Vatican na Serikali ya Italia kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi!
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 13 Desemba 2014 amekutana na kuzungumza
na Bwana Matteo Renzi, Waziri mkuu wa Italia pamoja na ujumbe wake, ambao baadaye
walikutana kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa
ameambatana na Askofu mkuu Dominique Mamberti aliyekuwa Katibu mkuu wa Mambo ya nchi
za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican.
Viongozi hawa wawili wamejadili
kwa kina na mapana kuhusu athari za myumbo wa uchumi kimataifa zinavyotendea mahusiano
ya kijamii, kiasi cha kuzalisha kundi kubwa la vijana ambao hawana fursa za ajira.
Baba Mtakatifu na mgeni wake, wamekazia umuhimu wa elimu na majiundo makini kwa vijana
wa kizazi kipya. Baadaye, viongozi hawa wamejikita katika masuala ya siasa kimataifa
hasa kutokana na kuendelea kuwepo kwa kinzani na vita sehemu mbali mbali za dunia.
Italia
imepongeza hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipotembelea Bunge
la Ulaya huko Strasbourg, Ufaransa hivi karibuni na kwamba, mambo yaliyotajwa na Baba
Mtakatifu ni kichocheo kikubwa cha maendeleo na mshikamano na mfungamano kati ya watu.
Vatican na Italia zimerudia tena wito wa kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi,
ili kutafuta ufumbuzi wa matatizo na changamoto zinazojitokeza baina ya pande hizi
mbili!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican