Ukatili ni vitendo vya kinyama, haviwezi kukubalika!
Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linaungana na viongozi wa dini mbali mbali nchini
humo kulaani mbinu za ukatili zilizotumiwa na Shirika la Ujasusi la Marekani, CIA,
katika kupambana na watuhumiwa wa vitendo vya kigaidi. Askofu Oscar Cantù, Mwenyekiti
wa Tume ya Masuala ya Kimataifa ya haki na amani anasema kwamba, Kanisa linaamini
na kulaani vitendo vya ukatili kwa kuwa ni dhambi na kamwe, haviwezi kuhalalishwa
kwa misingi yoyote ile.
Senate ya Marekani, hivi karibuni imepokea taarifa
inayoonesha jinsi ambavyo CIA ilivyowanyanyasa na kuwatesa watu waliokuwa wanashutumiwa
kwa vitendo vya kigaidi, mambo ambayo yanakwenda kinyume cha utu na haki msingi za
binadamu. Senate ya Marekani inamtaka Rais wa nchi kuimarisha utawala wa sheria ili
vitendo vya ukatili ambavyo vimeidhalilisha Marekani katika uso wa dunia visitokee
tena.
Taarifa inaonesha kwamba, tangu yalipotokea mashambulizi ya kigaidi hapo
tarehe 9 Novemba, Marekani imekuwa ikitumia ukatili mkubwa kwa watu waliokuwa wanashukiwa
kuhusika na vitendo vya kigaidi.