2014-12-10 15:52:21

Ujumbe wa Papa kwa ajili ya Siku ya amani duniani: hakuna mtumwa sote ni kaka na dada


Katika ukumbi wa Yohane Paulo II wa mjini Vatican, Jumatano hii majira ya adhuhuri, kulifanyika mkutano wa waandishi wa habari kwa ajili ya kuwasilisha ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko, kwa adhimisho la 48 la Siku ya kuombea amani duniani, ambayo hufanyika kila mwaka Januari 1Mosi. Kwa mwaka 2015 ujumbe huo unaongozwa na Kauli mbiu: "Hakuna mtumwa, sote ni ndugu, kaka na dada."

Katika uwasilishaji huo, Wazungumzaji wakuu walikuwa ni Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Haki na Amani, na Katibu wa Baraza hilo Mons. Mario Toso, SDB, Pia Dk Victor V. Alberti, na Sr. Gabriella Bottani, wa Shirika la Wakomboni,anayeshughulika na Mtandao wa Kimataifa wa Watawa kike dhidi ya Usafirishaji haramu wa Binadamu (UISG) .

Kardinali Peter Turkson,akitoa mchango wake , katika uwasilishaji huu amesema kwamba, ujumbe wa Papa Francisco kwa ajili ya tukio hili, ni mwendelezo wa tafakari juu ya Ujumbe wake alioutoa siku ya Amani Dunia 2014 juu ya mada: udugu, ni msingi katika njia ya amani, ambamo Papa anaona udugu una mahusiano ya karibu na amani. Kwa mtazamo huo, kaichagua kaulimbiu ya ujumbe wake kwa mwaka 2015 kuwa: hakuna tena mtumwa, lakini wote ni ndugu. Papa anaona uhusiano wa karibu uliopo katika hali halisi za utendaji wa maisha ya kila siku akiainisha na mshikamano, udugu na amani.

Kardinali anasema , ujumbe mpya wa Papa ni mwaliko wa kuwa na mbadiliko chanya katika mahusiano ya kijamii, kutoka katika uhusiano tegemezi wa utumwa, wenye kunyakua utu wa wengine, na kujenga uhusiano wa udugu, maisha ya kutetea heshima ya utu wa mtu na haki sawa kwa kila binadamu , umoja kati ya watu, kwa hoja msingi kwamba, wote ni watoto wa Baba mmoja.

Papa ameyaita mabadiliko haya kuwa ni njia ya ya wongofu inayowaongoza waaamini katika kuwatambua wengine kama ndugu na si adui, hakuna mtu mwenye hadhi ya chini, au mtu wa kudharuliwa na kuchezewa kama vile ni bidhaa , lakini kila binadamu ni ndugu , kaka au dada mwenye kuwa na stahili zote za kupendwa kwa sababu upendo hufungua minyonyoro yote ya utumwa.


Maelezo ya Baba Mtakatifu Francisko, yamelenga zaidi katika barua ya Mtakatifu Paulo kwa Filemoni, na aya zingine za Biblia, ambazo zinaonyesha kwamba katika mpango wa Mungu, kwa ajili ya wanadamu, hakuna nafasi ya utumwa kwa wengine, kwa sababu Mungu anawaita wote kuwa watoto wake. Wote wamefanywa upya katika mahusiano yao, kuheshimu katika kila mmoja, kwa kuwa kila mmoja ana sura na mfano wa Mungu, hata wale wanaoonekana kuwa ni wadogo na wanyonge, wakiwemo waathirika wa ndoa za kulazimishwa na wale ambao wameingizwa katika baishara haramu ya uhahaba na kwa ajili ya kutoa "faraja ya ngono n.k.







All the contents on this site are copyrighted ©.