2014-12-17 08:03:09

Mshikamano wa dhati katika kupambana na janga la Ebola!


Ziara ya Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani nchini Siera Leone na Liberia ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuonesha mshikamano wa udugu na upendo katika mapambano dhidi ya janga la Ebola ambalo linaendelea kusababisha maafa makubwa kwa wananchi wengi Afrika Magharibi. Ni ziara ya upendo, mshikamano na matumaini kwa watu ambao wamevunjika na kupondeka moyo kutokana na ugonjwa wa Ebola.

Kanisa linaendelea kuwahamasisha wafanyakazi katika sekta ya afya huko Afrika Magharibi kutokata tamaa katika kuwahudumia waathirika wa ugonjwa wa Ebola. Taarifa zinazonesha kwamba, kuna kundi kubwa la watoto yatima ambao wameachwa na wazazi wao kutokana na maafa ya ugonjwa wa Ebola na kwa sasa wanaishi katika mazingira hatarishi na wakati mwingine hawapokelewi na ndugu na jamaa zao kutokana na kugopa kuambukizwa virusi vya Ebola.

Taarifa ya Benki ya Dunia inaonesha kwamba, kutokana na madhara ya ugonjwa wa Ebola, nchi ya Siera Leone kwa mwaka 2015 itakuwa na hali ngumu sana ya uchumi. Kabla ya kuibuka kwa ugonjwa wa Ebola, Sierra Leone, ilikuwa imeanza kucharuka katika maendeleo ya kiuchumi, lakini kwa sasa hali ni ngumu na watu wamekata tamaa.

Kardinali Turkson anasema, kutokana na changamoto hizi zote, kuna haya ya kuwaonesha wananchi waliokumbwa na janga la Ebola mshikamano, ili hatimaye, ugonjwa huu uweze kudhibitiwa na watu kuendelea na mchakato wa kujiletea maendeleo yao wenyewe! Itakumbukwa kwamba, kuanzia tarehe 16 hadi tarehe 18 Desemba 2014, Kardinali Peter Turkson, yuko Afrika Magharibi ili kuonesha mshikamano wa upendo kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko.







All the contents on this site are copyrighted ©.