2014-12-10 14:43:37

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Majilio


Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican kipindi cha tafakari, ninakuleteeni tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya tatu ya Majilio. Masomo ya Dominika ya tatu daima hutupa ujumbe wa FURAHA. Ndiyo kusema tunaalikwa kufurahi daima katika kuishi imani yetu. RealAudioMP3

Wimbo wa kwanza katika litrujia ya Misa Takatifu unaoimbwa hivi, furahini katika Bwana siku zote, tena nasema furahini Bwana yu karibu ni ufupisho kamili wa ujumbe wa Neno la Mungu katika Dominka hii. Basi mpendwa, fungua moyo wako ukaianze siku na Dominika hii kwa uchangamfu wa moyo katika Bwana.

Katika masomo tukianza na lile la kwanza Nabii Isaya anawaalika wana wa Israeli katika furaha hiyo kwa maneno ya kutia moyo, maneno ya kuwatia nguvu ili kujenga tumaini yakwamba siku moja wataondolewa utumwani Babeli, watarudi nyumbani. Ujumbe wa tumaini anawapeni kwa maneno ya furaha akisema Roho wa Bwana amenitia mafuta niwahubirie maskini habari njema, niwagange waliovunjika moyo na kisha kuwatangazia mateka uhuru na zaidi kutangaza mwaka wa Bwana, mwaka wa furaha.

Kama wewe na mimi tungekuwa katika utumwa huo tungefurahi na kurukaruka kama Waisraeli. Leo hii tuko katika utumwa gani? Tuko katika vifungo vya dhambi kiroho, na hivi Masiya anakuja na kutangaza ukombozi toka mikasa hiyo, kwa nini tusifurahi? Tunapaswa na tunaalikwa kurukaruka na kuchangamka. Kuchangamka hakutakuja kama tutaiweka mbali nasi sacramenti ya Kitubio mlango safi, mlango mwembamba kwa ajili ya Ekaristia, umisionari na maisha ya uzima wa milele.

Nabii Isaya anasema tena “nitafurahi sana katika Bwana, nafsi yangu itashangilia katika Mungu wangu, maana amenivika vazi la wokovu. Furaha hii ya Nabii Isaya ni furaha ya kweli kwa maana anaondolewa katika dhiki ya dhambi. Nasi twaweza kufurahi lakini ili tuweze kupata furaha ambayo Masiya atatuletea inatupasa kuwa na moyo wa subira, matumaini, majitoleo toba na uwajibikaji kiroho na kimwili. Ndiyo kusema kuwa na moyo mnyoofu ambao hupokea yote kwa uchaji na furaha.

Kwa namna ileile ambayo Nabii Isaya anawaimarisheni Wana wa Israeli, Mtume Paulo anapowaandikia Watesalonike anawashauri daima waweni watu wa furaha na matumaini. Ndiyo kusema wanapomgonja Bwana wamngoje kwa furaha na wala si kwa kununa na kusikitika daima. Anawataka wapate furaha katika maisha ya sala, shukrani kwa Mungu na daima kumkaribisha Roho Mtakatifu ndani mwao. Kumkaribisha Roho Mtakatifu ni kujitenga na dhambi na kila aina ya ubaya katika maisha ya kila siku. Ni katika kuishi furaha hiyo Mama Kanisa katika mwaka huu anatualika kuungana na Watawa kuwa chachu ya Injili, tukiifanya ipenye katika jumuiya tunamoishi kwa njia ya unabii wetu na hivi kwa namna hiyo itaweza kuzaa matumaini mapya.

Mwinjili Yohane anatupatia namna nyingine ya kujipatia furaha, nayo ni kuwa ushuhuda kwa nuru, na nuru hii ni Kristo Mwana wa Mungu aliye katikati yetu ambaye mara kadhaa hatumfahamu vema. Ni kujishusha kama Yohane Mbatizaji ambaye mbele ya Mwana wa Mungu anaona yeye si kitu, ananyenyekea mbele ya mwumba wake. Yeye ni chombo cha Mungu, sauti iliayo nyikani- itengenenezeni njia ya Bwana. Hili ni fundisho kubwa kwa wanaojikweza ili waweze kuiga mfano wa Yohane mbatizaji na watakatifu wengine kama Mt Yosefu na zaidi sana Mama Mtukuka, Mama wa Mungu anayesema daima “mimi ni mtumishi wa Bwana nitendewe kama ulivyonena”. Ni fundisho na mwanga kwa wale wanyenyekevu ambao wanaalikwa kupiga hatua nyingine katika maisha yao ya kiroho wakikumbuka fundisho la Mt Paulo asemaye “siyo kwamba nimekwishakamilika bali nakaza mwendo ili niweze kulifikia lile taji”.

Habari nzima iliyo ya furaha imelala katika wokovu wetu ambao unakuja kwa njia ya Kristo, Mwana wa Mungu. Kumbe kazi ya kufurahi ni kushikamana na wokovu huo siku zote. Ni kujitahidi kugundua huyu Kristo anakuja namna gani kwetu na anataka tufanye nini, yaani tuishi mapendo. Tusome Neno lake, tupokee sakramenti na tushikamane na uongozi wa Kanisa takatifu. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.