Maandalizi ya Siku ya Familia Kimataifa yaanza kushika kasi!
Baraza la Maaskofu Katoliki Slovacchia, linaendelea kukitumia Kipindi cha Majilio
ambacho kinasheheni, imani, matumaini na mapendo, kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho
ya Siku ya Familia Duniani, itakayofanyika Jimbo kuu la Philadelfia, Marekani, Mwezi
Septemba 2015 kwa ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko.
Baraza la Maaskofu
Katoliki Slovacchia kwa kushirikiana na Jimbo kuu la Philadelphia, limekuwa likiendesha
Katekesi kuhusu maisha ya ndoa na familia; majiundo makini yanayojichimbia katika
kauli mbiu "Upendo ni utume wetu; familia ni utimilifu wa maisha". Katekesi hizi ambazo
zinasambazwa pia kwa kutumia mitandao ya kijamii, zinalenga kuisaidia Familia ya Mungu
nchini Slovacchia, kutambua, kuthamini na kudumisha misingi bora ya maisha ya ndoa
na familia, tayari kutoka kifua mbele ili kuwatangazia Watu wa Mataifa, Injili ya
Familia.
Maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa, ni tukio ambalo linakwenda
sanjari na maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, ambayo awamu yake ya
kwanza tayari imekwisha adhimishwa na sasa waamini wanaendelea kutafakari, ili kuwasaidia
Mababa wa Sinodi kuibua mbinu mkakati utakaoziwezesha Familia za Kikristo kutekeleza
wito na utume wao ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo!
Katekesi hizi
za kina zinapata chimbuko lake kutoka katika: Maandiko Matakatifu, Mafundisho na Mapokeo
ya Kanisa, ili kuonesha utajiri mkubwa wa imani katika Kristo na Kanisa lake kuhusiana
na maisha ya Sakramenti ya Ndoa na Familia. Maaskofu Katoliki Slovacchia wanawaalika
Wakristo kuanzisha na kuendeleza majadiliano yanayohusu: umuhimu wa maisha ya Sakramenti
ya Ndoa na Familia pamoja na changamoto zake, ili kweli waweze kuchangia katika kuenzi
tunu msingi za maisha ya Ndoa na Familia, ambazo kwa sasa zinakabiliwa na changamoto
kubwa kutokana na watu kumezwa mno na malimwengu, kwa kukumbatia utamaduni wa kifo,
mmomonyoko wa tunu msingi za maisha ya kiutu na kimaadili, kwa kisingizio cha uhuru
binafsi.
Ushiriki wa waamini na wadau kutoka sehemu mbali mbali katika Maadhimisho
ya Siku ya Familia huko Philadelfia, inaweza kuwa ni fursa kwa waamini kushirikishana
uzoefu, mang'amuzi, changamoto na matumaini katika mchakato wa kukuza na kudumisha
tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.