2014-12-18 07:16:26

Kilio cha wakimbizi na wahamiaji!


Kardinali Antonio Maria Veglio’, Rais wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum anasema kwamba, katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na ongezeko la kundi kubwa la watoto wanaotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na uhalifu wa kimataifa. RealAudioMP3

Hawa ni watoto ambao wamepokwa utu, heshima na matumaini yao kwa siku za usoni, kwani hakuna mtu anayewajali na kuwatunza na matokeo yake ni kwamba, wanaishia pabaya kama askari ambao ni chambo kinachopelekwa mstari wa mbele katika mapambano; ni watoto kama hawa wanaohusishwa katika biashara haramu ya dawa za kulevya na ukahaba.

Watoto hawa anasema Kardinali Veglio’ hawana ulinzi wala tunza kutoka kwa wazazi au walezi wao, ni watoto ambao wamekimbia vita,umaskini, nyanyaso na adha mbali mbali za maisha. Kanisa kwa kutumia taasisi zake mbali mbali limekuwa mstari wa mbele kuwasaidia na kuwahudumia watoto wanaotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, mada ambayo kwa sasa inavaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa kwani huu ni uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema ili kutoa taarifa kamili juu ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, mwenendo na tabia yake pamoja ya kupinga ukosefu wa haki msingi dhidi ya watu kama hawa.

Serikali zikiwa na sera makini juu ya wahamiaji, zinaweza kushirikiana kikamilifu na Kanisa katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kwa kuzingatia na kuheshimu utu wao kama binadamu na wala si kama mzigo na chanzo cha kampeni chafu dhidi ya wahamiaji, kama inavyojionesha katika nchi nyingi za Ulaya. Hivi karibuni, Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani wameunganisha nguvu zao na Baraza la Maaskofu Katoliki Mexico, ili kutekeleza mikakati ya pamoja kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji kutoka Mexico; ili kulinda na kutetea utu na heshima ya wakimbizi na wahamiaji hawa, ambao wakati mwingine wanakumbana na “Pazia la chuma”.

Kuna idadi kubwa ya watoto wanaoteseka kutokana na kukosa wazazi na walezi wakati wanapokuwa uhamishoni, matokeo yake wanajikuta wakiishia kwenye magereza ya watoto, hali ambayo inawachia madonda makubwa katika maisha na makuzi yao, hili kwa upande mwingine anasema Kardinali Antonio Maria Veglio’ kuwa ni janga la kimataifa, hali ambayo kamwe haiwezi kukubalika iendelee kama ilivyo.

Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, watoto hawa wanapokelewa na kupewa hifadhi kisheria sanjari na kuendeleza marekebisho katika sheria juu ya wahamiaji pamoja na kusaidia kupambana na mambo yanayopelekea kundi kubwa la watoto kukimbia kutoka kwa wazazi wao. Kwa maneno mengine, kuna haja ya kusaidia mchakato wa kupambana na umaskini ambao ndicho chanzo kikuu kinachowafanya watu wengi kukimbia nchi zao.

Watoto wengi wanaishi katika mazingira hatarishi, kiasi kwamba, wanakumbwa na kishawishi kikubwa cha kukimbia ili kutafuta maisha bora zaidi hata kwa gharama ya maisha yao na matokeo yake, wengi wao wanakufa maji baharini au kwa kiu na utupu jangwani.

Baadhi ya watoto hawa anasema Kardinali Veglio’ wanatumbukia kwenye mikono ya wafanyabiashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, hivyo wanauzwa kama biadhaa Barani Ulaya mambo yanayodhalilisha utu na heshima yao kama binadamu. Jumuiya ya Kimataifa inapoadhimsiha kumbu kumbu ya miaka 25 tangu Azimio la Haki ya Mtoto lilipoanzishwa kunako mwaka 1989, kuna haja ya kuendelea kukazia umuhimu wa watoto kutobaguliwa wala kutengwa, kwa kuhakikisha kwamba, haki za watoto zinalindwa na kudumishwa kwa kupatiwa: elimu, afya pamoja na kuungana na wazazi wao.

Takwimu zinaonesha kwamba, watoto wadogo ambao ni wakimbizi na wahamiaji, wengi wao ni kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara, yaani Eritrea, Somalia na Sudan na wengine wanatoka Mashariki ya Kati, huko ambako vita, nyanyaso na kinzani za kidini na kisiasa bado zinapamba moto. Watoto hao wanafanya maamuzi magumu yaliyo juu ya uwezo wao, kumbe, wanapaswa kusikilizwa kwa makini, kupewa tiba na kusaidiwa kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi kuliko walikotoka. Maisha ya watoto hayana budi kupewa kipaumbele cha kwanza badala ya mtindo wa sasa wa kuangalia idadi yao, kwani nyuma ya idadi, kuna utu na haki msingi za watoto.

Kardinali Antonio Maria Veglio’ anawashukuru wadau mbali mbali wanaojitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwasaidia watoto wahamiaji na wakimbizi kupata tena matumaini mapya, kwani watoto wanapokubalika na kupolekewa; wanapopendwa na kuheshimiwa; wanapohudumiwa na kulindwa, hapo jamii inaboreka zaidi na kuwa na uhakika wa amani, usalama na utulivu, vinginevyo, itakuwa ni patashika nguo kuchanika!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.