Askofu Renatus Nkwande wa Jimbo Katoliki Bunda katika maaadhimisho ya Ibada ya Misa
Takatifu Jumapili iliyopita tarehe 14 Desemba 2014 kwenye Parokia ya Mwili na Damu
ya Kristo, iliyoko Jimbo kuu la Roma, kwa ajili ya Jumuiya ya Wanafunzi Watanzania
Wakatoliki wanaosoma na kuishi mjini Roma, amewataka watanzania kuendelea kuombea
misingi ya: haki, amani na utulivu hasa wakati huu Tanzania inapokabiliwa na majaribu
makubwa katika historia na maisha yake.
Askofu Nkwande,
ametumia fursa ya Ibada ya Jumapili, kwa ajili ya kuombea uchaguzi wa Serikali za
Mitaa uliokuwa unafanyika nchini Tanzania kwa kuvishirikisha vyama mbali mbali vya
kisiasa. Tanzania kwa kipindi cha miaka 53 iliyopita, ilihesabiwa kuwa ni nchi ya
amani, lakini leo hii, wengi wanasema Tanzania ni nchi yenye utulivu.
Ameombea
uchaguzi wa Serikali za mitaa, ili kweli Jamii ya Watanzania iweze kupata viongozi:
wema na waadilifu; wakweli na waaminifu; watu wenye nia ya kuchochea maendeleo kwa
watu, huku wakijenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano kati ya watu kuliko
kuendekeza udini, ukabila na umajimbo; mambo ambayo yanaweza kulitumbukiza taifa la
Tanzania katika majanga makubwa.
Askofu Nkwande anasema: misimamo mikali ya
kidini, mauaji, dhuluma na vistisho kwa viongozi wa kidini; madai yasiyokuwa kweli
kuhusu baadhi ya watanzania kukandamizwa kwa misingi ya udini; rushwa, wizi na ufisadi
ni dalili kwamba, amani na utulivu nchini Tanzania vinaweza kutoweka kama ndoto ya
mchana, ikiwa kama watanzania wenyewe hawatasimama kidete kupinga chokochoko hizi
kwa kukazia: ukweli, umoja na mshikamano wa kitaifa.
Hapa Askofu Nkwande anawataka
pia viongozi wa Kanisa kuchunguza dhamiri zao mbele ya Mwenyezi Mungu kuona ikiwa
kama kweli, wamekuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa njia ya maisha na matendo yao, ili
kweli waweze kuwa na ujasiri wa kukemea maovu yanapojitokeza katika jamii, vinginevyo
watakuwa ni mashuhuda wasiokuwa na mvuto wala mashiko, tofauti kabisa na alivyokuwa
Yohane Mbatizaji anayesimuliwa katika Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya tatu
ya Kipindi cha Majilio.
Askofu Nkwande amesema, Kashfa ya Fedha za Escrow imelitikisa
Taifa hata Kanisa limeguswa, kwani kuna baadhi ya viongozi wa Kanisa wametajwa kupokea
mafungu makubwa makubwa ya fedha kutoka kwenye akaunti ya Escrow ya Tegeta. Kashfa
hii iwe ni fundisho kwa Kanisa kwamba, kamwe halitaweza kujitolesheleza, litaendelea
kutaabika na kuchakarika, huku likiwezeshwa na waamini wa kawaida kabisa kama ilivyotokea
kwa Yesu na Mitume wake.
Vinginevyo, anasema Askofu Nkwande, harambee zinazoitishwa
na Makanisa zinaweza kukusanya maelfu ya fedha chafu, kiasi kwamba, Makanisa, majumba
na mambo mengine ya Kanisa yatakuwa yananuka harufu ya fedha chafu. Umaskini na ukata
wa Kanisa, kisiwe ni kisingizio cha kukengeuka na kuacha misingi ya maadili, uwajibikaji,
ukweli na uwazi.
Jumapili iliyopita Jumuiya ya Wanafunzi Wakatoliki kutoka
Tanzania wanaosoma mjini Roma ilifanya uchaguzi mkuu na wafuatao wamepewa ridhaa ya
kuwaongoza watanzania wenzao kwa kipindi cha mwaka mmoja yaani 2014- 2014.
1.
Pd. Joseph Peter Mosha, M-Kiti 2. Pd. Pambo Martin Mkorwe OSB, Katibu. 3. Sr.
Martin Shayo CDNK, Fedha. 4. Pd. Sayoni Jeremiah SDS, Liturujia na Ibada. 5.
Pd. Klement Kihiyo, Mkutubi.
Imeandikwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.