Umaskini ni kikwazo cha maendeleo nchini Zimbabwe!
Viongozi wengi wa Zimbabwe wanagombania madaraka na kusahau kwamba, kuna maelfu ya
wananchi wa Zimbabwe wanaoogelea katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato na kwamba,
umaskini ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya wananchi wengi wa Zimbabwe. Kuna maelfu
ya wananchi wa Zimbabwe wamekimbilia katika nchi jirani kama vile: Botswana, Msumbiji,
Zambia na Afrika ya Kusini ili kutafuta riziki ya maisha.
Kwa wananchi waliobahatika
kutoka nje ya Zimbabwe wanaendelea kuzisaidia familia zao kwa kuwatumia fedha, lakini
si kila familia imebahatika kuwa na fursa hii! Lakini viongozi wa Kidini wanapozungumzia
hali ya umaskini na ukosefu wa haki msingi za binadamu nchini Zimbabwe wanatishiwa
maisha na wakati mwingine wanakiona cha mtema kuni! Viwanda vingi vimefungwa; mashamba
yaliyotaifishwa na Serikali yamegeuka kuwa ni misitu ya wanyama pori.
Padre
Felix Tachiona Mukaro kutoka Zimbabwe katika mahojiano maalum na Shirika la Kipapa
la Misaada kwa Makanisa hitaji anasema kwamba, wananchi wengi wa Zimbabwe hawatarajii
kupata mabadiliko makubwa ya kisiasa katika kipindi kifupi, lakini jambo la msingi
ambalo linapaswa kupewa msukumo wa pekee ni mabadiliko ya kifikra; kwa kutoa kipaumbele
cha kwanza kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; mambo yanayojikita katika utu
na heshima ya binadamu pamoja na kuheshimu haki zake msingi.
Kanisa nchini
Zimbabwe linaendelea kuchangia katika ustawi na maendeleo ya wananchi kwa kutumia
rasilimali yake "kiduchu" iliyopo kwa wakati huu. Lakini hata Kanisa pia linakabiliwa
na hali ngumu ya uchumi, lakini bado liko imara katika kuwatangazia watu waliopendeka
na kuvunjika moyo, Injili ya Matumaini.