2014-12-13 14:53:59

Utimilifu wa maisha ya binadamu unafumbatwa kwa kupenda na kujisadaka kwa ajili ya wengine!


Baba Mtakatifu Francisko, amewataka walemavu kuwa na ujasiri wa kuthubutu kukutana na wengine, tayari kuanza mchakato wa ujenzi wa jamii, hasa wakati huu ambapo haki binafsi zinazonekana kupewa kipaumbele cha kwanza katika medani za kitaifa na kimataifa. Baba Mtakatifu ameyasema haya, Jumamosi tarehe 13 Desemba 2014 alipokutana na kuzungumza na Baraza la Kitaifa la Vipofu, wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Lucia, msimamizi wa vipofu!

Mtakatifu Lucia, Shahidi aliyeuwawa kikatili kunako Karne ya nne, anaendelea kuwafunda walimwengu kuhusu tunu msingi za utu na maisha ya binadamu, zinazothaminiwa na wote bila kuangalia imani ya mtu, kama inavyojionesha hata katika Chama hiki ambacho kinaundwa na watu kutoka katika imani mbali mbali. Baba Mtakatifu anapongeza ujasiri na imani iliyooneshwa na Mtakatifu Lucia kwamba, ilikuwa inapata chimbuko lake kutoka kwa Yesu Kristo Mfufuka, changamoto kwa kila mtu kuwa na ujasiri wa kupambana na majaribu katika maisha pasi na kukata tamaa.

Vipofu na walemavu wengine wote hawana sababu ya kujifungia katika upweke wao, bali kuthubutu kushirikiana na wengine, kwa kukutana na watu wengine katika jamii ili kujifunza na kuthamini uwezo ambao Mwenyezi Mungu amewakirimia katika hija ya maisha yao hapa duniani na kwamba, hakuna mtu ambaye amenyimwa yote na Mwenyezi Mungu, lakini mambo haya yanahitaji ujasiri na msukumo wa ndani.

Mtakatifu Lucia aliweza kukabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha yake, kwani alibahatika kuishi katika Jumuiya na kwamba, Chama cha Vipofu na hazina muhimu sana kwa watu wengi na wala si tu kwa mtu binafsi. Leo hii watu wanachangamotishwa kuishi kwa furaha kwa njia ya kushirikiana na wengine katika maisha, kwani vinginevyo watu watajikuta wanatumbukia katika upweke. Mshikamano wa umoja, upendo na udugu ni rasilimali kubwa na utajiri kwa jamii husika.

Watu wenye ulemavu wanaoshirikiana na wengine katika Jamii wanaweza kushuhudia kwamba, si wapweke na wala hawakuumbwa ili kuishi pweke kama kisiwa, bali ni binadamu wenye kuhusiana na wengine katika Jamii, ili kusaidiana na kuhudumiana kwa hali na mali. Uwepo wa watu wenye ulemavu ni mwaliko wa kuanza mchakato wa ujenzi wa Jumuiya, ili kupokeana na kusaidiana kutokana na mapungufu ya kibinadamu, kwani kila mtu ana uwezo, lakini pia ana mapungufu yake.

Mtakatifu Lucia anawakumbusha walimwengu kwamba, utamu wa maisha unapatikana kwa kuwashirikisha wengine na kwamba, hii ndiyo siri ya furaha ya kweli. Mwanadamu hawezi kupata utimilifu wake kwa kuwa na vitu wala kwa kufanya mambo mengi, bali kwa kupenda na kujisadaka kwa ajili ya wengine!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.