ya fedha. Kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2014 aliteuliwa kuwa ni Balozi wa Rwanda nchini China. Kuanzia mwaka 2014 ni Balozi wa Rwanda nchini Uswiss na mwakilishi wa Rwanda katika Mashirika ya Kimataifa: UN, WTO na UNIDO.

Balozi Cheick Mouctary Diarra kutoka Mali alizaliwa kunako tarehe 8 Juni 1939, ameoa na amebahatika kupata watoto wawili. Amewahi kuwa ni Mkurugenzi wa Shirika la Habari la Taifa kuanzia mwaka 1970 hadi mwaka 1971. Akawa mhariri msaidizi wa Gazeti la L'Essor kuanzia mwaka 1971 hadi mwaka 1977. Baadaye aliteuliwa kuwa Mkurugenzi mkuu wa Wakala wa Magazeti na Matangazo ya Biashara kuanzia mwaka 1977 hadi mwaka 1991.

Balozi Diarra, kunako mwaka 1991 hadi mwaka 1992 aliteuliwa kuwa mshauri wa kiufundi katika Wizara ya Habari. Na kunako mwaka 1992 hadi mwaka 1995 alikuwa ni mshauri mkuu wa uhusiano wa kimataifa katika Ofisi ya Rais. Kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 1997 alikuwa ni Balozi wa Mali nchini Senegal, Gambia na Cape Verde. Kuanzia Mwaka 1997 hadi mwaka 1999 alikuwa ni msahuri wa Chama cha Umeme nchini Ufaransa na kwa sasa ni Balozi wa Mali nchini Ufaransa.

Balozi Kokou Nayo Atsumikoa M'beou kutoka Togo alizaliwa tarehe 25 Mei 1957 ameoa na ana watoto wanne. Kunako mwaka 1982 alipata shahada ya kwanza katika sheria kutoka katika Chuo Kikuu cha Benin-Lomè na kunako mwaka 1983 akajipatia shahada ya uzamili pamoja na kujiendeleza katika masuala ya kidiplomasia hadi mwaka 1985.

Balozi M'beou amewahi kuwa mkurigenzi wa masuala ya mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa kuanzia mwaka 1986 hadi mwaka 1991. Kunako mwaka 1991 hadi mwaka 1994 aliteuliwa kuwa mkuu wa Blitta. Kunako mwaka 1995 hadi mwaka 1998 alikuwa mfanyakazi katika Idara ya mambo ya siasa na mahakama. Kunako mwaka 1999 hadi mwaka 2000 aliteuliwa kufanya kazi katika Wizara ya mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa.

Kunako mwaka 2001 hadi mwaka 2004 alifanya kazi katika Idara ya Mashirika ya Kimataifa na Ushirikiano kama mshauri wa kifundi. Baadaye aliteuliwa kunwa ni mkurugenzi mkuu wa sheria na masuala tete. Kuanzia mwaka 2008 akateuliwa kuwa ni makamu mwakilishi wa Togo kwenye Umoja wa Mataifa, Jijini New York.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.