2014-12-11 08:21:32

Ibada kwa Bikira Maria wa Guadalupe ni moto wa kuotea mbali!


Baba Mtakatifu Francisko, katika maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria wa Guadalupe, Msimamizi wa Amerika ya Kusini, inayoadhimisha kila mwaka ifikapo tarehe 12 Desemba, anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vaticanili kuomba maombezi na ulinzi wa Mama Bikira Maria wa Guadalupe.

Lengo ni kuombea mchakato wa Uinjilishaji mpya miongoni mwa waamini wa Amerika ya Kusini; ili waweze kukua na kuimarika kiutu, daima wakijitahidi kujikita katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika msingi wa: haki, amani, umoja na mshikamano wa dhati. Kwa namna ya pekee, maadhimisho haya ambayo ni moto wa kuotea mbali, yanafanyika kwa namna ya pekee nchini Mexico na maeneo ambayo Ibada kwa Mama Bikira Maria wa Guadakupe imeenea kwa kiasi kikubwa.

Ibada hii ya Misa Takatifu inatarajiwa kuanza saa 12:00 jioni, lakini itatanguliwa na maandamano ya bendera kutoka katika nchi mbali mbali za Amerika ya Kusini, ili kutoa heshima kwa Bikira Maria wa Guadalupe, baadaye waamini watasali Rozari Takatifu, itakayosindikizwa kwa nyimbo kutoka Amerika ya Kusini.

Maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria wa Guadalupe kwa Mwaka huu yanachukua maana ya pekee kwa kushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko, ambaye kwa asili ni kutoka Amerika ya Kusini. Baba Mtakatifu ana ibada ya pekee kwa Bikira Maria, tangu achaguliwe kuliongoza Kanisa amekwenda kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu mara kumi na sita, ili kutoa heshima yake kabla ya kuanza matukio makuu katika maisha na utume wake.

Bikira Maria wa Guadalupe ni kielelezo cha Mama mfariji anayetembea pamoja na watoto wake na kushiriki nao furaha na matumaini; mateso na mahangaiko ya ndani; ni Mama anayependa kuwakumbatia wote chini ya ulinzi na tunza yake ya Kimama. Ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutetea na kuitangaza Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Watu waoneshe moyo wa upendo, ukarimu na mshikamano kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta maana ya maisha, bila ya kuwasahau maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kutambua kwamba, Amerika ya Kusini kimsingi ni Bara ambalo limesheheni ukarimu.

Waandaaji wa tukio hili wanasema, moto wa upendo na Ibada kwa Mama Bikira Maria wa Guadalupe utawashwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican Ijumaa, tarehe 12 Desemba 2014. Viongozi wakuu kutoka Vatican na wanadiplomasia wanaowakilisha nchi za Amerika ya Kusini wanatarajiwa kuipamba siku hii ambayo itashuhudiwa pia na waamini kutoka Jimbo kuu la Roma pamoja na watalii kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko inatarajiwa kutangazwa moja kwa moja kutoka Vatican kwenye nchi kadhaa za Amerika ya Kusini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S,
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.