2014-12-13 08:30:58

Je, wewe unamfahamu?


Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, kuna furaha na inalipa kweli kweli kumfahamu Yesu Kristo, Mkombozi wa ulimwengu na kuwashirikisha wengine furaha na matumaini haya yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake! Ukitaka kujua utamu wa ngoma, ingia mwenyewe! Mwenye masikio na asikie!

i. Isa 61: 1-2, 10-11. – Unabii wa Isaya unakamilika katika Yesu Kristo.
ii. 1 Thes: 5, 16-24. – Furahini siku zote.
iii. Yoh: 1,6-8,19-28. - Yesu tusiyemjua au kumfahamu.

Majilio ni kipindi cha kujitayarisha kwa ujio wa Bwana kibinafsi na kijumuiya. Yesu anakuja kwetu kisakramenti, katika maisha yetu na katika siku ya mwisho. Hivi sasa tukiambiwa kuwa Kristo yuko hapa katika yetu tungefanya nini? Au ni kwa kiasi gani tunamwonesha Kristo katika maisha yetu, katika jumuiya, na katika kuueneza ufalme wa Mungu?

Mfano wa monasteri moja ambayo ilikuwa kwenye shida kubwa. Baadhi ya watawa wameacha maisha ya kitawa, hakuna watakaji wapya, watu wameacha kwenda mashaurini na maungamo. Wale wachache waliobaki katika monasteri hiyo wanazeeka, wanaendelea kukata tamaa na machungu yanazidi katika mahusiano yao.

Abate anasikia habari juu ya mtu mwema mtakatifu anayeishi peke yake porini. Akaamua kumfuata kwa mashauri. Abate akamwelezea hali halisi ya monasteri yake na kwamba sasa wamebaki watawa saba tu, tena wazee. Baada ya kumsikiliza kwa makini, yule mzee mtakatifu akamwambia ninayo siri moja, nenda kawambie ndugu zako kuwa mmoja wao ni masiha, yuko kati yao na kwamba hata wenzake hawamfahamu.

Kwa ufunuo huu yule abate akaondoka akarudi kwenye monasteri yake na akawaita watawa wenzake na kuwaeleza siri aliyoipata. Baada ya ufunuo huo ikawa sasa shida nyingine kwamba kati yao wanamtafuta masiha kuwa ni nani? Wakaanza kuchambuana mmoja baada ya mwingine. Baada ya mtafaruku huu, kilichobaki ni kuwa waliona kuwa ukweli uko wazi ila wanashindwa kumtambua Masiha.

Tangu siku ile kila mtawa akaanza kumtazama na kukaa na wenzake kama masiha kwa heshima kubwa na uvumilivu wakiwa na ufahamu kuwa huyo mwenzake kuwa ndiye Masiha. Wakapendana zaidi, wakaishi kindugu zaidi na tena watu wakaanza kufurika tena katika monstri ile kwa sala, mashauri na maungamo. Hii tu ni kwa sababu mtu wa Mungu aliwakumbusha kuwa masiha yupo kati yao.

Injili ya leo yatuonesha pia hili. Yohana anatangaza kwa ndugu zake Wayahudi ujio wa masiha. Katika injili ya leo - 1;26-27 - Yohane akajibu akasema mimi nabatiza kwa maji ila kati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi, ndiye yule ajaye nyuma yangu ambaye mimi sistahili kulegeza gidamu ya kiatu chake.

Wayahudi wa wakati ule hawakumtambua masiha kwa sababu wao walimsubiri masiha kadiri walivyofikiri wao. Kwamba masiha angeshuka mara toka mbinguni na nguvu zote, kuuharibu utawala uliokuwepo dhidi ya waisraeli, walisahau hata maandiko yanasemaje kuhusu ujio wake - lakini huyu twamjua atokako ila Kristo atakapokuja hakuna ajuaye atokako. Hivyo alivyokuja kazaliwa na mwanamke hawakumtambua, alikuja katika hali ya kawaida mno na isiyotegemewa..

Je, Yesu yuko wapi hapa? Hili ni swali nililoulizwa binafsi na mwanafunzi baada ya kufundisha somo la dini katika kipindi cha mwaka mzima. Ni swali gumu sana na majibu yake hayahitaji maneno bali ushuhuda. Yohani mbatizaji leo anatupata changamoto kubwa. Anaweka waziwazi utume wake. Katika Isa. 40.3 – tunaona kuwa utume wa Yohani – ni sauti ya mtu aliyae nyikani, tayarisheni njia ya Bwana. Ubatizo wa Yohani ulikuwa na lengo la kuamsha mioyo. Ubatizo wa Yesu – ni mwanzo wa maisha mapya, dunia mpya, hutoa ubatizo wa Roho. Ubatizo wamaanisha kuzama. Na alama ya kuzama huko ni maji. Kwa hiyo mbatizwa huzamishwa katika Mungu, katika Mwana na katika Roho Mtakatifu.

Roho mtakatifu hutoa nini kwetu? Katika barua - Rom. 5: 5- tunasoma hivi - lakini matumaini hayadanganyi, kwa maana upendo wa Mungu umeenezwa mioyoni mwetu na Roho Mtakatifu tuliyempokea. Katika ubatizo ambapo tunaingizwa katika ushirika wa Utatu Mtakatifu, tunapata pendo kamili la Mungu. Hii inamaanisha kuwa tunapata uwezo wa kupenda kama Mungu Baba alivyotupenda/anavyopenda kwa njia ya Roho Mtakatifu afanyaye kazi ndani yetu. Ni roho huyo anayetusaidia kumjua Mungu na roho wake. Bila huyo Roho wa Mungu, hatutaweza kumtambua Kristo katika maisha yetu. Lakini tuendelee kutambua kuwa kila mmoja wetu ana wajibu wa kumwonesha huyu Kristo tunayemwamini.

Imetayarishwa na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.