Mwachieni nafasi Yesu ili azaliwe tena ndani mwenu!
Kardinali Angelo Comastri, mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican,
Jumanne, tarehe 16 Desemba 2014 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya wafanyakazi
wa Vatican, kama sehemu ya maandalizi ya Siku kuu ya Noeli, inayowakumbusha binadamu
kwamba, Neno wa Mungu amefanyika mwili na kuzaliwa kati yao katika hali ya umaskini
na unyenyekevu mkuu!
Yesu alizaliwa Pangoni, mahali pa kulishia wanyama! Swali
la msingi ambalo Kardinali Comastri anauliza, Je, kwanini Yesu aliamua kuzaliwa katika
mazingira duni kiasi hiki? Kimsingi, dunia ni sawa na tambara bovu, mahali panapoonesha
umaskini mkubwa, ikiwa kama waamini na walimwengu hawatakuwa tayari kupokea mwanga
kutoka kwa Kristo, ili kushuhudia matendo makuu ya Mungu yanayojikita katika toba
na wongofu wa ndani; katika misingi ya haki, amani na mshikamano.
Waamini na
watu wote wenye mapenzi mema wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuondokana na ubinafsi
unaopofusha mawazo na matendo ya watu, kiasi cha kushindwa kuona utu na heshima ya
binadamu; mateso na mahangaiko ya watu mbali mbali. Noeli ni fursa makini kwa waamini
kumwachia nafasi ili Mtoto Yesu aweze kuzaliwa ndani mwao, tayari kumshuhudia kwa
njia ya imani tendaji!