2014-12-15 09:03:10

Neno la Papa Francisko kwa makundi mbali mbali ya waamini!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 14 Desemba 2014 ametembelea Parokia ya Mtakatifu Yosefu iliyoko Aurelio, Jimbo kuu la Roma na kupata nafasi ya kuzungumza pamoja na makundi ya wanaparokia hii. Akizungumza na watoto, Baba Mtakatifu amewaambia kwamba, mwaka huu ameadhimisha miaka 70 tangu alipopokea Komunio Takatifu kwa mara ya kwanza kunako tarehe 8 Oktoba 1944.

Watoto waliokuwa wanajiandaa kupokea Ekaristi Takatifu walitakiwa kuonesha heshima, adabu na ibada. Tarehe hiyo hiyo, jioni, waliimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara, changamoto kwa watoto wote watakaopokea Ekaristi Takatifu na kuimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara kuikumbuka siku hii muhimu sana katika maisha yao ya Kikristo! Hii ni siku ya kwanza ambayo Yesu ameingia rohoni mwao, ili kuwa chakula chao cha maisha ya kiroho, kwa kuwajalia nguvu.

Baba Mtakatifu anawataka Wakristo kuwakumbuka, kuwasaidia na kuwaombea Makatekista wanaojitaabisha kwa ajili ya kuwarithisha imani. Waamini wafanye kumbu kumbu ya matukio haya kwa kujiandaa kikamilifu katika maisha ya kiroho, yaani kwa kuungamana na kupokea Ekaristi Takatifu.

Baba Mtakatifu akizungumza na watu wasiokuwa na makazi maalum, amewatakia kheri, amani, baraka na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo, ili iwawezeshe kusonga mbele kwa imani na matumaini, bila kukata tamaa, kwani iko siku Mwenyezi Mungu atawatembelea katika maisha yao. Amewapongeza wote wanaojibidisha kujifunza amani kuendeleza juhudi hizi kwani, Mwenyezi Mungu atawakirimia matunda ya amani kwa wakati muafaka.

Baba Mtakatifu Francisko akizungumza na wagonjwa, amewaombea amani na faraja na kuwataka kuendelea kusali kwa ajili ya Kanisa kwani wao ni chombo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Wagonjwa wapokee hali yao kwa imani, matumaini na uvumilivu, wakionesha furaha na amani ya ndani.

Baba Mtakatifu amebahatika pia kuzungumza na Watoto ambao wamebatizwa katika kipindi cha mwaka huu; watoto ambao walikuwa wameandamana na wazazi pamoja na walezi wao. Amewataka wazazi kuwalea na kuwatunza watoto wao vyema kwani hawa ni matumaini ya Kanisa na Jamii kwa ujumla. Watoto walirithishwe imani, matumaini na mapendo; kwa njia ya Sakramenti za Kanisa. Siku ya Ubatizo, waamini wanapata neema ya utakaso wanayopaswa kuitunza kwa njia ya maisha adili na safi.

Mwishoni, Baba Mtakatifu amewaombea watoto hawa furaha, imani na matumaini ya kweli! Baba Mtakatifu anasema, mtoto anapolia Kanisani, hii sehemu nzuri sana ya mahubiri na hapendi kuwaona watu wakiwatoa mama zao nje, ili waweze kuwanyamazisha!







All the contents on this site are copyrighted ©.