2014-12-11 09:16:00

Achana na Yohane Mbatizaji! Anatishaaa!


Mara nyingi tunasikia toka vyombo vya habari kwamba kuna watu wanashikiliwa na Polisi kwa uhalifu na wengine wamekamatwa ili kuisaidia vyombo vya dola kufanya upelelezi. Mashahidi wa mahakamani wanategemewa kutoa ushuhuda jinsi kituko au uhalifu ulivyotokea.

Kutokana na makashkash za mahakamani watu wengi wanatoroka kuweko sehemu za tukio wasije wakashikwa kuwa mashahidi. Hebu leo tumfuatilie jamaa mmoja aliyeshikiliwa na Mungu ili atoe ushuhuda wa kituko kimoja kilichojili hapa duniani. Tunaambiwa kuwa, “Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohane. Huyo alikuja kwa ushuhuda.”

Yohane ndiye mtu huyo aliyeshikiliwa na Mungu kwa malengo ya kutoa ushuhudia. Yohane mwenyewe alijua ni kwa malengo aliyotumwa kufanya hapa duniani na alitambua makashkash yanayoweza kumjiri kutokana na kuwa shahidi. Maana ya jina la mtoa ushuhudi linashuhudia ni kitu gani, amekuja kushuhudia, kwa sababu kila jina linatakiwa kuitambulisha hadhi ya mtu.

Jina hili Yohane linatokana na lugha ya kihebrania Yohanan lenye maana ya “Mungu ni upendo.” Hivi mbatizaji amezaliwa duniani kwa malengo ya kuushuhudia upendo. Injili nyingine zinamchora Yohane kuwa ni mtangulizi, anayeandaa ujio wa masiha, anawaandaa watu kusubiri kule kutekelezeka kwa unabii wa Agano la Kale, hasa namna ya kumpokea masiha. Kumbe mwinjili Yohane anamwonesha Yohane Mbatizaji kama shuhuda, yaani mtu anayeshuhudia.

Hiyo ndiyo hatua ya kwanza na katika hatua hii tunaweza kuanza kujiuliza: “Mimi ni nani na nimetumwa hapa duniani kwa ushuhuda gani, na niushuhudie vipi uwepo wangu. Kadhalika yatakiwa nijihoji ninaitwa jina gani ambalo Mungu anaweza kulifahamu. Mungu ni upendo na analinganishwa na Mwanga au nuru ambayo Yohane aliishuhudia. “Yohane alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa yeye. Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru.” Mwanga ni kitu kizuri hata jicho linapenda kuuona mwanga na kilikuwa kitu cha kwamza kuumbwa.

Kuona mwanga maana yake kuzaliwa, kadhalika ni alama ya uzima. Watu wanapoamkiana wanajibu “Tupo bado tunaona mwanga au kumekucha”. Mbatizaji anao utume muhimu, na mara tatu yasema kwamba amekuja kuushuhudia mwanga. Yohane anatolea ushuhuda mwanga huo mbele ya watu wenye mamlaka, mbele ya wanafunzi wake na mbele ya watu wote.

Yesu akiwa kama mtu mwenye umbo la kibinadamu alikuwa anaonekana na kila mtu, uso wake haukufichika na watu wote walikuwa wanauona. Katika mtazamo wa kawaida, tungeweza kusema kuwa Mbatizaji alikuwa anaona kitu kile ambacho watu wote walikuwa wanakiona kwa macho yao ya kawaida. Kwa hivyo, kama Yesu ni Nuru basi watu wote waliweza kuiona Nuru hiyo lakini hawakuitambua. Kumbe Yohane Mbatizaji alikuwa anamtazamo mwingine wa mambo, kutokana na uwezo aliopewa na Roho na mwanga wa Mungu aliweza kuona zaidi ya pale wanapofikia kuona wengine kwa macho yao ya kawaida, kama ilivyoandikwa “Wenye heri wale wanaoona kile mnachoweza kukiona ninyi.”

Vivyo hivyo, tunaweza kusema juu ya maisha yote ya Yesu hata ujumbe aliotoa, siyo wote walibahatika kuutambua. Ingawaje Yesu alifanya mambo yake hadharani bila mficho, watu wengi walishuhudia lakini walitoka mbukwa, kwani waliyaona kwa jicho la kiyakinifu, yaani kwa macho ya kawaida.

Tungeweza kusema kwamba Yohane Mbatizaji aliyekuwa kwenye tukio, akaishuhudia hiyo nuru kwa jicho la roho. Na akawa tayari kutumwa kutekeleza kazi ya kuishuhudia nuru hiyo. Huo ndio mwito tunaoalikwa kuushuhudia sisi, kwanza namna ya kuiona hiyo nuru kama alivyoona mbatizaji. Kwamba Mungu ni upendo na upendo huo unauona katika Kristo.

Kisha kuna ujumbe uliotumwa na viongozi wa Yerusalemu waliofika kumwuliza Yohane ni nani. Yohane alijulikana sana nchini pengine kumpita hata Yesu. Haiba ya Yohane iliweza kumtisha hata Herode Antipa, aliyeogopa kwamba Mbatizaji angeweza kuhamasisha watu kufanya hata mgomo au mapinduzi fulani na watu wangemsikiliza. Kadhalika watu wa dini – makuhani – walikuwa na wasiwasi naye kwa sababu, wengine walimdhani kuwa labda ndiye Masiha mwenyewe.

Kama anavyosema nabii Malakia kwamba Masiha ajaye angeisafisha dini na kuiweka sawa hasa kulitakasa hekalu, kwani humo kulikuwa kunatendeka madhambi mengi. Ndani ya hekalu kulikuwa na utapeli, rushwa ilikithiri hadi kufikia kiasi cha kupanga duka la kubadilisha pesa na biashara ndogondogo ndani ya Hekalu.

Hivi hata nao waliogopa, wakaenda kumwuliza: “Wewe ni nani?” Lakini yeye anaungama na kushuhudia waziwazi kwamba: “Mimi siyo Kristo”. Hapa hata sisi tunaweza kujiuliza je, tuna hadhi na nafasi gani, ili tusiweze kukosea kushuhudia wito na utume wetu. Tusije tukachukuliwa na upepo tukapitiwa na kushindwa kushuhudia utu wetu. Tusijiachilie kutekwa na watu wenye wivu, watu wabaya, bali tuongozwe na nuru ambayo ni Kristo. Wanaendelea kumwuliza “kama wewe siyo Masiha basi ni nani? Je, ni nabii Eliya?” Mbatizaji anajibu kwamba siyo yeye. Kisha wanamwuliza swali zuri linaloweza kuwa fundisho kwetu “Unasema nini juu ya wewe mwenyewe.” Maana yake wewe ni nani? Unajifahamu vipi.

Hapa hutakiwi kutoa kitambulisho au kuonesha uso wako, bali wewe mwenyewe unajishuhudiaje. Unajiju vipi? Yohane anajijua yeye ni nani hivi anajibu: “Mimi ni sauti ya mtu anayeshuhudia huko jangwani.” Katika kipengee hiki yaonekana maelezo sahihi yangeweza kuwa yale ya mt. Augustino pale anapotofautisha kati ya sauti na neno.

Sauti ni ile inayosikika mtu anapoongea. Hiyo inadumu kwa muda fulani halafu inapotea. Lakini sauti inaacha neno au ujumbe. Sauti yatakiwa ififie na neno libaki. Sisi wabatizwa tuko hapa duniani kama sauti, inayoshuhudia kwamba Yesu ni mwanga unaoangaza gizani. Hiyo ndiyo tabia tunayotakiwa kuwa nayo. Kama tunaongea tu na kutoa sauti kuhubiri, juu ya mwanga bila kushuhudia kwa matendo katika maisha yetu hapo sauti hiyo haiwakilishi ujumbe wowote ule bali inakuwa ni “debe tupu haliachi kutika.”

Wanamwuliza tena “kwa nini basi unabatiza kama wewe siyo Masiha?” Lakini yeye anajibu kwamba mimi ninabatiza kwa maji. Maana yake ni alama inayopita inayomaanisha kuacha mambo ya kale ili kuanza maisha mapya. Ubatizo wake ni wa kuwafanya watambue kwamba, wanaishi katika giza. Sisi leo hatupokei ubatizo wa Yohane, lakini ni alama inayoweza kutufaa hata sisi leo.

Endapo uko gizani, basi kumbuka kwamba inabidi ufanye mang’amuzi haya ya ubatizo yaani, kusikiliza ujumbe wa Yohane na kufanya ubatizo wa mpito kutoka gizani na kuingia mwangani. Kisha Yohane anaendelea kusema: “kati yenu kuna mwanga, na ambao hamuufahamu. Fungueni macho ya kiroho muweze kumwona kwani nuru hiyo iko kati yetu. Iko kati ya watu wanaoifahamu na wanaoiishi hiyo nuru, yaani watu wanaofaulu kuunganisha maisha yao na mwanga. Kwa hiyo leo Yohane anatuandaa kujijua sisi ni nani, kuipokea nuru hiyo na kuishuhudia katika maisha yetu.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.