2014-12-15 09:12:27

Msijenge urafiki na Shetani!


Askofu Renatus Nkwande wa Jimbo Katoliki la Bunda, Jumapili tarehe 14 Desemba 2014 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Jumuiya ya Wanafunzi Watanzania Wakatoliki wanaosoma na kuishi mjini Roma. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Parokia ya Mwili na Damu ya Kristo, Roma, kwa ajili ya kuombea: haki, amani, upendo na mshikamano wakati huu Tanzania inapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka 53 tangu ilipojipatia uhuru wake wa bendera kutoka kwa Mwingereza. RealAudioMP3

Askofu Nkwande amewataka watanzania wanaosoma na kufanya shughuli zao mbali mbali nchini Italia, kuwa ni cheche za furaha, matumaini na imani, hasa wakati huu, Mama Kanisa anapojiandaa kwa ajili ya ujio wa Yesu Kristo Mkombozi wa ulimwengu. Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ambao unaonesha dalili za kutaka kumweka Mwenyezi Mungu pembezoni mwa mipango na mikakati yao ya maisha, kwa waamini wahakikishe kwamba, Mungu anapewa kipaumbele cha kwanza kabisa, ili aweze kufanya maajabu katika maisha ya mwanadamu.

Askofu Nkwande amewataka waamini kunyoosha mapito na maisha yao, ili Masiha aweze kuzaliwa mahali pa salama na hatimaye, kuwawezesha kupata maisha ya uzima wa milele. Jumuiya ya Watanzania inayoishi na kufanya utume wake mjini Roma, imekumbushwa kwa namna ya pekee, kwa kweli ni mashhuhuda wa: imani, ukweli na haki, mambo yanayohitaji ujasiri na nguvu kutoka kwa Roho Mtakatifu, ili Injili iweze kupenya katika maisha na vipaumbele vya watu.

Ni Roho Mtakatifu anayewaongoza, anayewaelekeza na kuwaimarisha tayari kutoka kifua mbele ili kutangaza Habari Njema ya Wokovu, kama alivyofanya Yohane Mbatizaji anayesimuliwa katika Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Majilio. Yesu Kristo akiwa amejazwa na nguvu ya Roho Mtakatifu aliweza kushuhudia upendo, huruma na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kuwasamehe watu dhambi zao; kwa kuwaponya magonjwa na madhaifu yao ya kimwili pamoja na kuwapatia mahitaji yao msingi.

Askofu Nkwande anasema, Roho Mtakatifu anawajalia waamini nguvu, ujasiri na neema ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu, kwa kutambua kwamba, shida na magumu yataambatana nao hadi ukamilifu wa dahali. Waamini wanatakiwa kuwa na ujasiri wa kutangaza Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; ujasiri wa kushuhudia kanuni maadili na utu wema, dhidi mielekeo potofu ya kijamii inayotaka kuhalalisha hata mambo machafu kama ushoga kuwa eti ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Matendo kama haya ni kutaka kujenga na kuimarisha urafiki na Shetani.

Askofu Nkwande anawataka waamini kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwavisha vazi la haki, huruma, mapendo na ujasiri ili kupambana na kinzani za kimaadili, kama walivyofanya Mababa wa Kanisa la Mwanzo, kiasi hata wakawa tayari kujisadaka maisha yao kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mwenyezi Mungu. Umefika wakati kwa Kanisa la Bara la Afrika kusimama kidete, kulinda na kutetea tunu bora za Kiinjili bila ya kuyumbishwa.

Waamini kwa njia ya ushuhuda wa maisha na matendo yao, wawafundishe watu namna ya kuambatana na Mwenyezi Mungu; kwa kujikita katika kanuni maadili na ukweli; mambo msingi katika kuleta mabadiliko katika maisha ya watu wanaotaka kukengeuka na kumezwa na malimwengu. Waamini wachangie kwa hali na mali katika mchakato wa Uinjilishaji, kwa kulinda na kutetea hadhi, utu na heshima ya binadamu; kwa kutumia hekima na busara.

Imeandikwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.