Maaskofu Australia wasali kwa ajili ya watu waliofariki dunia huko Sydney!
Baraza la Maaskofu Katoliki Australia, Jumanne tarehe 16 Desemba 2014 limeadhimisha
Ibada ya Sala maalum kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea watu waliofariki dunia
kutokana na vitendo vya kigaidi vilivyofanywa mjini Sydney, Australia, siku ya jumatatu.
Kitendo hiki kimefanywa na Man Haron Monis, mwamini mwenye msimamo mkali wa kidini
kutoka Iran aliyeteka watu kadhaa nyara kwa kipindi cha masaa kumi na sita.
Katika
shambulio hili la kigaidi, watu watatu wamepoteza maisha yao! Baraza la Maaskofu Katoliki
Australia linaungana na wale wote wanaoomboleza msiba huu mkubwa kwa kuondokewa na
ndugu zao. Maaskofu wanavishukuru na kuvipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa
kutekeleza wajibu wao kwa kuhatarisha maisha yao, ili kuokoa maisha ya wananchi wengi
wa Australia kutoka katika tukio hili la kigaidi. Maaskofu wanawapongeza wafanyakazi
katika sekta ya afya waliotekeleza dhamana yao kwa utashi kamili, uvumilivu na ujasiri.
Baraza
la Maaskofu Katoliki Australia linawaalika wananchi na watu wote wenye mapenzi mema
kulaani vikali vitendo vya kigaidi, hasa wakati huu Wakristo wanapojiandaa kwa ajili
ya kuadhimisha Siku kuu ya Noeli; iwe ni fursa ya kutafuta, kujenga na kudumisha amani
na maelewano kati ya watu. Ni fursa ya kuwaendea wote kwa kutumia nguvu ya upendo,
ili kuwaonjesha amani na uponyaji!